Jinsi ilivyokuwa siku moja kabla ya muungano, usiri watanda

Robo ya kwanza ya mwaka 1964 ilikuwa na matukio mengi kwa siasa za Tanganyika na Zanzibar kuliko wakati mwingine wowote. Haijulikani hasa ni nini kilichomsukuma Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, kushawishi kuziunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar.

Harakati zake za kuzifanya nchi za Afrika Mashariki kuwa shirikisho zilionekana kuanzia mwishoni mwa Machi na mwanzoni mwa Aprili, 1964.

Lakini mpaka kipindi hicho hakuwa na lile wazo la kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar.

Hata mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na maasi ya Tangayika, hakukuwa na wazo la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kilichokuwa kikizungumzwa katika kipindi chote cha wakati huo ni Shirikisho la Afrika Mashariki, ambalo baadaye halikufanikiwa, na wajumbe wa mkutano wa kuanzishwa shirikisho hilo waliokutana mjini Nairobi, Kenya, waliumaliza bila maelewano.

Mawazo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yalikuja wiki moja baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya kuanzishwa kwa Shirikisho hilo. Mkutano huo ulivunjika Jumamosi ya Aprili 11, 1964, mjini Nairobi.

Hadi wakati huo habari za shirikisho ndizo zilizokuwa zikizungumzwa, lakini hakukuwa na habari, uvumi wala fununu zozote za kuwako kwa kitu kinachoitwa Muungano, au ambacho kilitazamiwa kwamba baadaye kingekuja kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Lakini kama hivyo ndivyo hali ilivyokuwa, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliibukaje na hatimaye ukafanikiwa harakaharaka kuliko hata lile shirikisho lililokuwa limeandaliwa kwa kipindi kirefu?

Alhamisi, Aprili 16, 1964, Mwalimu Julius Nyerere aliingia katika ofisi za gazeti la chama cha TANU, The Nationalist and Freedom, alikoalikwa kwa ajili ya uzinduzi na kutazama maandalizi ya chapa ya kwanza ya gazeti hilo ambalo lingetoka kwa mara ya kwanza kabisa kesho yake, Aprili 17.

Alipoonyeshwa kielelezo cha gazeti hilo, alimwita msaidizi wake aliyeongozana naye, Rashidi Mfaume Kawawa na kumwonyesha kimojawapo cha vichwa vya habari vya gazeti hilo kilichosomeka hivi: ‘Maofisa wa Kenya Watetea Shirikisho la Kenya, Tanganyika na Uganda.’ Hivyo ndivyo lilivyoandika gazeti hilo lililotoka kwa mara ya kwanza Ijumaa ya Aprili 17, 1964.

Ukweli ni kwamba maofisa hao hawakutetea “Shirikisho la Kenya, Tanganyika na Uganda” kama lilivyoripoti gazeti hilo, vinginevyo mkutano wa kuanzishwa shirikisho hilo haungevunjika wajumbe wake walipokutana mjini Nairobi.

Angalau gazeti hilo linasema kilichokuwa kikizungumzwa hadi Aprili 17 ni Shirikisho la Afrika Mashariki, na wala si Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Zikiwa ni siku tisa tu zilizokuwa zimebakia hadi kufika siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, gazeti hilo halikuzungumza habari yoyote ya Tanganyika kuungana na Zanzibar, na wala Shirika la Utangazaji la Tanganyika (TBC—Tanganyika Broadcasting Corporation) halikutangaza habari zozote kuhusu kile ambacho hatimaye kilikuja kujulikana sana kama Muungano wa Tanzania.

Inaelekea waandishi wa vyombo hivyo hawakujua lolote kuhusu kuungana huko. Na kama walijua, basi walifanya siri kwa masilahi fulani.

Lakini kama ni siri, ilikuwa ya nini na kwa masilahi gani? Ilivyo ni kwamba hadi tarehe hiyo, Aprili 17, Nyerere hakuwa amepata wazo la kile kinachoitwa leo kama Muungano wa Tanzania (Tanganyika-Zanzibar).

