Kauli sita zinazochangia kuharibu malezi, makuzi ya watoto nchini

Muktasari:

  • Wazazi, viongozi wa dini wataka mtoto awe wa jamii wakikemea maisha ya usasa, kuiga ya Magharibi. Shule binafsi zamulikwa kudekeza watoto.

Moshi. Wakati Serikali ikitoa waraka maalumu wa usimamizi wa maadili kwa wanafunzi kuanzia shule za awali hadi sekondari, wadau wa elimu nchini wamezitaja kauli sita za baadhi ya wazazi zilizoifanya jamii ijiweke kando kuwakemea watoto.

 Katika waraka huo namba sita wa mwaka 2022 uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuanza kutumika Oktoba 10, Serikali imetoa maelekezo 11 inayoamini yakitekelezwa maadili yataimarika.

Maelekezo hayo ni pamoja na shule zote kuanzisha au kuimarisha kamati za maadili na nidhamu kwa usimamizi wa karibu wa walimu wakuu na wakuu wa shule ili zijenge tabia na maadili kwa wanafunzi.

Maofisa elimu kata washirikiane na viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji kuhakikisha mazingira wanamoishi na kukulia watoto hayana vyanzo vya taarifa zinazoharibu maadili mfano wa vibanda umiza.

Hata hivyo, wadau wa elimu, wakiwamo wazazi, walimu na viongozi wa dini wamebainisha kauli sita ambazo kama hazitadhibitiwa basi jamii itaendelea kujiweka kando kumkemea mtoto anapokosea.

Kauli hizo ni pamoja na “unajua uchungu wa kuzaa, unajua niliyoyapata leba” au “unamfuatilia sana mwanangu wewe, zaa wako umfuatilie” na “unamchapa mwanangu, zaa wako umgeuze ngoma.”

Kauli nyingine ni “mwache afanye analotaka, kama unaona ni tabia mbovu mfundishe mwanao,” “mwacheni afanye analotaka, nyinyi inawahusu nini” na “mtoto wangu haguswi wala hachapwi, kama unapenda kupiga zaa wako.”

Kauli hizo na nyingine zinazofanana na hizo zinaelezwa kuchangia kuporomosha maadili ya watoto na kuifanya jamii ijiweke kando kumkemea na kumwadhibu mtoto anapokosea mtaani ili kumjengea nidhamu.


Mazito ya viongozi wa dini

Akizungumzia suala hilo, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kiborilon Dayosisi ya Kaskazini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fred Njama alisema ili kurudi kwenye mstari, mtoto anatakiwa awe wa jamii sio wa mzazi pekee.

“Wazazi wa zamani walikuwa wanakaa na watoto hata akikosea huko barabarani aliye jirani angeweza kumkemea au kumwadhibu, lakini sasa hivi hali ni tofauti. Turudi kama zamani, mtoto awe wa jamii,” alishauri mchungaji.

Hata hivyo, Mchungaji Njama alisema mmomonyoko wa maadili wa watoto umechangiwa na watu wazima wenye hadi miaka 60 kuwa na uhusiano na watoto wadogo wenye mpaka miaka 15, hivyo anapotokea wa kumkemea mtoto anakuwa mkali.

“Kwa hiyo mzazi mwingine mtaani akimuona amefanya jambo ambalo si sawa akimkemea anaona ameonewa kuitwa mtoto kwa sababu ana mahusiano na babu wa miaka 60 au 70. Turudishe maadili ya zamani, tutavuka,” alisisitiza.

Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa Kilimanjaro, Awadhi Lema alisema wakati wanakua katika rika lake, kila mwanamume alikuwa baba na mwanamke alikuwa mama.

“Hii ilifanyika bila kujali amekuzaa au hajakuzaa, bila kujali ni kabila gani au rangi gani na yeyote aliyekuwa mkubwa kwako alikuwa kaka yako au dada yako. Lakini siku hizi kila mtoto ana mwenyewe anaishi maisha ya wazazi wake,” alisema lema na kuongeza:

“Sasa hivi mzazi anajiona ndio anajua kulea kuliko watu wote na wengine wote hawajui malezi na ikitokea mtoto anafanya mambo yasiyokuwa na maadili njiani na akikanywa inakuwa shida kwa aliyemkanya.”

