Jamii yatakiwa kujikinga homa ya ini

Muktasari:
- Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel amewataka Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini.
Dk Mollel alitoa kauli hiyo kupitia taarifa iliyotolewa na wizara yake leo Julai 28, 2023 ikiwa ni maadhimisho ya siku ya homa ya ini duniani iliyobebwa na kaulimbiu ‘Tunaishi mara moja, ini moja.
Katika taarifa yake hiyo, Dk Mollel ameeleza kwamba homa ya ini husababishwa na virusi waliogawanywa katika makundi matano yaani A, B, C, D na E.
“Aina ya virusi vya A na E huambukizwa kwa njia ya kunywa maji na chakula kisichokuwa salama kwa kuchafuliwa na kinyesi chenye maambukizi ya virusi hivyo,” amesema.
Ametaja njia za maambukizi ya homa ya ini kundi B, C na D kuwa, ni kuongezewa damu zenye virusi vya ugonjwa huo, kujamiiana, utumiaji usio salama wa sindano na kujichoma na vitu vyenye ncha kali,
Amesema homa ya ini inayosababishwa na virusi vya kundi B yaani Hepatitis B (HBV) ndiyo inayoongoza kwa maambukizi nchini kwa mujibu wa takwimu.
“Hepatitis B inaweza kuzuiliwa …kwa kupunguza idadi ya wapenzi wengi, kuacha kujidunga madawa ya kulevya, kuepuka ngono zembe na kuepuka matumizi ya vilevi kupita kiasi,” ameongeza.
Kuhusu utoaji wa chanjo ya homa ya ini aina B, Dk Mollel amesema huduma hiyo inatolewa kwa watoto wachanga na kwa watu wazima hasa wale walio kwenye makundi hatarishi.
“Kwa watu wazima hutolewa kwa watu walio kwenye makundi hatarishi kama watumishi wa afya, watu wanaojidunga madawa ya kulevya, watu wenye wapenzi wengi, watu wenye magonjwa sugu ya ini, figo, kisukari na wenye upungufu wa kinga mwilini.”
Akizungumzia upatikanaji wa chanjo amesema zinatolewa katika Hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za rufaa za kanda na pia katika Taasisi ya Saratani Ocean Road na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Naye Mtaalamu wa maabara Tumaini Warioba ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi isiyo ya kiserikali Organization for Medical Outreach to Communities amesema changamoto kubwa iliyopo kwenye jamii ni wananchi kutokuwa na uelewa juu ya homa ya ini.
“Homa ya ini ipo nchini lakini utamaduni wa watu kupima na kuchanja bado uelewa upo chini, hivyo jamii ni muhimu ichukue tahathari ya ugonjwa huu kw akupima na wale ambao hawajagundulika wachanje,
Wengi wanaofika hospitali wanakuja ugonjwa ukiwa katika hatua za mwisho zaidi hatua ambayo huibua ugumu wa watu kumsaidia mgonjwa kutokana na kwanza yeye mwenyewe kukata tamaa,”amesema.
Amesema mjamzito anapofika kliniki apime homa ya ini ili kuugudua ugonjwa huo mapema ili kumlinda mtoto aliyetumboni.
“Pia hatuna miongozo ya matibabu ya ugonjwa wa homa ya ini ambayo utamuelekeza mtaalamu namna ya kutoa tiba ya ugonjwa huo,
Kutengenezwe mfumo wa rufaa kwa wagonjwa wa homa ya ini na hospitali zinazopima kama mtu ana maambukizi ya homa ya ini wawezeshwe kupata vitendanishi kutumia kwasababu zimetolewa mashine lakini hakuna vifaa,” ameeleza.