Mwalimu jela maisha kwa kulawiti mwanafunzi

Mshtakiwa Livingston Kyarwenda ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi ya St Mathew ikiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga, baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumlawiti mwanafunzi. Picha na Hadija Jumanne.

Muktasari:

  • Hukumu hiyo ya kutumikia kifungo cha maisha jela Mwalimu Livingston Kyarwenda, imetolewa na Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga, baada ya kumkuta na hatia ya kumlawiti mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka tisa.


Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga, imemhukumu kifungo cha maisha jela, aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Mtakatifu Mathew iliyopo Kongowe, Livingston Kyarwenda (40), baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka tisa.

Kyarwenda, mkazi wa Mbagala Chamanzi anadaiwa kumlawiti mwanafunzi huyo wa kiume aliyekuwa anasoma darasa la nne katika vyoo vilivyopo shule hapo.

Uamuzi huo umetolewa leo, Novemba 29, 2023 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Herieth Mwailolo, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

“Kwa kuzingatia uzito wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapa na mashahidi watano ukiwemo ushahidi wa mtoto mwenyewe, mahakama hii imeridhika pasina kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa ulitenda kosa hilo kinyume cha sheria,” amesema Hakimu na kuongeza;

"Baada ya kukutia hatiani, mahakama hii inakuhukumu kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii na haki ya kukata rufaa iko wazi iwapo hujaridhika na hukumu hii."

Awali, Wakili wa Serikali Leon Kaikuye alidai kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu na upande wa mashtaka upo tayari kwa ajili ya uamuzi.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 308 ya mwaka 2023, Mwalimu huyo anadaiwa kumwingilia kinyume cha maumbile, mwanafunzi wake wa kiume mwenye umri wa miaka 9 kinyume cha kifungu cha 154 (1) (a) na (2) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code).