CAG: Makato ya HESLB yamepitiliza
Muktasari:
- CAG amebaini mabadiliko ya makato ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu yaliyopanda kutoka asilimia nane mpaka 15 yamesababisha baadhi ya wafanyakazi kukatwa zaidi kuliko inavyokubalika kisheria.
Dar es Salaam. Unakikumbuka kilio cha wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kukatwa kinyume na mkataba walioingia, basi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini makato hayo ni makubwa sana na yanavunja sheria ya marejesho.
Kwa utaratibu uliopo, mfanyakazi anayekopa kwa makubaliano ya kukatwa mshahara wake ni lazima abakiwe na kiasi kinachomtosha kujikimu mahitaji muhimu ya maisha ya kila siku.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kurejesha Madeni ya mwaka 1970 na waraka wa katibu mkuu wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Machi 2009, mfanyakazi hatakiwi kukatwa zaidi ya theluthi mbili ya mshahara wake ghafi kwa mwezi.
Hata hivyo, katika ukaguzi wa mishahara ya watumishi kwa mwaka 2019/20, CAG amebaini taasisi 10 zenye watumishi 112 wanaopokea mshahara chini ya theluthi moja kwa mwezi.
“Nilibaini upungufu huu unatokana na sheria mpya ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iliyoongeza makato ya wanufaika kutoka asilimia nane hadi 15 ya mshahara,” amesema CAG kwenye ripoti yake.
Wafanyakazi sita, CAG amebaini wapo Wizara ya Viwanda na Biashara wakati Wizara ya Afya ikiwa nao 13 na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ikiwa na wengi zaidi, 24.
Mkoa wa Kilimanjaro unao 10 na Tanga sita wakati Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wanane. Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi wapo sita huku Hospitali ya Mirembe na Chuo cha Isanga wakiwa 22. Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania wapo 12.
Hata hivyo, CAG anasema watumishi wanaokatwa zaidi ya kiasi kinachokubalika kisheria wamepungu kwa asilimia 16 ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2018/19 alipowabaini 134.
“Naendelea kuzishauri taasisi husika kuzingatia sheria zinazohusu makato na ulipaji mishahara. Taarifa zaidi kuhusu upungufu huu inaoneshwa,” ameasa Kichere.
CAG anasema kutodhibiti kiwango cha makato ya mishahara kwa watumishi, kunaweza kuathiri utendaji na ufanisi wao hivyo kushusha ufanisi wa taasisi za Serikali kwa ujumla.
Kwa kuwa suala hili linajirudia kwenye ripoti zake, CAG anawashauri maofisa masuuli kuhakikisha wanadhibiti uidhinishaji mikopo na kufanya mawasiliano ya karibu na taasisi za fedha ili kutotoa mikopo kwa wafanyakazi kinyume na kiwango kinachotakiwa.