CAG : Mradi wa umeme bwawa la Nyerere unatumia upembuzi wa mwaka 1970

CAG : Mradi wa umeme bwawa la Nyerere unatumia upembuzi wa mwaka 1970

Muktasari:

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeshindwa kuhuisha vipengele vyote vya upembuzi yakinifu uliofanyika awali katika ujenzi wa mradi wa umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), imeeleza ripoti ya Mdhibiti na  Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeshindwa kuhuisha vipengele vyote vya upembuzi yakinifu uliofanyika awali katika ujenzi wa mradi wa umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), imeeleza ripoti ya Mdhibiti na  Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

Badala yake ripoti hiyo ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 2020 imesema Tanesco lilitegemea upembuzi yakinifu ambao ulifanywa katika miaka ya 1970 na 1972 na kampuni ya M/S Norconsult ya Norway.

Pia shirika hilo linatumia mpango mtambuka wa mradi na ripoti ya uchunguzi wa kiufundi uliofanywa na kampuni ya M/S Hafslund na M/s Norplan pia kutoka Norway ambayo ilihuisha vipengele vya taarifa ya upembuzi yakinifu miaka ya 1980.

“Vipengele ambavyo havikufanyiwa mapitio na kuhuishwa ni pamoja na utafiti wa kiuchumi na kifedha wa mradi, tafiti za kuwepo kwa maji na uendeshaji endelevu wa mradi,” imesema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo imesema maofisa waandamizi wa Tanesco waliozungumza na CAG walieleza kwamba, upembuzi yakinifu uliofanyika katika miaka ya 1970 ulionesha kwamba mradi unawezekana kitaalamu, kiuchumi na kifedha.

“Maofisa waliongeza kuwa kutokana na uharaka wa kuanza utekelezaji wa mradi, taarifa za upembuzi za awali hazikuweza kupitiwa upya zote ili kuzihuisha,” inaeleza.

Ripoti hiyo imesema kuhuishwa huko kwa upembuzi kunatakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Umeme ya mwaka 2008, Sheria ya Umwagiliaji ya Kitaifa ya mwaka 2013, Sheria za Usimamizi ya Vyanzo vya Maji ya mwaka 2009 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004.