CAG: Wafanyakazi 1,538 ujenzi reli ya kisasa hawana vibali vya kazi

CAG: Wafanyakazi 1,538 ujenzi reli ya kisasa hawana vibali vya kazi

Muktasari:

  • Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya miradi ya maendeleo inaeleza kuwa wafanyakazi wa kigeni 1,538 kati ya wafanyakazi  2,408 wa kigeni wanaojenga reli ya kisasa kipande cha kwanza na cha pili kutoka Dar es Salaam hawakuwa na vibali vya kazi.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya miradi ya maendeleo inaeleza kuwa wafanyakazi wa kigeni 1,538 kati ya wafanyakazi  2,408 wa kigeni wanaojenga reli ya kisasa kipande cha kwanza na cha pili kutoka Dar es Salaam hawakuwa na vibali vya kazi.

Ripoti hiyo ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 20, 2020 iliyotolewa leo Alhamisi Aprili 8, 2021 inaeleza kuwa hali hiyo ni kinyume na Kifungu cha 9 (2) (a) cha Sheria za Ajira za Raia wa Kigeni ya mwaka 2015. 

“Mapitio ya ripoti ya maendeleo ya kazi ya mwezi wa Novemba 2020 yalibaini kuwa jumla ya raia wa kigeni 586 kati ya 924 walioajiriwa kwenye kipande cha kwanza cha ujenzi wa reli ya kisasa hawakuwa na vibali vya kufanya kazi.”

“Hali hii pia ilibainika kwenye kipande cha ujenzi cha pili ambapo ilibainika kuwa jumla ya raia wa kigeni 952 kati ya 1,484 hawakuwa na vibali vya kufanya kazi,” inaeleza ripoti hiyo ya miradi ya maendeleo.

Inabainisha kuwa kutozingatiwa kupata vibali vya kazi kulisababisha kutolipwa kwa ada ya vibali vya kazi inayofikia Dola za Marekani 1,538,000 ambazo ni sawa na Sh3,537,400,000 (kiwango cha ubadilishaji kilichotumika ni 2,300).

“Mahojiano zaidi na maafisa wa TRC (Shirika la Reli Tanzania) yalionesha kuwa idara ya uhamiaji ilitoa idhini ya raia hao wa kigeni kutumia visa ya biashara kuendelea kufanya kazi wakati maombi yao ya vibali vya kazi yakishughulikiwa.”

“Hata hivyo, ilielezwa wazi katika barua hiyo kwamba kutolewa kwa viza ya biashara hakikuwa kisingizio cha kutokuwa na vibali vya kufanya kazi kwa raia hao wa kigeni walioajiriwa katika mradi wa SGR,” imesema ripoti hiyo.

CAG pia amebainisha kuwepo kwa raia wa kigeni 1,026 wanaofanya kazi katika mradi wa SGR (kwa vipande vyote viwili) wasio na vyeti vya sifa zao za masomo.

“Ripoti ya Maendeleo ya kazi ya mwezi wa Novemba 2020 ilionesha kuwa, vyeti vyao vilikuwa vikiendelea na michakato anuwai ya uthibitishaji. Hata hivyo, asilimia 83 kati yao bado walikuwa wakisubiri kwa sababu ilibainika waombaji hawakuwa na vyeti halisi vya masomo na walikuwa wakingojea kuvipokea kutoka Uturuki,” ameeleza.