Jicho la CAG Bodi ya Mikopo

Muktasari:

  • Atoa angalizo kiwango cha mikopo kinachotolewa na kinachorudishwa, ashauri namba ya Nida kutumika kuomba mkopo.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),  Charles Kichere amebainisha uwepo wa hatari ya Bodi ya Mikopo ya Wanafuzni wa Elimu ya Juu (HESLB) kushindwa kukusanya mikopo iliyotolewa siku za usoni.

 Kwa mujibu wa CAG, kiwango cha mikopo kinachoendelea kutolewa na bodi ni kikubwa, lakini kinachorudishwa bado ni kidogo.

CAG katika ripoti ameainisha kinachosababisha hali hiyo ni kukosekana mfumo unaowaunganisha wadau wa kimkakati, akieleza asilimia 38 ya mikopo iliyoiva haijakusanywa kutoka kwa wanufaika.

Imeelezwa pia kuwa, kiwango cha wanufaika ambao mikopo yao imeiva na wameanza kurejesha kimekuwa kikipungua kila mwaka kati ya 2017/2018 na 2022/2023.

Wakati hayo yakiainishwa, wataalamu wa uchumi na wadau wa elimu wametaka wigo wa ajira kutanuliwa kwa wanufaika, ili waweze kupata kipato cha kurejesha mikopo.

Ripoti ya CAG kuhusu ukaguzi uliofanywa katika bodi hiyo mwaka 2022/2023 iliyowasilishwa bungeni Aprili 15, 2024 inasema kiwango cha mikopo kinachoendelea kutolewa na bodi ni kikubwa, lakini kile kinachorudishwa bado ni kidogo, jambo linaloelezwa huenda HESLB itakuwa katika hatari ya kushindwa kukusanya mikopo iliyotolewa siku za usoni.

Ripoti inaeleza hadi Juni 30, 2023 bodi ilikuwa na deni la mikopo ya wanafunzi lililoiva la Sh2.10 trilioni, lakini ni Sh1.29 trilioni ndizo zilikuwa zimekusanywa, zaidi ya Sh800 bilioni zikiwa bado zipo kwa wanufaika.

Hali hiyo inatajwa kuwa kikwazo kwa bodi kushindwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wengine wenye uhitaji.

“Kuchelewa kurejeshwa kwa mikopo kumetokana na kukosekana kwa mfumo unaowaunganisha wadau wa kimkakati, hii ni kwa sababu mkataba wa maelewano na baadhi ya wadau wa kimkakati haujakamilika, ili kuwafuatilia kwa urahisi wadaiwa waliokiuka,” imeeleza ripoti hiyo.

Mikopo ambayo haijakusanywa ni iliyoiva tangu mwaka 2006/2007, CAG akibainisha, miongoni mwa vitu vinavyochangia kuwapo urejeshaji hafifu ni kutokuwapo utambulisho wa lazima wa kutegemewa na wa kipekee kwa wanafunzi wanaopokea mikopo.

Hali hiyo pia inachangiwa na kukosekana mfumo shirikishi na wadau wa kimkakati kama utaratibu wa kuwatafuta wanufaika.

“Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inategemea nambari za mitihani ya kidato cha nne, ili kubaini wapokeaji wa mkopo. Hata hivyo, mbinu hii haiwezi kufanya kazi ipasavyo baada ya kuhitimu, huku wanafunzi wakijiajiri, au kuajiriwa, au kuendelea kusoma zaidi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

CAG amesema ili kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo kunahitaji kuwapo kwa mfumo thabiti na wa jumla wa utambulisho kama vile namba ya kitambulisho cha Taifa (Nida).

Amesema utekelezaji wa Nida kama hitaji la lazima utaiwezesha bodi kuwafuatilia wakopaji ipasavyo na kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mikopo na hatimaye kuhakikisha uendelevu wa utoaji mikopo.

“Ninapendekeza uongozi wa bodi uweke mwongozo unaohitaji uwasilishaji wa namba ya Nida kuwa ni lazima kwa waombaji wote wa mikopo wenye umri wa zaidi ya miaka 18. Waombaji walio chini ya umri wa miaka 18 wanapaswa kuwasilisha watakapofikisha miaka 18 kwa ajili ya kulipwa awamu za mikopo zinazofuata,” inaelekeza ripoti ya CAG.

HESLB iwatake wanafunzi wanaoendelea au wakopaji waliopo kutoa namba za Nida kabla ya kupokea mikopo zaidi na kuingia makubaliano na wadau wa kimkakati ili kuimarisha ujumuishaji wa mfumo huo.

Huenda wazo la matumizi ya Nida likawa linaenda sambamba na alichosema Rais Samia Suluhu Hassan, Agosti, 2023 akitaka  kuwapo namba moja ya utambulisho kwa kila Mtanzania.

“Lakini niseme na watoa huduma ndani ya Tanzania, mabenki, Wizara ya Elimu inayoandikisha Watanzania wakiwa wadogo, lakini Wizara ya Afya inayotibu Watanzania na wizara nyingine zote zinazotoa huduma, hebu sasa twendeni tukatumie namba moja tu ya Mtanzania,” alisema Rais Samia.

“Namba moja tu ya Mtanzania. Anapoambiwa Samia Suluhu ni namba 20 ndani ya Tanzania basi taarifa zangu zote, taasisi zote zikivuta namba 20 awe Samia Suluhu mmoja yuleyule taarifa zilezile,” alisema.

Rais Samia aliagiza Serikali kushirikiana na taasisi mbalimbali kuondokana na mfumo wa kutumia namba nyingi, huku akitaka mfumo utakaowawezesha kila Mtanzania kutumia namba moja ya utambulisho wake.

