Bosi Jatu asota rumande siku 311 akisubiri kesi
Muktasari:
- Gasaya anadaiwa kutenda makosa yake, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, ambapo akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia zaidi ya Sh5.13 bilionikutoka JATU Saccos.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33) anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, anaendelea kusota rumande, kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokukamilika.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Kwa mara ya kwanza, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Desemba 29, 2023 akikabiliwa na mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Hata hivyo, tangu afikishwe mahakamani hapo hadi leo, Novemba 6, 2023, upelelezi wa shauri bado haujakamilika, amefikishwa miezi 10 na siku nane ambazo ni sawa na siku 311 bila upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Leo Wakili wa Serikali, Frank Michael ameieleza Mahakama hiyo kuwa upekekezi wa shauri hilo bado haujakamilika, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Michael amedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 20, 2023 itakapotajwa.
Gasaya yupo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili, halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Aprili 23, 2023, Gasaya alimwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) akiomba kukiri mashtaka yake na kuomba apunguziwe adhabu.
Lakini, Julai 31, 2023 mshtakiwa huyo aliondoa nia yake ya kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi yake kwa madai kuwa barua aliyokuwa ameandika ya kuomba kukiri mashtaka na kuiwasilisha upande wa mashtaka, haionekani.
Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa, katika ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia zaidi ya Sh5.13 bilioni kutoka Saccos ya Jatu.
Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu SACCOS, alijihusisha na muamala wa zaidi ya Sh5.13 bilioni kutoka katika akaunti ya Jatu SACCOS iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC liyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke.