Jinsi Dola 3,900 zilivyomtupa jela bosi wa  kampuni ya Utalii Arusha

New Content Item (2)

Muktasari:

  •  Majaliwa Gogo alipokea kundi la watalii 17 kutoka India walioingia nchini kupitia mpaka wa Namanga kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Manyara, Serengeti na Ngorongoro kwa gharama ya Dola 18,657 za Marekani (Sh47 milioni).

 Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imemhukumu Mkurugenzi wa kampuni ya Expedition Africa Limited, Majaliwa Gogo, kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela na kulipa faini ya Sh2 milioni kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Gogo alipokea kundi la watalii 17 kutoka India walioingia nchini kupitia mpaka wa Namanga kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Manyara, Serengeti na Ngorongoro kwa gharama ya Dola 18,657 za Marekani (Sh47 milioni).

Kwa kuwa kampuni yake ilikuwa haijakata leseni ya utalii inayojulikana kama Tourist Agency License (Tala), mshitakiwa alimuomba shahidi wa pili, Christian Ayo ili atumie kampuni yake ya West Way Safaris kwa ajili ya kuwapeleka watalii hao hifadhini.

Licha ya kulipwa fedha hizo na Pradeep Mogasati ambaye ni mmiliki wa kampuni ya utalii inayofanya shughuli zake Jijini Nairobi Kenya, Gogo hakulipa ada stahiki katika malango ya kuingia katika hifadhi hizo akisingizia akaunti zake zimefungwa na Serikali.

Safari ya watalii hao ilianza Desemba 22,2022 wakielekea Hifadhi ya Taifa ya Manyara, lakini wakiwa njiani, Mogasati akapokea ujumbe mfupi (SMS) kutoka kwa mkurugenzi huyo kuwa ada katika hifadhi hizo hakuwa amezilipa kwa sababu akaunti zimefungwa.

Mkurugenzi huyo akamuomba Mogasati kulipa ada hizo kwa masharti kuwa angezirejesha fedha hizo mara tu akaunti yake ikifunguliwa na Serikali, hivyo Mogasati akalipa Dola 7,800 za Marekani, sawa na zaidi ya Sh19.5 milioni za Tanzania.

Kulingana na hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi, Regina Oyier,  Machi 15,2024 na nakala yake kupatikana leo Alhamisi Aprili 11, 2024, inasema mshitakiwa hakurejesha fedha hizo na Mogasati alipokuwa akimpigia simu na kumtumia SMS, alikuwa hapokei wala kujibu.

Hata hivyo, siku moja walikutana Jijini Arusha ambapo aliahidi kulipa fedha hizo Januari 3, 2024 lakini hakulipa ndipo Mogasati akafungua malalamiko kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia na kesi kupelelezwa kwa weledi na Mrakibu wa Polisi (SP), Waziri Tenga.

Baada ya upelelezi kukamilika, mkurugenzi huyo akafikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuendesha biashara ya utalii, makosa ambayo mahakama ilimtia hatiani Machi 15,2024.

Katika utetezi wake, mkurugenzi huyo alikana kumfahamu shahidi wa tatu, Mogasati wala kufanya naye biashara yoyote inayohusiana na utalii na pia akakana kumiliki kampuni yoyote ya utalii, bali anajishughulisha na asasi ya kulinda haki za watalii.


Hukumu ilivyokuwa

Akisoma hukumu dhidi ya mshitakiwa, Hakimu Oyier alisema shahidi wa tatu alieleza  kuwa Novemba 2022 alikuja Arusha na kupokelewa na mshitakiwa ambaye alimpeleka hotelini, na siku iliyofuata walifanya mazungumzo kuhusiana na biashara ya watalii 17.

“Ni mshitakiwa ndiye aliyependekeza maeneo ambao watalii hao watatembelea na gharama ya safari nzima. Lakini hiyo haikuwa siku pekee ambapo walikutana bali walikutana tena Arusha Desemba 22,2022 na Mto wa Mbu Desemba 26,2022”alieleza.

“Ni dhahiri kuwa shahidi huyo alimfahamu mshitakiwa vizuri na Dola 12,000 ambazo mshitakiwa alipokea kutoka kwa shahidi wa tatu, zilikuwa ni kwa ajili ya kugharamia safari ambayo yeye ndio aliipanga kwa watalii 17 walioletwa na Mogasati,”alisema.

“Mahakama hii inaona hakuna sababu ya kutilia mashaka ushahidi wa shahidi huyo wa tatu. Hii ni kwa sababu  hata ushahidi wa shahidi wa 2 ambaye naye anafanya biashara ya utalii anamfahamu mshitakiwa kama mkurugenzi wa Expedition Africa Ltd”

Mbali na kumfahamu, lakini ofisi zao zilikuwa katika jengo moja la Kwa Kondo.

Hakimu alisema kampuni hiyo haikuwa na leseni ya kuendesha biashara ya utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, pia  kitendo cha mshitakiwa kumuomba shahidi wa pili atumie kampuni yake inathibitisha kuwa kampuni ya mshitakiwa haikuwa na leseni.

“Kulingana na ushahidi tunaona namna mshitakiwa alivyojitambulisha kama mmiliki wa kampuni ya Expedition Africa Limited ambayo inafanya biashara jijini Arusha na kwa mwavuli huo, ndio maana shahidi wa tatu alimwamini na kumpa fedha.

Hakimu alisema ni jambo lililo wazi kuwa mshitakiwa alipaswa kulipa ada za kuingia kwenye malango ya hifadhi za Manyara, Serengeti na Ngorongoro, lakini badala yake akaja na hadithi kwamba alishindwa kulipa kwa kuwa Serikali imefunga akaunti zake.

Alisema shahidi wa tatu aliieleza mahakama kuwa alitumia Dola 7,800 kulipa katika malango, lakini baada ya kupitia kielelezo P3 cha upande wa mashitaka anaona fedha ambazo shahidi huyo alizilipa kwenye malango ni Dola 3,974 na Sh229,920 tu.

Hakimu huyo alisema akaunti za mshitakiwa hazikuwa zimefungwa na Serikali kama mshitakiwa alivyomuongopea shahidi wa tatu, kwani ushahidi uliofanywa na SP Tenga ulibaini akaunti hiyo  haikuwa imefungwa na Serikali katika kipindi cha Desemba 2022.

Kulingana na ushahidi huo,  Desemba 16,2022 kiasi cha Dola 5,000 kilitolewa kwenye akaunti hiyo na Desemba 21, 2022 kiasi kingine Dola 400 kilitolewa kwenye akaunti na Hakimu akasema kama aliweza kutoa fedha hizo, kwa nini hakulipa ada za hifadhini.

Hakimu alisema upande wa mashitaka uliweza kuthibitisha mashitaka dhidi ya mkurugenzi huyo pasipo kuacha mashaka, hivyo anamhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kwanza, na kulipa faini ya Sh2 milioni kwa shitaka la pili.