Jaji Warioba: Viongozi wasipende kusifiwasifiwa

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akijibu maswali ya waandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wakati wa mahojiano yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Jaji Joseph Sinde Warioba ni miongoni mwa viongozi walioitumikia nchi kwa muda mrefu kwa nyadhifa tofauti na kujijengea umaarufu kutokana na misimamo yao isiyoyumba.

Jaji Joseph Sinde Warioba ni miongoni mwa viongozi walioitumikia nchi kwa muda mrefu kwa nyadhifa tofauti na kujijengea umaarufu kutokana na misimamo yao isiyoyumba.

Juzi Mwananchi lilifanya mahojiano na Jaji Warioba ofisini kwake jijini Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali ya taifa. Endelea

Mwandishi: Mambo gani yanayokukera zaidi?

Jaji Warioba: Tabia ya viongozi kupendakusifiwa, woga wa watu kutoa maoni, kujipendekeza na kutoambiana ukweli.

Mimi nimekulia kwenye misingi ya kuambiana ukweli…hatukuwa na unafiki. Sasa hivi naona unafiki mwingi. Mimi nilikuwa msaidizi wa Mwalimu (Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere) kwa miaka kumi kwa wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nilikuwa miongoni mwa wasaidizi waliokutana na Rais mara nyingi.

Nilikuwa simuogopi Rais, nilikuwa namheshimu. Tulikuwa tunaweza kuwa na mjadala na tukatofautiana. Akawa na mawazo tofauti na tukaendelea, lakini mwisho wa siku akitaka atafanya uamuzi na mimi nitakwenda kutekeleza. Nitaondoka pale sina wasiwasi.

Sasa hivi naona kama watu wanapenda sana kujipendekeza. Kusifu, kufanya hivi. Mie nadhani uongozi ni kuonyesha njia. Wananchi wanataka waone kiongozi amenyooka, lakini leo uko hivi, kesho uko vile hutaaminika.

Hili la kusifu viongozi kila wakati linaua fikra zao, hawaumizi vichwa dhidi ya mambo wanayoletewa kwa kuwa mengi yanaonekana ni mazuri, wakati ule tukiwa madarakani ulikuwa ukisoma magazeti unapata makala, barua za wasomaji na tahariri zenye kukosoa na kujenga, hivyo unazifanyia kazi kwa faida ya wananchi.

La pili, kuna woga wa kutoa mawazo.Sijui kwa nini watu wanaogopa kutoa mawazo na hata wakitoa wanashambuliwa binafsi na si hoja waliyoitoa.

Mwandishi: Labda ni kwa sababu ya kuanzishwa kwa sheria zinazolalamikiwa, ikiwemo ile ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 na sheria ya takwimu ya 2015?

Jaji Warioba: Lakini kuna sheria nyingine sizielewi zilipitishwaje (akionyesha hali ya kushangaa). Sasa takwimu, unasema mtu akifanya utafiti ili azitoe au kuzitumia takwimu mpaka ziende zipitishwe mahali, mimi hilo naliona kama halijakawa sawa…maana hapa ni kama unazuia watu wasifanye utafiti, sasa sijui kwa nini watu hawakusema juu ya hizi sheria.

Hivi kweli bado mtu akifanya utafiti apeleke takwimu kwenda kuthibitishwa. Unajua centralization inaleta inefficiency. Na siye tumepitia huko, mie nilikuwa msaidizi wa mzee Mwinyi (Rais wa awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi). Lakini siku moja Mzee Mwinyi alinipa uhuru kabisa akasema wewe (Jaji Warioba) utawasimamia wenzako na tukaelewana na wenzangu.

Kama isingekuwa kuelewana hivyo, kipindi kile kilikuwa kigumu sana. Tulifanya kazi kwa timu, tukasema hapa sio urafiki ni uwajibikaji wa pamoja hivyo wote tufanye kazi. Mkiwa na kitu msikifiche, mnakisema wote tunakaa pamoja tunakizungumza. Tulikuwa wawazi.

