Jaji Feleshi ashtuka utitiri wa malalamiko ziara za Makonda

Muktasari:

  • Ashangaa mambo aliyoyasikia miaka 15 iliyopita bado yanalalamikiwa na wananchi, aona umuhimu wa kuanzisha vituo jumuishi kila mkoa, kusikilliza malalamiko ya wananchi kwa saa 24

Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dk Eliezer Feleshi ameeleza kushtushwa na utitiri wa watu kwenye ziara za Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda wakilalamika kudhulumiwa haki na utekaji wa ndugu zao.

 Jaji Feleshi amesema hayo leo Alhamisi, Februari mosi 2024 alipokuwa akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yanayofanyika jijini Dodoma na mgeni akiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mimi napenda utafiti, kati ya vitu nilivyoshangaa mambo niliyoyasikia labda miaka 15 nyuma bado hayo hayo wananchi wanayalalamikia, nikifuatilia ziara ya yule katibu wa itikadi wa Chama cha Mapinduzi (Paul Makonda) naona wananchi bado wanajisomba kwake kama mafuriko.

“Hivyo hivyo ukifuatilia nyumba za ibada wananchi wanajisomba huko, kwa hiyo hii sasa mheshimiwa Rais tunaichukulia kama changamoto, pamoja na kusoma kwetu, pamoja na kupata nyenzo na maboresho tunayoendelea nayo, tujue wananchi wanahitaji kupata kile wanachokusudia kukipata.

“Kwa minajili hii mheshimiwa Rais wewe ndiye mlezi wa ofisi yetu na taasisi za kiserikali, tumekusudia vile vile tuwe na vituo vya huduma wezeshi saa 24. Yeyote aliyekosa huduma mahala afike kwenye hicho kituo na kuelekezwa taratibu za kuchukua,” amesema na kuongeza;

“Na sisi tutanzia hapa Dodoma nafikiri tutaomba usaidizi wa kibajeti, ikiwezekana mwaka huu unaokuja wa fedha, kituo hicho cha kwanza jumuishi kianze, mtu ambaye kafungiwa mlango sehemu fulani, basi apewe yale maelezo yote ya msingi, ilimradi tupunguze huu utitiri wa watu kwenda mahala pasipostahili,” amesema Feleshi.

Ziara ya Makonda mikoani zimeibua malalamiko mengi ya watu kutekwa na wengine kudhulumiwa haki zao, huku wakikosa usaidizi wa kisheria na wengine walialamikia askari polisi kushindwa kuwasaidia au kushiriki uhalifu huo.

Kwenye mikoa ya Singida, Shinyanga na Simiyu alikutana na malalamiko ya watu kupotea tangu mwaka 2021 na wengine walitoweka kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana tangu mwaka 2022 na mwaka jana.

Wananchi hao wamedai malalamiko yao yanafahamika kwenye vituo vya polisi na hata serikalini, lakini hakuna msaada waliopata.

Hata makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya na viongozi wa Serikali wakiwamo wakuu wa mikoa wamekiri kufahamu malalamiko hayo.