Zaidi ya maboma 900 yamejengwa kwa nguvu ya wananchi

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange

Muktasari:

  • Ukamilishaji wa maboma ya zahanati nchini wawaibua wabunge kuihoji Serikali ina mpango gani wa kuyakamilisha.

Dodoma. Serikali imesema katika kipindi cha miaka mitatu imemalizia maboma ya zahanati zaidi ya 900 yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Oktoba 31, 2023 na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalumu Ester Bulaya.

Bulaya amesema tatizo la maboma limekuwa kero nchi nzima na muda mrefu tangu mwaka 2010 na kuhoji Serikali imefanya utafiti kwa hiyo ni yapi yanaweza kutengenezeka.

Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema ni kweli kumekuwa na maboma mengi katika vijiji vyetu kwa ajili ya zahanati lakini katika kipindi hiki cha miaka mitatu maboma zaidi ya 900 yamekamilishwa.

“Kazi ya Serikali ni kutambua maboma yanayokidhi vigezo vya kuendelea kukamilishwa na fedha zinaendelea kutengwa na mwaka huu wa fedha Sh90 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma hayo,”amesema.

Amesema wamefanya utafiti na wataendelea kukamilisha kwa awamu.

Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM) Mwita Waitara amehoji ni hatua gani Serikali inachukua kwa watu ambao wamekuwa wakipita katika majimbo yao wanaowapotosha wananchi wasishiriki katika maendeleo kwa kuchangie kwenye ujenzi wa maboma ya shule na zahanati.

Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema utaratibu wa ujenzi wa maboma ya zahanati kwa utaratibu wa mpango wa afya ya msingi upo kwa mwongozo wa 2007.

Amesema ni maamuzi ya Serikali kuwa wananchi wanashiriki kwa sehemu na Serikali inahitimisha

 “Kwa hiyo kama wapo watu wanapita katika maeneo yetu na kupingana na maelekezo ya Serikali basi nawaomba Serikali kwa maana wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya wawatambue watu hao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,”amesema.