Lakini siku hizi mtu kabla ya kusema au kutenda jambo kwanza anatazama kulia na kushoto ili kuangalia nani yuko karibu naye, hili si sahihi hata kidogo, kwa kuwa ni lazima watu wawe na uhuru kamili.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya watu waliamua kukaa kimya ilhali mambo yalikuwa yakienda sivyo ndivyo.

Ni lazima tujenge taifa ambalo kila mmoja atakuwa huru kutoa maoni yake bila kuvunja Katiba na sheria za nchi, kutofautiana kwa mawazo ndiko kunajenga kitu bora zaidi.

Sijui kitu gani kilipita katika miaka michache iliyopita ambapo watu walikuwa waoga mno na hata vyombo vya habari vikawa na taarifa za kusifu viongozi, hali iliyonifanya nisisome vyombo vya habari kwa kuwa nilikosa makala na uchambuzi makini.

VIDEO: Jaji Warioba-Viongozi wasipende kusifiwasifiwa


Mmomonyoko wa maadili


Mwandishi: Hivi sasa kuna mnyukano wa maneno na vijembe baina ya makada wa CCM kwa kuitana majina ya kudhalilishana, wakati wenu mliwezaje kudhibiti hali hii?

Jaji Warioba: Vijana tulikuzwa katika maadili na tuliyafuata, lakini hivi sasa maadili yameporomoka, ndiyo maana unasikia wanaitana chawa mara kiroboroto na majina mengine mengi yasiyofaa.

Hili suala la maadili, wananchi walizungumzia sana wakati wa kutoa maoni kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na likawekwa kwenye rasimu ya mabadiliko ya Katiba kama mojawapo ya tunu za taifa, lakini likaondolewa kwenye Bunge Maalumu la Katiba.

Kuondolewa kwa kipengele hicho pia kulinipa wasiwasi na kushindwa kuelewa kwa nini wajumbe wa Bunge lile walifanya vile wakati wakijua fika Katiba Inayopendekezwa itakwenda kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Sasa kama wananchi walitaka jambo fulani liwemo ndani ya Katiba halafu jambo hilo halimo kwenye Katiba Inayopendekezwa unadhani watapiga kura ya aina gani?

Hata hao vijana na makada wanaorushiana vijembe wanatoka ndani ya jamii ambayo maadili yake yameporomoka. Bado misingi ya chama kile (CCM) ni ileile. Ukienda usome zile ahadi za mwanachama wa CCM ambazo zilikuwa msingi, unazifuata zile.


Awamu ya tano

Mwandishi: Rais wa tano, John Magufuli alipambana sana na rushwa lakini bado inazidi, tatizo ni nini?

Jaji Warioba: Mimi nilikuwa na matumaini sana na awamu ya tano ilipoingia madarakani ilikuwa na msimamo mzuri sana wa kupambana na mambo haya ya rushwa, ufisadi, dawa za kulevya. Ikaanzishwa hata mahakama ya mafisadi lakini matokeo yake bado hayaridhishi, kwa sababu kwa miaka mitano hiyo hatukushughulikia suala la maadili ndani ya jamii na ndani ya vyama vyetu.

Sasa ukiona ni kama tulishughulika na rushwa lakini sidhani kama kweli tunashughulika na rushwa, nadhani tulishughulika na ubadhirifu zaidi badala ya rushwa.

Tumefuata watu kwa mambo ya fedha zaidi. Mie naogopa sana rushwa, hususan ndani ya uongozi na hiyo bado hatujaifanyia kazi sana.

Ukiuangalia uchaguzi wa mwaka juzi, hususan hatua ya uteuzi wa wagombea ndani ya vyama, kulikuwa na rushwa nyingi sana, lakini sikusikia kesi hata moja. Sasa ukiona tunapata uongozi kwa msingi wa rushwa, hata kiongozi akiwa na nia nzuri namna gani akishazoea rushwa basi inakuwa ni wote pia wanaofuata (vijana).

