Jalada kesi mkurugenzi wa Jatu latua polisi

 Mkurugenzi JATU PLC, Peter Gasaya, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa masharti ya dhamana. Hata hivyo mshtakiwa huyo ameshindwa kutimiza masharti hayo na hivyo kurudishwa rumande. Picha  na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Gasaya anadaiwa kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, kwa udanganyifu alijipatia Sh5.1 bilioni kutoka Saccos ya Jatu.

Dar es Salaam. Jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33) lipo polisi kwa ajili ya upelelezi zaidi.

 Wakili wa Serikali Eva Kasa, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Novemba 20, 2023 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Gasaya anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh 5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao, ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, wakili Kasa, amedai kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea.

“Mheshimiwa hakimu, kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea, jalada halisi la shauri hilo lipo polisi kwa upelelezi zaidi, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili kutajwa" amedai Kasa.

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi, Nafikile Mwamboma alipinga maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka kuhusiana na upelelezi kutokamilika.

Mwamboma amedai wameandika barua ya kuomba mwenendo wa kesi hiyo tangu ilipofunguliwa mpaka sasa.

“Mheshimiwa hakimu tukipata mwenendo wa kesi hii tangu ilipofunguliwa hadi ilipofikia sasa, tutachukua hatua zaidi za kisheria," amedai wakili Mwamboma.

Hakimu Kabate baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, ameahirisha kesi hadi Desemba 4, 2023 itakapotajwa.

Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video conference huku mshtakiwa akiwa rumande.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 jijini Dar es Salaam, akiwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, kwa udanganyifu alijipatia Sh 5,139,865,733 kutoka Saccos ya JATU.

Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa si kweli.

Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.

Siku hiyo, mshtakiwa akiwa mtendaji mkuu na mwanzilishi wa Jatu SACCOS, alijihusisha na muamala wa Sh 5,139,865,733 kutoka akaunti ya Jatu SACCOS iliyopo Benki ya MNB, tawi la Temeke kwenda akaunti ya Jatu PLC liyopo Benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa udanganyifu.