Jaji Feleshi ahamasisha matumizi ya Tehama kuharakisha kesi

Jaji Feleshi ahamasisha matumizi ya Tehama kuharakisha kesi

Muktasari:

  • Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Eliezer Feleshi amewaagiza mahakimu wafawidhi wa mahakama hapa nchini kuhakikisha wanaendesha mashauri kwa mfumo wa Tehama ili mashauri yawafikie wananchi kwa haraka.

Njombe. Mahakimu wafawidhi wa mahakama hapa nchini wameagizwa kuhakikisha wanatumia mfumo wa Tehama katika kuendesha mashauri ili yawafikie wananchi kwa haraka zaidi.


Hayo yamesemwa  leo 27 Aprili 2021  na Jaji kiongozi wa mahakama kuu ya Tanzania Eliezer Feleshi wakati wa uzinduzi wa majengo ya mahakama ya hakimu mkazi na mahakama ya wilaya ya Njombe uliyofanyika mkoani Njombe.


Amesema Waraka Na.3 wa mwaka 2018 unawalazimu mahakimu wafawidhi na watumiaji wote wa mahakama kuhakikisha mashauri yao yanaingizwa kwenye mfumo wa uendeshaji wa mahakama.

Amesema katika kutimiza hilo usajili wa mashauri ya madai na jinai kwa sasa ni haki iliyopo kwa saa 24 kwa sababu kuna usajili wa kidijitali ambao unamuwezesha mtumiaji wa mahakama kufungua shauri lake mahali popote alipo kwa kuingia na kupata haki za kufunguliwa na kusajili shauri hilo.


"Lakini kwa wale wasio na uwezo au uelewa vipo vioski maalum ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya usaidizi," amesema  Feleshi.
Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ya intaneti lakini mahakama ina wajibu wa kukabiliana na tatizo hilo ili waendelee kuwahudumia wananchi kwa kutoa haki ambayo wanastahili kuipata.


Amewataka  watendaji wa mahakama kubaini maeneo ya kipekee ambayo mkongo wa taifa haujafika ili wahusika wa mahakama kuangalia kwa upande wa bajeti ili maafisa Tehama na wataalam wawezeshwe kwa njia mbadala  ili wananchi wasishindwe kuifikia mahakama kwa njia ya mtandao.

Amewataka pia watumishi wengine wa idara za serikali kuendelea kuifunza na kufuatilia utendaji kazi wa mahakama ili kuepuka dhana iliyojengeka kuwa mahakama inawaburuza.


Msajili mkuu wa mahakama ya Tanzania, Wilbert Chuma amewataka watumishi wa mahakama na wadau wengine kuwajibika kwa kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia maadili ya kazi na viapo ili huduma watakazozitoa ziendane na uzuri wa jengo hilo.


Amewataka mawakili kufungua mashauri yao kwa njia ya mtandao kama ilivyoelekezwa ili kuweza kuokoa muda na gharama kwa wananchi wanaotaka huduma za mahakama.


"Naomba tuyaishi maboresho kwasababu hakuna pakukwepa na niwaombe wananchi mahakama hii ni yenu muitumie katika kutatua changamoto zenu mbalimbali na tusaidiane katika kuilinda ili iendelee kudumu na kutoa huduma," amesema  Chuma.


Jaji mfawidhi kanda ya Iringa, Pentelni Kente amesema  kwa upande wa mahakama wamepita katika hishoria ndefu kuhusiana na majengo kwani zamani waliweza kufanya kazi katika majengo ya vyama na wakati mwingine kwenye nyumba za watu binafsi.


"Kuna wakati tulikuwa tunapanga jengo la mwananchi wa kawaida mahakama ya mwanzo ipo pale upande wa pili kuna cherehani na nyumba haina dari halafu unasikiliza kesi maeneo hayo" amesema Kente.


Mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya amesema kukamilika kwa jengo hilo sambamba na majengo ya Makete na Wanging'ombe ni ukombozi kwa mkoa wa Njombe kwasababu mhimili wa mahakama utaendesha shughuli zake katika mazingira bora.


"Nimeelezwa kuwa kwa mikoa ya nyanda za juu kusini mkoa wetu wa Njombe una idadi kubwa ya kesi za mauaji," amesema  Rubirya.