Kwa hiyo haya mnayosema wanaitana wahuni, wahuni mitandaoni actually sio vijana wa CCM tu, nadhani ni jamii nzima hata wasomi. Kwa machache niliyoletewa nikaona kutoka mitandaoni na wakati mwingine kwenye WhatsApp, sijiungi na kundi lolote ila napata clips nyingi tu. Wakati mwingine nashangaa hatuzungumzi hoja ila tunajadili watu, mtu analeta hoja mara anaambiwa sijui Lumumba, Ufipa badala ya kuzungumzia hoja.

Na hili la matusi (wahuni na viroboto) wanaona ni kitu cha kawaida tu. Labda tuseme ni kufuata matendo ya viongozi. Kwa wakati ule nadhani tulikuwa na bahati nzuri, chochote utakamchosema Mwalimu Nyerere kwa mambo yake, mkosoe mahali popote lakini suala la maadili ilikuwa hata usipofuata anachosema, wewe fuata anachotenda.

Mwandishi: Tumeanza kuhesabu kalenda ya mwaka 2022, Watanzania wafanye nini?

Jaji Warioba: Mwaka 2021 haukuwa mwaka rahisi. Tulikuwa na matatizo makubwa, ugonjwa wa Uviko-19 ulitusumbua na uchumi wetu ukaingia kwenye matatizo, pamoja na hiyo Taifa likapata pigo kubwa sana la kumpoteza Rais John Magufuli. Sio jambo dogo, lakini kwa bahati njema tulipita salama baada ya msiba ule tukajipanga, tukaenda vizuri na kwa kiwango kikubwa bado Watanzania tuko na umoja wetu, mshikamano wetu.

Nadhani tuwe na matumaini, ningependa kuona mwaka 2022 uwe mwaka wa maridhiano kisha wote kwa pamoja tupambane na matatizo tuliyonayo. Kwa kweli tujitahidi kwa sababu nchi yetu bado ni nchi ya amani, tusiruhusu tofauti zozote zile zikaingilia umoja wetu, tuendelee kuwa na umoja, mshikamano, utulivu na tudumishe amani yetu. Hayo ndio msingi wa amani yetu. Tuyatazame matatizo yetu ya Kitanzania. Kwa hiyo natumaini mwaka huu tutapata mafanikio zaidi.


Hali ya kisiasa

Mwandishi: Mwishoni mwa mwaka jana ulifanyika mkutano wa wadau wa vyama vya siasa, unadhani utasaidia kutatua mikwaruzano ya kisiasa inayojitokeza mara kwa mara?

Warioba: Ni hatua nzuri kwa viongozi na wadau kukutana kwa kuwa wanapata nafasi ya kuzungumza yanayowakwaza na kuyatafutia ufumbuzi.

Baada ya kikao kile tuliyatoa mambo zaidi ya 80 ambayo ninaamini kikosi kazi kilichoundwa na ofisi ya msajili kitafanya kazi vizuri na iwasikilize hata wale ambao hawakuhudhuria ule mkutano

Mimi ni muumini wa maridhiano na viongozi kukutana, jambo ambalo ninaliona kwa muda mrefu watu walikuwa hawakutani lakini Rais Samia Suluhu Hassan alipokutana nasi pale Dodoma aliweka wazi utayari wake wa kuzungumza, kusamehe na utaratibu wa kufanya siasa hapa nchini.

Kule Zanzibar kwa muda mrefu kulikuwa na mgogoro wa kisiasa ambao baada ya Rais mstaafu Amani Abeid Karume kukutana na Maalim Seif Sharrif Hamad na kuzungumza walikubaliana kuzika tofauti zao na kuweka mipango madhubuti ya kuendeleza nchi yao na hivi sasa Zanzibar imetulia.