Jaji Mutungi: Kumbe wakati mwingine Polisi wana nia njema

Jaji Mutungi: Kumbe wakati mwingine Polisi wana nia njema

Muktasari:

  • Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi amesema kuna baadhi ya mambo ambayo laiti watu wangeelezwa na Jeshi la Polisi wangeanza kushuku kama wanafanya siasa ama wanaleta fujo.

Dodoma. Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi amesema kuna baadhi ya mambo ambayo laiti watu wangeelezwa na Jeshi la Polisi wangeanza kushuku kama wanafanya siasa ama wanaleta fujo.

Mutungi amesema hayo leo Alhamis Septemba 23, 2021 baada ya mkutano wake na Jeshi la Polisi uliomshikirisha pia Mkuu wa Jeshi hilo, Simon Siro.

“Na leo kwa mara ya kwanza nimegundua kuwa kumbe wakati mwingine polisi wanakuwa na nia njema, kuna mambo ambayo tunakuwa hatuyajui sisi raia lakini laiti wangekuwa kila kitu wanakieleza tungeanza kushuku kama tunafanya siasa ama tunaleta fujo,”amesema.

Amesema katika kikao hicho wamezungumza mambo mengi ambayo yamemfungua macho na kwamba alichojifunza mawasiliano ya mara kwa mara ni muhimu.

Jaji Mutungi amesema baadhi ya mambo watayafikisha kwa wanasiasa na hivyo watakapokuja kukaa kikao cha pamoja watakuwa na mwelekeo mzuri wa huko wanaokokwenda kisiasa.

Amesema kikao hicho ni miongoni ya mchakato wa kujenga (reconciliation) kabla ya kikao cha pamoja cha wadau kitakachofanyika Oktoba 21 mwaka huu.

Amesema wanajaribu kupunguza misuguano ambayo haina ulazima.

Kwa upande wake, IGP Sirro amesema jambo la kwanza walilokuwa wanaangalia ni changamoto ambazo zinajitokeza kati ya vyama vya siasa vinavyolalamika kuzuiwa kufanya mikutano ya ndani.

“Kimasingi tumezungumza na kuona kwenye suala zima la mikutano ya nje kwa kweli hakuna shida na si vyama vingi vinavyolalamika tumekuwa tunaingilia lakini shida kubwa iko katika mikutano ya ndani,”amesema.

Amesema wameona kuwa sheria haijatamka bayana kuhusu sheria inayotawala vikao vya ndani vya vyama.

Amesema hilo wameliona kuwa kumekuwa na mwingiliano au sintofahamu baadhi ya vyama vya siasa kwa mkutano badala ya kuufanyia nje wanaufanyia ndani.

“Sisi jeshi la polisi tunaangalia usalama kwanza, tunaangalia suala la amani na utulivu katika hiyo mikutano. Tukishabaini amani na utulivu ni changamoto au kuna tishio lolote la amani na utulivu basi ni lazima tuchukue hatua,”amesema.