Jaji Warioba alia na nyufa alizozisema Nyerere

Waziri Mkuu, mstaafu Jaji Joseph Warioba akizungumza katika mdahalo wa wanasiasa na wadau wa siasa ulioandaliwa na taasisi ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwenyekiti wa taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema nyufa alizokuwa anazizungumzia Mwalimu Julius Nyerere ambazo ni ukabila, udini na ukanda, bado zipo nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema nyufa alizokuwa anazizungumzia Mwalimu Julius Nyerere ambazo ni ukabila, udini na ukanda, bado zipo nchini Tanzania.

Jaji Warioba ameyasema hayo leo Jumanne Sepetmba 20, 2022 wakati wa kongamano la kufanya tathmini ya kazi ambayo Taasisi ya Mwalimu Nyerere imefanya katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.

Amesema mwaka 1995, Mwalimu Nyerere alizungumzia nyufa zilizokuwepo, hata hivyo amesema nyufa hizo bado hazijazibwa kwa sababu mambo ya ukabila, udini na ukanda bado vipo kwenye jamii ya Watanzania.

"Sasa ukabila unaanza kuzungumzwa na hasa katika siasa. Hakuna kiongozi siku hizi ambaye atagombea asijihusishe na ukabila, mara nyingi wanakimbilia ukabila, ndiyo msingi hasa wa kuchaguliwa," amesema Warioba.

Amesema ufa huo umezidi kupanuka, jambo ambalo ni hatari kwa umoja wa kitaifa, hivyo amewataka Watanzania kutafakari jambo hilo na kuona namna ya kuziba ufa huo.

"Sasa tunataka uchifu urudi, sasa kila chifu akianza kuleta maadili ya kabila lake, hali itakuwaje. Lazima tutafakari hili na kuona namna ya kuziba nyufa hizo," amesema Warioba.

Kuhusu suala la udini, Warioba amesema nao upo hasa kwa viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakitumia nyumba za ibada kama majukwaa ya kisiasa, jambo ambalo sio zuri kama alivyoonya Mwalimu Nyerere.

"Siku hizi viongozi wanakwenda kwenye ibada kama viongozi, sio kama waumini na mara nyingi wanataka wapewe nafasi ya kuzungumza na mambo yanayozungumzwa hayaendani na somo la siku hiyo," amesema mstaafu huyo.

Warioba ambaye aliwahi pia kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema ukanda nao unazungumzwa hasa kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linapanua ufa huo na kuhatarisha umoja wa kitaifa.

"Mambo ya ukanda yanazungumzwa sana kwenye mitandao, ukizungumzia Muungano yanajitokeza mambo ya ukanda; kwamba Wazanzibari ni bora kuliko wa Bara au wa Bara ni bora sana kuliko Wazanzibari," amesema Warioba.

Hata hivyo, Warioba amebainisha kwamba nyufa hizo zinajitokeza zaidi kwa wanasiasa, wananchi wenyewe wana woga wa mambo hayo, ndiyo maana wanafanya shughuli zao bila woga wowote.