Jicho letu mahakamani: Magafu achambua udhaifu wa ushahidi wa Jamhuri (57)

Muktasari:

  • Katika sehemu ya 56 ya simulizi hii ya Kesi ya Zombe, tuliona jinsi wakili wa mshtakiwa wa pili, SP Bageni, Gaudioz Ishengoma alivyopambana kumnusuru mteja wake huyo kwa hoja akijaribu kuishawishi mahakama imuone hana kesi ya kujibu na hivyo imwachie huru.

Katika sehemu ya 56 ya simulizi hii ya Kesi ya Zombe, tuliona jinsi wakili wa mshtakiwa wa pili, SP Bageni, Gaudioz Ishengoma alivyopambana kumnusuru mteja wake huyo kwa hoja akijaribu kuishawishi mahakama imuone hana kesi ya kujibu na hivyo imwachie huru.

Hii ni simulizi ya kina ya Kesi ya Zombe, kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe, Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID) ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni na askari wengine 11.


Washtakiwa hao walikuwa wakidaiwa kuwaua kwa makusudi wachimba madini watatu kutoka Mahenge wilayani Ulanga mkoani Morogoro, Sabinus Chigumbi maarufu Jongo, mdogo wake Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam aliyekuwa akiwaendesha.

Walikuwa wakidaiwa kuwapiga risasi katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam Januari 14, 2006, baada ya kuwatia mbaroni Sinza Palestina, nyumbani kwa mchimbaji mwenzao.

Katika sehemu hii ya 57 leo tunaangazia hoja za wakili Majura Magafu, aliyekuwa akiwatetea aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Urafiki, (OC-CID), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ahmed Makelle na wenzake watano.

Katika hoja zake, Wakili Majura Magafu anayewatetea washitakiwa saba katika kesi hiyo, alidai kuwa kesi hiyo ni ya kupika yenye lengo la kuwaharibia washitakiwa kazi, maisha na vyeo vyao. Naye alikuwa na haya ya kusema na ninamnukuu:

Kifungu cha 293(1) na 293 (2) vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai vinaitaka mahakama iamue iwapo upande wa mashtaka umeleta ushahidi usio na mashaka kwa kosa la watuhumiwa kiasi kwamba hata wakikaa kimya mahakama itaona tu kuwa wana hatia.

Katika tuhuma za mauaji ambalo ni kosa kinyume cha kifungu cha 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ili mshtakiwa atiwe hatiani lazima mahakama iridhike na ushahidi kuwa alitenda/hakutenda jambo lililosababisha kifo.

Upande wa mashtaka wanajua wajibu huo na tuliamini wataleta ushahidi wa kutosha usioacha mashaka kuwa washtakiwa walitenda kosa gani, lakini bahati mbaya haikufanyika hivyo.

Katika kesi hii kuna ushahidi wa mazingira tu, hakuna ushahidi wa moja kwa moja. Huu ni sawa na mnyororo uliokatika unahitaji kuungwa, maana huu ni kama mnyororo uliokatika lazima uungweungwe ili uwafunge watuhumiwa.

Kwa ujumla robo tatu au ushahidi wote ni wa kuambiwa tu hakuna aliyeshuhudia. PW2, Bernard, PW6, Mjatta Kayamba na PW7, Hadija Mohamed Chaka ushahidi wao si mzuri, maana walizungumzia tu kukamatwa kwa marehemu (wachimba madini) na polisi ambao hawakuwafahamu majina wala kutambua mahali walikokwenda.

Kesi kama hii utambuzi watuhumiwa ni muhimu sana. Mahakama inapaswa kujiuliza kuwa nani walihusika na mauaji haya maana hadi leo tuko gizani.

Mashahidi hawa watatu hawajawahi kupelekwa kwenye gwaride la utambuzi wa watuhumiwa waliokuwapo wakati wa kuwakamata (wachimba madini hao) kinyume cha kifungu cha 60 cha CPA.

Mkumbi (kiongozi wa timu ya Polisi iliyoundwa kufanya upelelezi wa mauaji hayo baada ya ripoti ya Tume ya Jaji Mussa Kipenka (iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza ukweli wa mauaji hayo) alisema hajui kwa nini DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) aliamua washtakiwe wachache badala ya wengi.

Kama hakuna hujuma kwa nini wengine wabaki? Inaleta mashaka kuwa wasiokuwepo ndio waliohusika na mauaji. Nina imani hawa hawakuhusika, wametolewa kafara tu kwa matakwa ya wakubwa.

PW2 na PW6 wanasema mshtakiwa wa tatu, ASP Makelle, wa tano, WP Koplo Jane Andrew na wa 10 Koplo Abeneth Saro walikuwepo eneo la tukio na hawakuwa na silaha.

Kwa ushahidi wa PW24, SSP Sebastian Masinde (aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Chuo Kikuu) askari wote waliotajwa waliokuwa wamepewa silaha (siku ya tukio) zilirejeshwa salama bila kutumika.

Swali ni kwamba wengine (waliopaswa kuunganishwa kwenye kesi kati ya askari 15) wako wapi, ni siri ya upelelezi na waendesha mashtaka.

Kwa kushindwa kuwaunganisha washtakiwa hao, upande wa mashtaka umefanya jitihada kuwapata mshtakiwa wa 11 (Koplo Rashid Lema) na wa 12 (Koplo Rajabu Bakari) kutoka mafichoni, wakiongozwa na ofisa mkubwa wa polisi wanasema mauaji yalitokea msituni Pande wakiongozwa na mshtakiwa wa pili.

