Mwanamke jela maisha kwa kumbaka mvulana wa miaka 15

Muktasari:

  • Tukio lilitokea nyumbani kwa mwanamke huyo aliyekuwa akiuza keki na chapati  na ilidaiwa amekuwa na tabia ya kuwarubuni wavulana wadogo.

Mtwara. Mahakama ya Wilaya ya Mtwara imemhukumu kifungo cha maisha jela, Asha Ismail Chanchoni (47) kwa kosa la shambulio la aibu, baada ya kujihusisha kimapenzi na mvulana mwenye umri wa miaka 15.

Hukumu hiyo imetolewa Aprili 2, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Lucas Jang’andu aliyesema Mahakama imethibitisha bila kuacha shaka kuwa mwanamke huyo alikuwa akijihusisha kimapenzi na mvulana huyo.

Kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri, tukio hilo lilitokea Februari 2023 katika mtaa wa Chuno katika manispaa ya Mtwara Mikindani anakoishi mwanamke huyo.

Akichambua ushahidi, Hakimu Jang’wandu alisema siku ya tukio mshtakiwa alimbaka mtoto huyo kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kutoka kwa mashahidi mawili.

Mshtakiwa alikanusha shtaka hilo pamoja na maelezo ya mashahidi. Hata hivyo, mtoto huyo alikiri kushiriki kimapenzi na mwanamke huyo.

Hakimu baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, aliukataa utetezi wa mshtakiwa na kueleza upande wa mashtaka umethibitisha shitaka hilo pasipo kuacha mashaka na kwa viwango vinavyokubalika.

Baada ya kutiwa hatiani, Hakimu Jang’andu alisema kwa kuwa kosa hilo linaangukia katika kifungu 156(1) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha maisha.