Jenista, Simbachawene waapishwa

Muktasari:

  • Mawaziri waliobadilishana wizara wameapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, tayari kuanza majukumu yao.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaapisha George Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Jenista Mhagama kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.

Wawili hao waliteuliwa kushika nyadhifa hizo jana, katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanya na Rais Samia.

Mabadiliko hayo ni kama wamebadilishana wizara, kwani kabla Simbachawene alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu na Jenista alikuwa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.

Uapisho wa mawaziri hao umefanyika leo, Aprili 2, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam bila kurushwa mubashara katika vyombo vya habari.

Kwa upande wa Jenista hii ni mara ya nne anateuliwa kuiongoza wizara hiyo, kwani aliwahi kuhudumu miaka ya 2014, 2015, 2020 wakati huo ikiitwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge, Uratibu, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu.

Baadaye iligawanywa na kupatikana wizara mbili ambazo ni ile inayoshughulikia sera, bunge na uratibu na nyingine kwa ajili ya ajira, kazi, vijana na wenye ulemavu.

Wakati Simbachawene anaukwaa wadhifa huo katika wizara hiyo kwa mara ya kwanza, lakini akiwa na rekodi ya mwanasiasa aliyedumu katika wizara mbalimbali bila kuwekwa benki.

Tangu mwaka 2012, Simbachawene amekuwa akitumia wizara mbalimbali hadi mwaka 2017 alipowekwa benchi na utawala wa Hayati John Magufuli, lakini baadaye 2019 alirudishwa na anaendelea hadi sasa.