Jina la baba wa Anthony linavyoakisi shida zake

Muktasari:

Anthony (10), anasema kwamba mchana anashindia andazi na maji ambavyo anavipata kwa kuomba mitaani wakati jioni mlo uliozoeleka nyumbani ni maparachichi na mafenesi ambayo miti yake imepandwa kuzunguka nyumba yao.

Kwa familia nyingi za Kitanzania watoto hufurahi unapopikwa wali nyumbani, lakini kwa Anthony Petro Magogwa nyumbani kwao wali hauna nafasi, baba yake Mzee Petro Magogwa hana uwezo wa kununua mchele ili watoto wake wale wali.

Anthony (10), anasema kwamba mchana anashindia andazi na maji ambavyo anavipata kwa kuomba mitaani wakati jioni mlo uliozoeleka nyumbani ni maparachichi na mafenesi ambayo miti yake imepandwa kuzunguka nyumba yao.

Wakati mwingine Anthony na dada zake wawili, Editha (13) na Eliza (9) hunywa uji ambao pia unaweza usipatikane, yote ni kutokana na ugumu wa maisha unayoikabili familia hiyo.

Shughuli pekee anazofanya baba yake ni kilimo cha maparachichi na mihogo, mahindi, maharage na mazao ya jamii ya kunde ambayo hata hivyo hustawi kwa tabu kwa kuwa ardhi haina rutuba, kazi nyingine anayofanya mzee huyo ni ya kubatahisha, kazi inayoakisi shida alizonazo ambazo pia zinahusishwa na maana ya jina lake la Magogwa ambalo linamaanisha mtu anayeishi maisha ya kubahatisha.

Kazi hiyo ni ya kuokota chupa za plastiki na kuziuza, ni kazi ya kubahatisha, kipato chake kidogo na wakati mwingine asipate kitu.

“Huwa nauza chupa kwa wauza pombe, wananipa Sh500 wakati mwingine Sh2000 ambazo nanunulia unga kwa ajili ya watoto lakini wakati mwingine sipati kitu,’’ anasema akionekana mwenye kutaka kulia.

Ugumu wa maisha ni sababu tosha iliyomfanya Anthony ageuke ombaomba mitaani, anapenda zaidi kwenda kuomba mpakani mwa Tanzania na Burundi maeneo ya Kobero na Kabanga hali ambayo wakati mwingine humfanya akose masomo.

Akizungumzia ugumu wa maisha, Mzee Magogwa anasema kwamba alikuwa na shamba katikati ya kijiji lakini aliliuza kwa Sh 120,000 ili apate fedha za kujiuguza yeye na mkewe aliyekuwa mgonjwa pamoja na kumudu gharama nyingine za maisha lakini baadaye mkewe alifariki.

Baada ya kufiwa na mkewe, alioa mke mwingine kutoka Burundi na kuzaa naye watoto wanane, saba walifariki, baadaye mwanamke huyo alitoroka na kurudi kwao Burundi. “Mke wangu wa tatu aliyezaa watoto hawa alifariki na kuacha mtoto mchanga wa siku nane, nilihangaika kumlea ingawa alifariki baada ya miezi minane,” anasema Mzee Magogwa huku akiwa mwenye kulia kwa kwikwi.

“Nilimkosea nini Mungu jamani maisha haya lakini yeye ndiye muweza huenda atanibariki,” anasema akijipa matumaini.

Pamoja na kuuza shamba lake lakini ndoto aliyokuwa nayo mzee huyo ni kutenga eneo katika shamba lililobaki kwa ajili ya watoto wake akiwamo mvulana mmoja aliyeko Burundi anayedai aliondoka na dada zake wawili walioolewa baada ya kufariki mama yao.

Hali ilivyozidi kuwa mbaya kiuchumi, wazo la kuuza shamba hilo lilimjia Mzee Magogwa lakini wakati akitaka kulifanyia kazi wazo hilo ndipo alipoibuka Anthony na kujipatia umaarufu.

Anthony pamoja na utoto wake aliibuka na kuamua kumshitaki baba yake Kituo cha Polisi Kabanga ili kuzuia shamba hilo lisiuzwe, habari hiyo ilimpa umaarufu kiasi kwamba juhudi za kukusanya michango zimeanza kufanyika kwa lengo la kuboresha maisha ya familia hiyo.

“Alitaka kuuza shamba ili tukaishi wapi na tukalime wapi au tutatunzwa na nani, niliamua kwenda polisi,’’ anasema Anthony katika kauli ya kijasiri iliyomfanya awe gumzo kwenye mitandao ya kijamii.

Jina la Magogwa

Matatizo na dhiki zilizomzunguka Mzee Magogwa zinaakisi maana halisi ya jina lake, kwa mujibu wa mzee huyo, jina la Magogwa linamaanisha mtu aliyepitia katika shida na misukosuko katika maisha na alipewa jina hilo na baba yake, Niyonsaba.

Inadaiwa kwamba jina hilo hutumika kwa jamii ya waha wa Kigoma, waangaza na washubi wa Ngara pamoja na wenyeji wa Rwanda na Burundi likimhusisha na mtu aliyepoteza matumaini ya jambo analofanya na hivyo kuwa mwenye kuishi na kufanya mambo yake kwa kubahatishabahatisha.

Maisha ya Anthony shuleni

Anthony ambaye ndio kwanza yuko darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ngundusi kata ya Kabanga wilayani Ngara mkoani Kagera, ndoto yake ni kuwa mwalimu akiwa na lengo la kuwasaidia wanafunzi kitaalum ingawa ili kufikia lengo hilo anajua kwamba anahitaji kuwa mwanafunzi bora na mwenye kujiamini.

