Jafo : Sitoruhusu ofisi yangu kuwa kikwazo cha uwekezaji

Muktasari:

  • Ili kufikia lengo la Serikali kuongeza uwekezaji nchini, Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo amesema hatoruhusu ofisi yake iwe kikwazo cha utekelezaji wa lengo hilo.

Dar es Salaam. Ili kufikia lengo la Serikali kuongeza uwekezaji Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Seleman Jafo amesema hatoruhusu ofisi yake iwe kikwazo cha utekelezaji wa lengo hilo.

 Amesema kila siku anahakikisha vyeti vinavyofika kwenye ofisi yake anavifanyia kazi ili kuruhusu shughuli kuendelea.

Akizungumza leo Ijumaa Juni 11, 2021 katika mkutano mkuu wa Chama cha Wataalam na Washauri wa Mazingira (TEEA),  Jafo amesema hataki kuwa sehemu ya kuwavuruga wawekezaji kwa kuchelewesha vyeti vya tathmini ya athari ya mazingira.

Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya watu wanaotaka kuwekeza kucheleweshewa vyeti hivyo lakini tangu ameingia wizara hiyo amelifanyia kazi suala hilo.

“Hadi leo kabla sijafika hapa nimehakikisha mezani kwangu hakuna cheti kinachosubiri kupitishwa na waziri. Niwaombe washauri na baraza la usimamizi mazingira kwenda na kasi hii ili kupunguza kelele za madai ya kukwama kwa kusubiri vyeti,” amesema Jafo.

Amesema kupitia mfumo wa kidigitali ambao unatumika sasa ni rahisi kufuatilia maendeleo ya maombi ya vyeti na hatua zilipofikia hivyo wawekezaji wasisite kuwasilisha malalamiko ofisi yake wakiona mambo yamesimama.

Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc),  Dk Samwel Gwamaka amesema mfumo wa usajili kwa njia ya digitali umezidi kuimarika na hadi Juni 10, 2021  imesajiliwa miradi 956.

Amesema matumizi ya mfumo huo yanasaidia kuwaondoa washauri elekezi wa mazingira vishoka ambao wamekuwa wakifanya kazi chini ya viwango.