Jela miezi 10 kwa kuvunja, kuiba vitu vya ndani
Muktasari:
- Mshitakiwa Pastory Meza amehukumiwa kwenda jela miezi 10 na Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo baada kuiba vitu mbalimbali ikiwemo sufuria nne pamoja na gunia la mkaa.
Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Kariakoo imemuhukumu, Pastory Meza (25) kifungo cha miezi 10 jela baada ya kukiri kutenda makosa ya kuvunja nyumba na kuiba vitu vyenye thamani ya Sh790, 000 mali ya Rukia Magere.
Hukumu hiyo imesomwa leo Aprili 18, 2023 na Hakimu, Gladness Njau, akisema pia mshitakiwa alikutwa na baadhi ya vitu alivyoiba ikiwemo televisheni, redio pamoja na pasi.
Njau amesema kwa kuwa mahakama hiyo imemtia hatiani hivyo inamuhukumu kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kuvunja na miezi minne kwa kosa la wizi.
"Adhabu hizo zitakwenda tofauti na mshtakiwa anaweza kukata rufaa kama hajaridhika na hukumu," amesema Njau.
Awali akisoma mashitaka mahakamani hapo Karani, Linda Kivaju alidai mahakamani hapo kuwa April 5, 2023 nyuma ya ukuta wa shule ya sekondari ya Azania iliyopo Upanga mshtakiwa huyo alivunja mlango wa nyumba ya, Rukia Magere na kuingia ndani.
Katika shtaka la pili alidai kuwa baada ya kuvunja mshitakiwa huyo aliiba Televisheni aina ya Samsung, redio, baiskeli, sufuria nne, jiko la gesi, pasi ya umeme pamoja na gunia la mkaa huku vitu vyote vikiwa na thamani ya Sh790, 000.
Kwa upande wake Rukia aliyedai kuwa siku ya tukio alikuwa shamba Mkuranga na mtoto wake aliyemuacha nyumabani alikwenda shule ndipo mshitakiwa alitumia nafasi hiyo kuvunja na kuiba.
Amedai kuwa alipigiwa simu na kutaarifiwa juu ya wizi huo na baada ya kurudi alikwenda kutoa taarifa polisi ambako walimuambia asubiri upelelezi.
Amedai kabla ya upelelezi haujakailika alipigiwa simu na mdogo wake ambaye ni miongoni mwa walinzi shirikishi na kumtaarifu kuwa mwizi aliyeiba vitu vyake tayari amekamtwa.