Kamati ya Sera ya Fedha yapunguza riba kuongeza pesa kwenye mzunguko

Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, Benki Kuu ya Tanzania itatekeleza sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75
Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imepunguza Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia sita iliyotumika katika robo ya mwaka iliyoishia Juni 30 2025 hadi kufikia asilimia 5.75 itakayoishia September 31 mwaka huu.
Mwenyekiti wa MPC, Emmanuel Tutuba akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 3, 2025 amesema lengo la hatua hiyo ni kuongeza fedha katika mzunguko kipindi ambacho ni cha mavuno ili kuwezesha biashara ya mazao ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi.
Katika kikao chake kilichofanyika jana, Julai 2, 2025, Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) iliamua kupunguza Riba ya Benki Kuu kutoka asilimia 6.00 hadi asilimia 5.75.
‘‘Hivyo, Benki Kuu itatekeleza sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75,” amesema Tutuba ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Tutuba amesema hatua hiyo inaashiria mahitaji makubwa ya fedha yanayotarajiwa katika msimu wa mavuno huku akisema itakuwa na athari chanya kwa sekta ya benki na wananchi kwa kuwa, fedha zinapokuwa nyingi katika benki huchechemua ukopeshaji.
‘‘Fedha zikiwa nyingi ndani ya benki maana yake taasisi hizo zinakuwa na uwezo wa kutoa mikopo kwa wale wenye vigezo jambo ambalo litatunisha mifuko ya wananchi na kuchechemua shughuli za kiuchumi,” amesema Tutuba.
Tutuba amesema uamuzi wa kupunguza CBR unaakisi imani ya kamati katika mwenendo wa mfumuko wa bei ambao umeendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3-5, na matarajio yanayoonesha kuendelea kuwa tulivu ndani ya wigo huo kwa sababu ya utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuanza kwa msimu wa mavuno na utulivu wa thamani ya shilingi.
‘‘Ingawa migogoro ya kisiasa duniani na ongezeko la ushuru wa bidhaa za forodha umeongeza sintofahamu kwenye mwenendo wa uchumi wa dunia, mazungumzo na makubaliano ya hivi karibuni yanaashiria hatari hizi zinaweza kupungua,” amesema Tutuba wakati akitoa taarifa hiyo ya MPC.
Amesema kamati hiyo ilipitia mwenendo wa uchumi wa ndani na kubaini kuwa, umeendelea kuimarika kwa kasi ya kuridhisha, ukichochewa na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu na kuongezeka kwa shughuli za sekta binafsi, kutokana na kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara.
‘‘Hatari za misukosuko ya nje kwenye matarajio ya mwenendo uchumi ni ndogo, kutokana na muundo wa uchumi wetu wenye kutegemea sekta mbalimbali za uzalishaji pamoja na utekelezaji thabiti wa sera na programu zinazochochea ukuaji wa uchumi, zinazotarajiwa kusaidia kuhimili misukosuko hiyo,” amesema Tutuba.
Kuhusu hatua hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) Theobald Sabi amesema haitakuwa na athari za mara moja katika kupunguza riba za benki kwenda kwa wateja wake lakini ni ishara nzuri kuelekea hatua hiyo tarajiwa.
Hali ya uchumi
Tathimini ya MPC katika kikao chake ilibaini kuwa, uchumi wa ndani uliendelea kuwa stahimilivu na unatarajiwa kuendelea kuimarika. Ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara unakadiriwa kufikia asilimia 5.8 katika robo ya kwanza na asilimia 5.5 katika robo ya pili ya mwaka 2025.
Ukuaji huu umechangiwa zaidi na sekta za kilimo, ujenzi na huduma za fedha na bima.
Uchumi wa ndani unatarajiwa kuendelea kuimarika kwa ukuaji kufikia asilimia 6.0 na 6.9 katika robo ya tatu na ya nne, mtawalia huku uchumi wa Zanzibar nao ukitarajiwa kufuata mwelekeo huo.
Kasi hii ya ukuaji inachochewa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya reli, barabara, viwanja vya ndege na viwanja vya michezo kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Chan na Afcon, pamoja na uwekezaji unaoendelea katika sekta za kilimo na madini.