Nchi Afika Mashariki zatakiwa kuwekeza kwenye malezi, makuzi ya mtoto

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, akizungumza  katika mkutano wa kimataifa wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.

Muktasari:

Sayansi ya malezi na makuzi ya mtoto inaeleza kuwa, ubongo wa binadamu unakua na kufikia hadi asilimia 90 katika umri wa miaka 0, yaani mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake hadi miaka minne.



Herieth Makwetta, Mwananchi

Dar es Salaam. Nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zimetakiwa kutenga bajeti ya kutosha kushughulikia malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, ikiwa ni uwekezaji katika lishe, afya na usalama wa mtoto.

Wakati zikitenga bajeti hiyo, zimetakiwa kuhakikisha elimu inatolewa kupambana na migogoro ya kifamilia na matumizi ya vifaa vya kielektroniki vinavyotajwa kuwa kikwazo kwa kundi la watoto.

Wito huo umetolewa leo Jumatatu, Machi 11, 2023 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.

Dk Gwajima amesema katika kutekeleza hayo kila nchi iende ikaangalie inatenga bajeti kiasi gani katika eneo hilo, akizitaka zijitathmini na ziweke nguvu katika uwekezaji kwa mtoto.

"Lakini, tafiti mbalimbali zilizofanyika hapa Afrika zimebaini uwekezaji kwenye malezi na makuzi ya watoto wadogo bado ni mdogo na hauna uwiano ulio sawa kama unavyobainishwa na sayansi ya malezi ya watoto.

"Hali hii ikiendelea tutakuwa tunaandaa watoto na hatimaye nguvu kazi isiyo na tija kwa mataifa yetu. Naomba kutoa wito kwa mataifa kuimarisha uwekezaji kwa watoto wadogo kwa kutumia mapato ya serikali zetu. Wadau, watusaidie katika eneo hili muhimu," amesema Gwajima.

Aidha Dk Gwajima ametoa wito kwa nchi za ukanda huo kuja na mbinu bora na afua kwa kuzingatia mila na desturi za Kiafrika pindi wakimaliza mkutano huo wa siku nne.

Katika hotuba yake,  mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani  hapa nchini, Dk Charles Moses amesema kwa zaidi ya miaka 40, WHO kwa ushirikiano na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine kadhaa, wamekuwa wakijitahidi kusukuma ajenda ya maendeleo ya mtoto.

Amesema lengo la Maendeleo Endelevu la 4.2 linaeleza kuwa ifikapo mwaka 2030 nchi zinapaswa kuhakikisha kuwa wasichana na wavulana wote wanapata maendeleo bora ya utotoni (ECD).

Amesema, duniani inakadiriwa kuwa watoto milioni 250 hasa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, wako katika hatari ya kutofikia ukuaji wao kamili.

"Kuweka mazingira mazuri na endelevu kwa watoto wadogo kufikia uwezo wao kamili wa maendeleo,  ni haki ya msingi ya binadamu ambayo ni muhimu kwa ukuaji endelevu wa uchumi," amesema.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema lugha ina nafasi kubwa na inachangia katika malezi na makuzi bora kwa watoto.

"Lazima tutambue nafasi ya lugha katika kumsaidia mtoto kukua, kama mzazi hayupo katika mazingira mazuri au hana utashi katika kuzungumza changamoto inaanzia hapo, kwani msingi wa jambo lolote unaanzia ngazi ya chini," amesema.

Chalamila ametaja jambo jingine kuwa ni mazingira ya kumkuza mtoto.

 "Kumekuwa na suala la kuzungumza kuhusu watoto wa mitaani, hakuna mtaa unaozalisha watoto lakini ni migogoro ya kifamilia inasababisha haya, "amesema.