IGP Wambura ataka wazazi kuimarisha malezi kuzuia vifo vya watoto

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camillus Wambura akizungumza katika Parokia Kuu ya Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki Moshi mkoani Kilimanjaro

Muktasari:

  • Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania(IGP), Camillus Wambura amewaasa wazazi na walezi kuimarisha malezi katika ngazi ya familia na kutimiza wajibu wao wa ulinzi wa mtoto, ili kuepusha vifo visivyo vya lazima ambavyo vimekuwa vikichangiwa na uzembe.

Moshi. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camillus Wambura amewataka wazazi na walezi kuimarisha malezi katika ngazi ya familia na kutimiza wajibu wao wa ulinzi wa mtoto, ili kuepusha vifo vinavyochangiwa na uzembe.

Wambura ametoa wito huo leo Aprili 14, 2024 alipozungumza katika Parokia Kuu ya Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi mkoani Kilimanjaro na kusema ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata malezi sahihi, ili wafikie ndoto zao za kimaisha.

Amesema katika kipindi cha hivi karibuni, watoto wengi wamepoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kusombwa na maji, kuzama kwenye madimbwi wakati wakiogelea na hata wengine wamefariki kutokana na uzembe wa wazazi, walimu na hata madereva wa shule.

Hivyo, amesema kuna haja ya wazazi na walezi  kuhakikisha wanazingatia malezi sahihi na kumlinda mtoto.

“Kwetu sisi polisi, nafahamu kuna maofisa wetu ngazi ya kata na nyingine, wanaendelea kutoa elimu kuhusu malezi ya watoto, lakini pia wanatoa elimu kuhusu upendo, mshikamano na ushirikiano katika ngazi ya familia hadi Taifa.

“Ninawaomba ndugu zangu katika ngazi ya familia, muende mkadumishe upendo na mkatoe malezi sahihi kwa watoto wetu,” amesema na kuongeza;

“Watoto wetu wadogo kipindi hiki wengi wamepoteza maisha kwa sababu ya kusombwa na maji, kuzama kwenye madimbwi wakiogelea lakini wengine wamefariki ama kwa uzembe wa wazazi hata walimu na madereva wa shule kama ilivyotokea. Hivyo, twendeni tukawaangalie watoto wetu, wanahitaji malezi na mwongozo wetu kama wazazi.”

Pia amezitaka familia kuimarisha upendo na mshikamano miongoni mwao, ili kuepusha mifarakano itakayosababisha athari kwa watoto na kuchochea ongezeko la watoto wa mitaani katika jamii.

“Kenye ngazi ya familia, kuna mume na mke, twende tukadumishe upendo katika ndoa zetu, kwa sababu kama ndoa hizi zinafika mahali zinaparanganyika, ndipo tunakwenda kupata watoto wa mitaani ambao mara nyingine wanajihusisha na uhalifu na si kwa mapenzi yao bali kutokana na hali halisi wanayokutana nayo,” amesema.

Akizungumza katika ibada hiyo, Padri Josephat Charles amewataka waumini kuacha dhambi, kutoa taarifa za uhalifu na kuwa sehemu ya kufanya mabadiliko kwa kulinda familia zao, huku akiwaasa wazazi kuwa makini na watoto hasa katika malezi.

“Wazazi tumrudie Mungu, tuwatoe watoto wetu walipo na kuwaleta kwa Mungu ili ashughulike nao, tupate muda mwingi wa kuwaombea, kuwaonya na kuwaelekeza hasa kwenye mitandao ya kijamii, hawaelewi faida yake wala hawapati chochote chema,” amesema.