Jafo aagiza kukamatwa kwa aliyeingiza nchini vifaa vya shisha zilizokwisha muda

Jafo aagiza kukamatwa kwa aliyeingiza nchini vifaa vya shisha zilizokwisha muda

Muktasari:

  • Mtu huyo aliyetajwa jina moja la Kaissy aliingiza kontena hizo kuanzia mwaka 2019 hadi sasa.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo ameagiza kukamatwa kwa raia mmoja wa kijeni kwa tuhuma za kuingiza nchini bidhaa za shisha zilizokwisha muda wake.

Mtu huyo aliyetambuliwa kwa jina moja la Kaissy anadaiwa kuingiza nchini takribani kontena 500 zenye urefu wa futi 40 zikiwa na bidhaa za shisha (Molasis) kuanzia mwaka 2019 hadi sasa.

Jafo ametoa agizo hilo leo Mei 3 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake kutembelea bandari na kuangalia kontena hizo ambazo zinadaiwa kuwa na shisha ambayo imeharibika na inadhaniwa kwamba iliingizwa nchini ikiwa tayari imeharibika.

Amesema ni dhahiri kwamba mzigo huo ni uchafu ambao umekuja kutupwa hapa nchini, ameliagiza Baraza la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kuhakikisha kwamba mtu huyo anakamatwa na anarudisha mzigo ulikotoka kwa gharama zake mwenyewe.

"Nina taarifa kwamba ameingiza kontena zaidi ya 500 tangu mwaka 2019, sasa anaingiza bidhaa za shisha wakati hakuna hata kiwanda, kweli huyo ni mwekezaji? Tangu mwaka 2019 anaingiza makontena tu lakini hakuna kiwanda, hilo sitakubali," amesema Jafo.

Waziri Jafo amewataka Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Nemc kujiridhisha kwanza mzigo unapoingizwa nchini ili Tanzania isiwe dampo la kutupa takataka zinazoweza kuhatarisha afya za wananchi.

Kutokana na kutoridhishwa na jambo hilo, Jafo ametoa siku tatu kwa Nemc kubaini idadi halisi ya makontena yaliyo na bidhaa ambazo zimekwisha muda wake kabla ya kwenda sokoni.

Vilevile, ametoa siku 10 kwa walioagiza mbolea na viuatilifu ambavyo vimekwisha muda wake wajisalimishe wenyewe, baada ya muda huo, ameiagiza Nemc kufanya ukaguzi kwenye bandari kavu zote ili kujiridhisha.