Jambo jingine linaloharibu tabia za watoto na kuwajengea kiburi alisema ni shule za binafsi kwamba baadhi zinawadekeza kwa kuwapa maadili ya kizungu, jambo ambalo ameshauri Serikali iliangalie kwa jicho la ziada.

Mchungaji mwingine wa KKKT, Veraluis Mtey, alisema kabla ya utandawazi, mtoto alikuwa wa jamii lakini sasa hivi ukimwona mtoto barabarani anafanya matendo mabaya na ukamwadhibu, unafungiwa kibwebwe na mzazi wake.

“Sisi wazazi ndio wa kulaumiwa kwa hali tuliyonayo. Utandawazi umetuletea usasa tukamwondoa mtoto kutoka kuwa wa jamii akabaki wa baba au mama,” alisema.


Wazazi nao wafunguka

Baadhi ya wazazi wanathibitisha kuwapo kwa kauli zinazochangia kuwapa kiburi watoto kiasi cha kuwa wakali wanapoadhibiwa na jamii au kushitaki huku wakiongeza chumvi.

Marry Mosha, ambaye ni mwandishi wa habari na mzazi, alisema tabia ya wazazi kuwa wakali watoto wao wanapoadhibiwa wakikosea ndio kumechangia kuporomoka kwa maadili.

“Hizo kauli zipo sana kwenye jamii yetu kwa sasa, ingawa ni tatizo la baadhi ya wazazi kutojitambua. Mimi nashauri kuwe na by laws (sheria ndogo) za kumwadhibu mtoto anayekosa nidhamu sio shuleni tu hata njiani,” alisema.

Bright Ngakongwa, mkazi wa Chita mkoani Morogoro alitaka jamii ielimishwe kuwa kuna adhabu za kuvumilika na za kumuumiza mtoto, hivyo mtoa adhabu apime ili isilete madhara.

“Halafu tusiongee kutetea watoto wetu mbele ya walimu au wanaowalea, unaweza kuongelea pembeni mkaelewana na si kumkanya mlezi mbele ya mtoto unamvimbisha kichwa mtoto. Tuelimishane pasipo maneno makali,” alishauri Ngakongwa.


Walimu na wadau nao

Basil Lema, mkazi wa Shanty Town mjini Moshi ambaye ni mwalimu kitaaluma alisema wazazi wa sasa waliadhibiwa na jamii walipokosa walipokuwa watoto ndio maana ni wema na wa kutumainiwa katika jamii.

“Kumwadhibu mtoto kwa kiasi ni agizo la Mungu mwenyewe. Mtoto aadhibiwe shuleni kama namna ya kutengeneza nidhamu na kumfanya mtu wa kutumainiwa baadaye. Kwa nini wazazi wa sasa wanaleta usasa kwenye malezi?” alihoji Mwalimu Lema.

Mwalimu wa Sekondari Mawenzi ya mjini Moshi, Wilfred Mauki alisema kauli hizo ni tatizo kubwa kwa kizazi cha sasa na imesababisha mzazi kumwona mtoto wake ni wa thamani kuliko wa wengine na jamii haihusiki na malezi wala makuzi yake kwa lolote.

“Hii inatokana na wazazi kuiga malezi ya nchi za Magharibi ambayo yamechangia kuharibumaadili na mtoto kujiona ana mamlaka ya kufanya jambo lolote. Imesababisha wazazi kushindwa kukemea. Jamii irudi katika kukemea maadili mabovu kwa watoto. Tunaweza kukemea bila kuadhibu ila ikibidi kuadhibu ifanyike hivyo. Mtoto awe wa jamii kama ilivyokuwa awali na sio kuwaachia walimu tu ambao sasa ndio wamebebeshwa jukumu la malezi,” alisema.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Maadili Centre, Florentine Senya alisema matamshi hayo na mengine yanachangia watoto kuwa watukutu na wakatili, akitolea mifano msemo kama “wewe ni mjinga kama mama yako.”

“Mtoto anatoka hapo akiwa na akili iliyojengeka kuwa wanawake ni wajinga au hawana akili. Wapo wazazi wanamwambia mtoto ‘mbwa wewe au ng’ombe wewe.’ Matamshi ya aina hii yanaharibu maadili ya watoto,” alisema.

Renalda Evance alisema cha kufanya kwa sasa ni kurudisha viboko shuleni na kulea kijamii kama zamani ambapo mtoto akimkosea jirani anamwadhibu na jirani akienda kumweleza mzazi wake alichokifanya mtoto, naye anamwadhibu.