Jeshi la China, JWTZ wanavyoshirikiana kiulinzi
Viongozi wa Ulinzi wa Tanzania na China wakishiriki maadhimisho ya miaka 99 ya Jeshi la Jamhuri ya Watu wa China jinini Dar es Salaam, Julai 2026.
Muktasari:
- Tanzania imesema ushirikiano wa kijeshi na China umeimarisha ulinzi, usalama na amani kupitia mafunzo, uzoefu wa pamoja, teknolojia na mahusiano ya muda mrefu.
Dar es Salaam. Tanzania imeeleza umuhimu wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ikisema umeendelea kuwa msingi wa kuimarisha uwezo wa ulinzi na usalama wa mataifa hayo mawili.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho, katika warsha ya kuadhimisha miaka 99 ya kuanzishwa kwa PLA, iliyojadili historia ya jeshi hilo na mchango wake katika kulinda amani duniani.
Katika maadhimisho hayo kwenye Ubalozi wa China jinini Dar es Salaam, usiku wa Julai 21, 2026, Dk Nyansaho alisema ushirikiano kati ya Tanzania na China ulianza kujengwa na waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong, na umeendelea kuimarishwa na viongozi wa sasa akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Xi Jinping.
Alisema mahusiano hayo yamepanuka kutoka eneo la ulinzi na usalama hadi sekta nyingine za maendeleo, ikiwemo elimu, afya na miundombinu.
“Tunathamini ushirikiano huu kwa sababu unaimarisha ulinzi na usalama wetu na kuongeza mshikamano kati ya mataifa yetu,” alisema.
Alisema dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama ikiwemo migogoro ya kimataifa, magonjwa ya mlipuko na vitisho vingine vinavyohitaji ushirikiano wa nchi mbalimbali katika kulinda amani na maendeleo.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema PLA ilianzishwa mwaka 1927 na imeendelea kuwa chombo muhimu katika kulinda uhuru, maisha ya wananchi na kushiriki katika shughuli za kimataifa za kulinda amani.
Alisema chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping, PLA imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za usalama na kusaidia juhudi za kulinda amani duniani.
“Urafiki wa China na Tanzania ulijengwa na waasisi wa mataifa yetu na umeendelea kuwa msingi wa kusaidiana katika nyakati mbalimbali,” alisema Chen.
Askari wa Jeshi la China (PLA) wakionesha Stadi za Kijeshi Katika maadhimisho ya miaka 99 ya Jeshi hilo jinini Dar es Salaam, Julai 21, 2026.
Alisema China na Tanzania zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali, akitaja reli ya Tazara kama alama ya urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizo.
Aidha, alisema mikutano ya mara kwa mara kati ya Rais Xi Jinping na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha uhusiano wa kimkakati na ushirikiano wa maendeleo kati ya mataifa hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma za JWTZ, Meja Jenerali Amri Mwami, alisema JWTZ linajivunia ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Tanzania na China katika maeneo ya ulinzi na usalama.
Alisema ushirikiano huo umeleta manufaa mbalimbali ikiwemo mafunzo, misaada ya kijeshi na teknolojia ya ulinzi.
“JWTZ inajivunia ushirikiano wa kidiplomasia uliopo ambao umekuwa na faida kubwa kwa nchi. Tunaipongeza China kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuleta maendeleo,” alisema.
Naye Ofisa Mambo ya Ulinzi wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, Kanali Mwandamizi Wang Haijun, alisema katika kipindi cha miaka 99, PLA limeendelea kushiriki katika majukumu ya kulinda amani katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo misheni za kimataifa za Umoja wa Mataifa.
"PLA na JWTZ zitaendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali yenye masilahi ya pamoja ili kuchangia amani na usalama wa dunia," alisema.