“Unakuta mtu ana namba moja ya Nida lakini akienda benki kuna taarifa nyingine, hospitali kuna taarifa nyingine, shule kuna taarifa nyingine. Sasa hi inasababisha ata usalama ndani ya nchi unakuwa wa wasiwasi kidogo,” alisema.

Agizo hilo tayari limeshaanza kufanyiwa kazi kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Benedict Ndomba kupitia kauli  aliyoitoa Machi 8, 2024 katika mkutano wa taasisi za kifedha, mkutano uliofanyika jijini Arusha.

“Rais ametoa maagizo kuwe na namba moja ya utambulisho maalumu kwa Watanzania wote na kazi hii imeanza chini ya Wizara ya Mawasiliano na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa. Wanafanya kazi pamoja kuileta Jamii Namba, namba maalumu ya utambulisho kwa kila Mtanzania kuanzia anapozaliwa, na kwa wageni kuanzia wanapoingia nchini mpaka wanapoondoka,” alisema Ndomba.


Warejeshaji wapungua

Ukitafutwa ufumbuzi wa kudumu wa kuwapata watu ambao watarejesha mikopo, ripoti ya CAG inaonyesha kiwango cha wanaorejesha mikopo kimekuwa kikishuka kati ya mwaka na mwaka.

Mwaka 2017/18, jumla ya wanufaika ambao mikopo yao ilikuwa imeiva walikuwa 293,827 lakini waliokuwa wakilipa ni 115,004 sawa na asilimia 39.

Kiwango hicho kilishuka hadi kufikia asilimia 23 mwaka wa fedha 2022/23 ikiwa na maana kuwa, kati ya wanufaika 486,549 ambao mikopo yao ilikuwa imeiva ni 112,582 waliokuwa wakirejesha.

Hali hiyo inatajwa kuchangiwa na ufuatiliaji hafifu wa wanufaika wa mikopo hiyo, takwimu zikionyesha kati ya ambao mikopo yao ilikuwa imeiva hadi mwaka jana ni 224,050 waliopatikana.

 Taarifa kutosomana      

Kutofautiana kwa taarifa za urejeshaji wa mikopo ni miongoni mwa changamoto zilizobainika katika ripoti ya CAG.

Imeelezwa kumekuwa na mkanganyiko wa taarifa za wanufaika na kiwango cha deni ambacho wanadaiwa pindi wanapoangalia taarifa za mishahara (Salary slip) na wanapoangalia deni katika mfumo wa bodi.


Nini kifanyike

Mtafiti wa elimu, Muhanyi Nkoronko amesema ili watu waweze kurejesha mikopo kwa kiasi kikubwa inatakiwa kutafutwa namna bora ya kutoa fursa sawa kwa watu waliomaliza vyuo, ili waweze kuajiriwa na kuajirika ili wapate kipato kwa ajili ya kurejesha mikopo HESLB.

Ameeleza wengi ambao wanalipa mikopo kwa sasa ni ambao wameajiriwa serikalini, lakini urejeshaji kwa wengine bado ni hafifu.

“Lakini njia nyingine inayoweza kusaidia ni bodi kushirikiana na benki katika utoaji wa mkopo, urejeshaji wake utakuwa ni mkubwa kwa sababu mzazi anaomba kama mikopo mingine,” amesema Nkoronko.

Mtaalamu wa uchumi, Dk Donath Olomi amesema kukosekana ajira rasmi ni moja ya sababu ya urejeshaji hafifu wa mikopo, akitaka ufanyike mchakato wa kujenga uchumi, ili kutanua wigo wa ajira unaokwenda sambamba na wanufaika kusoma kile kinachohitajika sokoni.

“Siku hizi mtu anasoma anamaliza sheria lakini ukiongea naye unaona kabisa huyu hawezi kuwa mwanasheria, hana wito na hata hakijui anachokifanya. Unaona kabisa huyu labada angesomea ufundi,” amesema Dk Olomi.

Amesema ipo haja ya kujenga mfumo utakaosaidia kuandaa kitu kinachohitajika sokoni jambo ambalo litaongeza upatikanaji wa ajira na kuongeza marejesho.

“Lakini hata wanaopata ajira hakuna mfumo mzuri wa kuwafuatilia ili waanze kurejesha mkopo kwa kiasi kidogo, hivyo ni vyema kuboresha mfumo ili kuwafuatilia wanufaika hao,” amesema.

Maoni ya wawili hao yanaungwa mkono na mmoja wa wanufaika wa mikopo ambaye anakiri kutoanza kurejesha kutokana na kukosa ajira.

“Nilimaliza ualimu mwaka 2015 mpaka sasa nafanya shughuli zangu nyingine, kiwango cha fedha ninachokipata hakitoshi kulipa deni la kila mwezi la Bodi ya Mikopo, nia tunayo lakini kipato ndiyo tatizo,” alisema akiomba hifafhi ya jina lake.

Kutokana na kiwango cha deni kuongezeka, amesema kuna wakati alilazimika kutafuta kiasi cha fedha na kurejesha ili kuondoa riba.


Bodi yazungumza

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia amesema wamepokea ushauri waliopewa na CAG na wameufurahia.

“Alichosema CAG ndicho tulitamani kiwe hivyo, na tunatamani tuelekee huko kwa kuwa moja kati ya changamoto tulizonazo kama HESLB ni urejeshwaji wa mikopo hasa katika sekta isiyo rasmi. Hii tukiifanyia kazi kwa kuwapo ushirikiano na Nida itatusaidia sana katika kuwafuatilia wale wanufaika wa mkopo waliopo kwenye sekta isiyo rasmi,” amesema.

Amesema hilo likifanyika litasaidia kukuza mfuko wa bodi uweze kutoa mikopo zaidi kwa wanafunzi.