Katika maelezo yao, hakuna swali waliloulizwa kuwa ni kwa nini walikimbia, ili kupata ukweli. Zinaleta shaka kuwa ziliandikwa makusudi ili kuwaunganisha washtakiwa.

Ushahidi wao ni wa kupikwa kwa sababu, PW25 (Shabani Manyanya) na PW26 Ramadhan Tupa walidai kuwa ndio waliohusika na uporaji wa pesa kwenye gari la kampuni ya Bidco.

Inatia mashaka kwa sababu hadi tunakuja hapa mahakamani PW25 na PW26 wako huru. Hivi ndivyo sheria inavyotaka kwa jambo ambalo lilileta mtafaruku na kusababisha watu kufa?

Pamoja na kulalamika, hadi PW36 (SACP Mkumbi kiongozi wa timu ya upelelezi) anatoa ushahidi hapa walikuwa hawajachukuliwa hatua.

Katika maelezo ya washtakiwa wa 11 na wa 12 (washtakiwa waliotoa siri ya mauaji hayo) zinaonesha walikuwa na maslahi ya kujinasua maana nao walihusika.

Ushahidi wa mtuhumiwa ni lazima uungwe mkono na ushahidi mwingine ambao ni huru, lakini hapa hakuna ushahidi huru unaounga au unaotumiwa na upande wa mashtaka. Maelezo ya mshtakiwa wa 11 na wa 13 yamezua utata wa mahali mauaji yalikotokea.

Ripoti ya PW37 (David Elias, Mkemia Mkuu Daraja la II aliyechunguza sampuli za udongo uliodaiwa kuwa na damu) inaonesha kulikuwa na mapigano Sinza ukuta wa Posta kati ya askari na majambazi (wachimba madini waliouawa) (maana sampuli hizo alizozichunguza zinadaiwa kuchukuliwa eneo hilo).

Sasa nani wa kumwamini kati ya timu ya upelelezi ya SACP Mgawe na PW37 pamoja na washtakiwa wa 11 na wa 12?

Si jukumu la washtakiwa kuthibitisha kosa, bali ni jukumu la upande wa mashtaka. La kusikitisha mashahidi wa upande wa mashtaka mmoja anasema Sinza (mauaji yalikotokea) mwingine Pande (msituni) sasa washtakiwa waseme nini?

Upande wa mashtaka ndio ulitakiwa uondoe hayo mashaka, lakini mpaka leo yapo.

Tumekwenda Sinza tumeona ushahidi wa matundu (ukuta wa Posta) na ushahidi wa Nickobay (PW33) wa damu (kupatikana eneo hilo) na PW22 alikiri. Wote hawa ni mashahidi wa Jamhuri.

Wakati huohuo PW30, PW31, PW36 nao walipelekwa msitu wa Pande na mshtakiwa wa 11 nao wakakuta damu za watu, which is which? Kulikuwa na matukio mawili? Nani wa kuyatatua? Ni upande wa mashtaka hawajaleta ushahidi.

Maelezo ya mshtakiwa wa 11 kuwa mauaji yalifanywa na Koplo Saad yako wapi mahakamani? Wala maelezo yake hasemi kama alikuwepo (Saad) Sinza (mahali walikotiwa mbaroni wachimba madini wale).

PW8, PW9 na PW10 walisema hapakuwa na mapambano katika eneo la ukuta wa Posta. Timu ya SACP Mgawe (timu ya awali ya upelelezi wa mauaji hayo iliyoundwa na Jeshi la Polisi) ilisema yalikuwepo. Sasa nani mahakama imwamini? Washtakiwa waseme nini.

Hizo zote ni contradiction (mikanganyiko) ya mashahidi wa upande wa mashtaka. Hivyo Mheshimiwa Jaji ninaomba mahakama yako tukufu iseme kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuleta ushahidi wa kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka.

Kama ushahidi huu si wa kupikwa na hawajaletwa (mashahidi) kwa nia mbaya, mshtakiwa wa kwanza hakufika msitu wa Pande na hata maelezo ya washtakiwa wa 11 na wa 12 hayamtaji. Sasa tusijekuwa tunaumiza vichwa kumbe kesi yenyewe ni ya kutambiana kazi, vyeo na sifa.

Kuna ushahidi wa tukio la Bidco, upande wa mashtaka hawajaeleza mchakato wake (upelelezi na hatua) uliishia wapi, Ni aibu kina Manyanya (shahidi wa 25 aliyesema ndio waliopora pesa za Bidco) bado Serikali inasema ni mashahidi wake.

Kwa maelezo ya Ndaki (PW23 Juma) aliyekuwa Mkuu wa kituo cha Polisi Urafiki, kuwa mshtakiwa wa Nne, Koplo Frank Noel na wa Sita Morris Nyangelera, walirudisha gari la watuhumiwa wa ujambazi (wachimba madini) kulipeleka Urafiki.

Hakuna ushahidi mwingine wa kurudi kuzungumza na wenzao na kwenda msitu wa Pande.

Kwa hiyo Mheshimiwa Jaji na Waungwana Wazee wa Baraza, ni rai yangukwamba washtakiwa wote waonekane kuwa hawastahili kusimama kizimbani kujitetea kwani hawana kesi ya kujibu, hivyo waachiliwe huru, isipokuwa mshtakiwa wa 11 na wa 12 kama mahakama itaona kuwa kuna ushahidi wa kutosha ingawa naamini hakuna yawezekana nao walidanganywa tu.

Nini kitaendelea katika kesi hii iliyotikisa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania? Kesho usikose kununua gazeti la Mwananchi ujue yaliyojiri.