Au kama alikuwa nalo tayari, hakulitilia maanani na wala hakuona kama lingewezekana. Pengine alilipata kesho yake au aliletewa. Pengine lilimjia katika ndoto, lakini akaitilia mashaka ndoto hiyo.

Vinginevyo ingejulikana kwa vyombo vya habari, hususan kwa gazeti kama The Nationalist and Freedom alilokwenda kulizindua.

Hata Nyerere mwenyewe, pamoja na kutembelea ofisi za gazeti hilo na kuzungumza na waandishi wake, hakuwaambia mambo ya Muungano.

Hata kwa kuwagusia tu. Aliridhishwa tu na habari kuu ya gazeti hilo iliyozungumzia Shirikisho la Kenya, Uganda na Tanganyika, na wala si Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akitabasamu, Nyerere alimgeukia Kawawa na kumwambia, “Hili (The Nationalist) litakuwa kinara katika jitihada za Umoja wa Afrika.” Kawawa naye akatabasamu. Wakatabasamu pamoja.

Jioni ya siku hiyo, waziri mdogo wa mambo ya ndani wa Tanganyika, Roland Mwanjisi akatumwa kwenda Kenya kueneza habari za gazeti hilo, na wala si kueneza habari za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa hiyo hadi wakati huo hakukuwa na wazo wala habari zozote kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Hata wazo lilipopatikana hatimaye, mazungumzo kuhusu Muungano wenyewe yalifanyika kwa siri kubwa. Hata viongozi wengine serikalini hawakujua kilichokuwa kinaendelea.

Jumatano ya Aprili 22, 1964, Mwalimu Nyerere alizuru Zanzibar kwa kile kilichoitwa “…ziara ya kirafiki katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuonana na Rais Abeid Aman Karume.”

Hii ilikuwa ni ziara yake ya kwanza Visiwani humo tangu Serikali ya Mapinduzi ilipotwaa madaraka Januari 12, 1964.

Ziara yake ya mwisho ilikuwa ni miaka minane iliyokuwa imepita, alipokwenda huko kuhudhuria sherehe za kuzaliwa kwa ASP kutokana na muungano wa Shirazi Association na African Association uliofanyika Februari 5, 1957.

Saa 6:40 mchana wa Jumatano ya Aprili 22 siku nne kabla ya kufanyika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanziba, Nyerere aliwasili uwanja wa ndege wa Unguja kwa ndege ya Tanganyika akiongozana na Waziri mdogo katika Ofisi ya Rais, Bhoke Munanka.

Nyerere alilakiwa na mwenyeji wake, Rais wa Zanzibar, Sheikh Karume; Makamu wa Rais wa Zanzibar, Sheikh Kassim Hanga; Waziri wa Fedha, Abdul Aziz Twala; Katibu wa Bunge na Baraza la Mapinduzi; Salim Rashid, pamoja na wanachama wengine wa SMZ.

Watanganyika waliotangulia Zanzibar mapema asubuhi ya siku hiyo ili kumpokea Nyerere uwanja wa ndege ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ulinzi, Oscar Kambona na Waziri wa Mambo ya Ndani, Job Lusinde.

Taarifa hiyo ilichapishwa pia na jarida Africa Confidential la Jumamosi, Mei 9, 1964.

Baada ya kulakiwa, Karume na Nyerere waliongozana katika msafara hadi Ikulu ya Zanzibar, ambako ni Nyerere na Karume tu walioingia ndani ya chumba kimojawapo katika Ikulu hiyo kuzungumza, wakiwaacha mawaziri wao nje wakiwa kwenye veranda.

Mazungumzo yao ya ‘siri kubwa’ yalidumu kwa muda wa nusu saa (dakika 30) tu.

Walionekana wamefurahi walipotoka katika chumba walimokuwa wamejifungia. Jioni ya siku hiyo, tangazo la kuziunganisha nchi lilitolewa jijini Dar es Salaam.

Wabunge wa Bunge la Tanganyika wakaitwa kwenye kikao cha dharura kilichoitishwa na Mwalimu Nyerere.

Je, waliambiwa nini kwenye kikao hicho? Soma toleo lijalo.