Anthony anakiri kuwa maisha ya familia yao ni shida tupu lakini hali hiyo haijamtoa katika dhamira yake ya kuhakikisha anasoma na kufika mbali na hapo anakuja na kauli nyingine ya kijasiri kwa kusema, “hapa hakuna wa kutusaidia ila namshukuru Mungu nikishiba nikaenda shule nataka niwafundishe na wengine.”

Deniza Rutazika ambaye ni mwalimu wa darasa la kwanza katika shule anayosoma Anthony, anasema Anthony akipatiwa chakula na kuwa katika mazingira salama anaweza kuhudhuria masomo yake na kuwa mwanafunzi bora kitaaluma kutokana na kujiamini kwake.

Mwalimu Deniza anasema mara kwa mara mwanafunzi huyo amekuwa akionyesha mshikamano wa kujali familia na anapohudhuria masomo japo ni mara chache kwa sababu ya uduni wa maisha, amekuwa akifanya vizuri darasani baada ya kuelekezwa ingawa dada zake wanamzidi kitaaluma

“Huyu mtoto si mtoro bali anatingwa na mawazo ya familia akibaini baba yake ni mzee na mazingira yao ni shida sana hivyo akisaidiwa mazingira rafiki atafanya vizuri,” anasisitiza mwalimu huyo.

Anaongeza kuwa jamii inamuunga mkono Anthony kwa kuzuia baba yake kuuza shamba kwa sababu yeye na wadogo zake hakuna sehemu wanayoweza kwenda, isipokuwa watakuwa watoto wa kuzurura na kuitwa wanaoishi katika mazingira magumu licha ya kuwa wana baba ambaye yupo hai.

Wanafunzi wa shule hiyo nao wamemzungumzia Anthony kwamba ni mwenye upendo lakini shuleni anafika mara chache, muda wote hufikiria familia jinsi itakavyopata chakula, ni kijana pekee anayetetea haki za wadogo zake pia anayependwa na baba yake.

Uongozi wa kijiji

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngundusi, Paul Henerico Kitungwa amekiri Mzee Magogwa kuwa miongoni mwa watu maskini na kuna wakati amekuwa akisaidiwa na waumini wa Jumuiya ya Kikristo ya Kikatoliki na wasamaria wema wengine.

Henerico anasema kijiji hicho hakijaingizwa kwenye mpango wa kusaidia kaya maskini ndani ya wilaya licha ya kuwepo familia kama za Mzee Magogwa ambaye hata mazingira anayoishi si salama hivyo ikiwezekana wasamaria wema wajitokeze na kuwanunulia shamba jingine.

Ameahidi kusimamia misaada na michango itakayotolewa ili ajengewe nyumba ya kuishi karibu na watu maana watoto wake wanatembea kilomita tatu kutoka nyumbani hadi shuleni na hawana huduma za kijamii kama maji, afya na huduma nyinginezo muhimu.

“Hofu yetu wakijitokeza wa kumsaidia akiendelea kukaa kwake hata akijengewa nyumba usalama wa mazingira bado si mzuri, kwa niaba ya Serikali ya kijiji naahidi kutafuta eneo tumpatie ili aishi jirani na wananchi wenzake,” anasema mwenyekiti huyo.

Conibert Stephano ni jirani yake Mzee Magogwa ambaye anamiliki shamba la miti lakini anaishi Kabanga, umbali wa kilomita nane, Stephano alipendekeza mzee huyo kuhamishiwa ili aishi karibu na watu ambako anaweza misaada kwa urahisi.

Ustawi wa Jamii

Ofisa Ustawi wa Jamii wilayani Ngara, Musa Niyonsaba Balagondoza ametembelea shule ya msingi Ngundusi na kubaini tatizo katika mahudhurio ya Anthony, ofisa huyo alifika kwa baba yake na kusema Serikali na jamii wakiungana mtoto huyo na ndugu zake wanaweza kusaidiwa.

Amesema idara yake inasimamia na kulinda haki za watoto kwa mujibu wa sheria namba 21 ya mwaka 2009 hivyo familia itafunguliwa akaunti benki kupitia Benki ya CRDB Ngara ili wenye kuguswa na maisha ya Anthony na wadogo zake waweze kuwasaidia.

Pia ofisa huyo aliwashukuru wananchi walioibua tatizo la mtoto huyo na kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari akiisifia Mwananchi Digital, iliyoonyesha hali halisi ya familia hiyo hadi baadhi ya watu kuguswa na kuanza kujitokeza kutoa misaada.

Pia aliwashauri viongozi wa serikali ya kijiji kupaza sauti zao kuhakikisha Kijiji cha Ngundusi kinaingizwa kwenye mpango wa kusaidia kaya maskini kupitia Tasaf na kwamba familia hizo ikiwemo ya Magogwa zipate ruzuku ya fedha kila mwezi.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ngara, Aidan Bahama amesema Anthony amepata mfadhili wa kumsomesha Shule ya Same, Kilimanjaro na wadogo zake watasomeshwa Shule ya Kibwa English Medium iliyoko Kabanga, Ngara huku wafadhili wengine wakiendelea kutafutwa.

Alisema akaunti itakayofunguliwa itakuwa chini ya watia saini ambao ni baba wa Anthony na mlezi wa kiroho Padre Pamphilius Kitondo wa Parokia ya Ntungamo Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara.