Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinsi mitandao ya kijamii ilivyobadili maisha

Muktasari:

  • Hata hivyo, teknolojia hiyo kwa upande wa mitandao ya kijamii imehamisha maisha yaliyozoeleka na kuyapeleka kwenye simu za mkononi. Mitandao ya kijamii inayotumiwa zaidi nchini ni Twitter, Instagram, Whatsapp na Facebook.

Dar es Salaam. Hivi maisha yangekuwaje kama mitandao ya kijamii isingekuwepo katika miaka ya karibuni? Teknolojia imeleta mapinduzi makubwa duniani. Imeleta raha, imerahisisha mambo na kuinua uchumi, imesogeza mawasiliano karibu na kupunguza muda uliotumika zamani kuwasiliana kwa barua au kusafiri.

Hata hivyo, teknolojia hiyo kwa upande wa mitandao ya kijamii imehamisha maisha yaliyozoeleka na kuyapeleka kwenye simu za mkononi. Mitandao ya kijamii inayotumiwa zaidi nchini ni Twitter, Instagram, Whatsapp na Facebook.

Takwimu za mwaka 2017 zinaonyesha idadi ya watumiaji wa mitandao hapa nchini ilifikia watu milioni 23.

Maisha yalivyobadilika

Kwa mfano, hapo zamani ilikuwa ni kawaida kwa wanafamilia kukaa pamoja, kuzungumza au kujadili jambo kwa usikivu huku kila mmoja akizingatia kinachozungumzwa, lakini siku hizi ni kawaida kuona baadhi yao wako vikaoni wakichati kwa simu zao.

Si hivyo tu, miaka kumi iliyopita ilikuwa ni kawaida marafiki wakutanapo, kila mmoja anazingatia mada inayozungumzwa, lakini si ajabu siku hizi wakakutana na kila mtu akawa ametingwa na mada zinazoendelea mitandaoni kupitia simu yake. Kasi ya matumizi ya mitandao inaongezeka katika kila nyanja kiasi cha kuwatenga wanajamii hata wanapokuwa pamoja kushindwa kuzungumza wakielekeza akili kwenye simu zao.

Katika ngazi ya familia, athari za teknolojia hii zinaonekana wazi. Kwa mfano, ni kawaida kuwakuta baba, mama na mtoto au watoto wameketi sebuleni, lakini kila mmoja ameinamia simu akifanya kimfaacho. Hali ipo hivyo hata kwenye sherehe au sehemu za starehe.

Si ajabu mkakubaliana mkutane mahali lakini mkifika kila mmoja anahamishia mawazo kwenye simu yake. Misibani nako siku hizi mambo ni hayo, kwani si ajabu kuwakuta watu wakiomboleza, lakini kila mmoja ameinama akichati mitandaoni kwa kutumia simu yake.

Licha ya mambo hayo, matumizi ya mitandao yamerahisisha mawasiliano kati ya mtu na mtu ambayo zamani yalihitaji kutumiana barua au kusafiri ili kuonana.

Vilevile yamerahisisha mawasiliano ya kikazi na kibiashara, huku watumiaji wengine wakinufaika kwa kutumia mitandao kupata elimu.

Kwa wengine, simu ni nyenzo ya kuonyesha maisha yao kupitia mitando ya kijamii. Siku hizi kuweka picha ya chumba mtu anacholala, chakula, mavazi, nyumba, magari na utajiri ni jambo la kawaida.

Wananchi wanasemaje?

Mkazi wa Dodoma, Geofrey James anasema maisha ya kawaida yamehamia kwenye mitandao ya kijamii kupitia simu za mikononi na kuwafanya watu kusahau wajibu na utu.

“Inawezekanaje mtu yuko msibani, halafu badala ya kuomboleza anachukua picha za wafiwa na za marehemu na kuzisambaza? Hili halikubaliki na siyo utu,” anasema.

Naima Mabrook anasema zamani mtu akifiwa alikaa ndani na kulia, lakini siku hizi anakuwa wa kwanza kuchapisha picha ya mtu aliyefariki duni na kuutangaza msiba kupitia mitandao, hivyo kuwahisha taarifa kwa ndugu na jamaa zake.

“Teknolojia hii pia imechangia kupunguza utu kwani wapo wanaojali kupata picha za awali za ajali kuliko kuwasaidia majeruhi wanaotapatapa wakiomba msaada baada ya ajali kutokea,” anasema Naima.

Akizungumza na gazeti hili, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa anasema licha ya kuwa mtumiaji mzuri wa simu na mitandao ya kijamii, lakini hajaruhusu teknolojia hiyo imtawale.

“Sijaifanya simu (kuwa) ni kila kitu kwangu, nimezuia haijanitawala. Kuna muda naweza nisiitumie na maisha yanaendelea, ila ukweli ni kwamba kwa maendeleo ya sasa inasaidia kwa kiasi kikubwa,” anasema Msigwa. “Kwetu wanasiasa inawezekana ukapata kitu cha kuupasha umma, teknolojia inasaidia kufanya hivyo ndani ya muda mfupi, hata kama kuna kitu unaona hakiko sawa naweza kuandika kwenye ukurasa wangu watu wengi wakasoma.”

Getrude Celestine, mkazi wa Msasani anaeleza kuwa hawezi kuishi bila simu hata kwa saa moja, labda awe na tatizo kubwa. “Kwa kweli haiwezi kupita saa moja au nusu saa sijaigusa simu, nikifanya hivyo nitapitwa na mengi kwa kuwa ni mfuatiliaji sana wa Twitter na Instagram, sasa huko dakika 10 ni nyingi sana unaweza kukuta mengi yamekupita,” anasema.

Ushauri wa mtaalamu

Mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia, Modesta Kimonga anasema matumizi ya mitandao ya jamii yana athari kubwa katika saikolojia ya binadamu na ni muhimu mazungumzo yakahusisha watu kukutana ana kwa ana.

Anasema kisaikolojia binadamu anategemea uwepo wa binadamu mwenzake ili aweze kuishi na hiyo inatokana na mchangamano ambao huanzishwa na mazungumzo. “Kuna wakati mtu anataka akuelezee hisia zake, lakini wewe uko ‘busy’ na simu, hii ni hatari,” anasema.

Anaongeza kuwa, “kuna mwanasaikolojia mmoja aliwahi kuandika kuwa kama teknolojia hii itatutawala kupita kiasi upo uwezekano wa binadamu kuwa kama wanyama. Wanyama hawazungumzi, kila mmoja ana mambo yake.”

Anasema simu na mitandao ya kijamii vimekuwa vyanzo vikubwa vya migogoro katika mahusiano na wakati mwingine inapunguza ufanisi katika utendaji kazi.