Jinsi ziara za marais 15 zilivyoinufaisha Tanzania

Muktasari:

  • Tangu Novemba 5, 2015 alipoapishwa, tayari wakuu wa nchi 15 wameshakuja nchini wakiwa na mikakati mbalimbali kwa ajili ya nchi zao, huku Serikali ikiitumia kunufaisha ujenzi wa uchumi wa Tanzania.

Rais John Magufuli ana staili yake ya utendaji; hasafiri nje kutafuta fursa za kiuchumi, lakini zinamfuata.

Tangu Novemba 5, 2015 alipoapishwa, tayari wakuu wa nchi 15 wameshakuja nchini wakiwa na mikakati mbalimbali kwa ajili ya nchi zao, huku Serikali ikiitumia kunufaisha ujenzi wa uchumi wa Tanzania.

Ziara hizo zitasaidia kuboresha kuanzia ujenzi wa miundombinu ya usafiri, viwanda, elimu, afya, kilimo, mawasiliano, utalii, utamaduni na zaidi ya yote ushirikiano huo kuzaa miradi itakayoongeza ajira, kwa mujibu wa makubaliano baina ya viongozi wa nchi hizo na Tanzania.

Wakuu hao ni pamoja na marais 12, mfalme mmoja na mawaziri wakuu wawili, ambao mfumo wa utawala wa nchi zao unawafanya kuwa wakuu wa nchi.

Tofauti na mtangulizi wake, mpaka sasa Rais Magufuli amefanya ziara nje zisizozidi tano na hajatoka nje ya ukanda wa Afrika Mashariki; amezuru Rwanda, Uganda na Kenya.

Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi amekuwa kiongozi wa 15 wa nchi baada ya marais wa Rwanda, Uganda, Vietnam, Zambia, Malawi, Chad, Uturuki, Afrika Kusini, Sudan Kusini, mfalme wa Morocco na mawaziri wakuu wa India na Ethiopia walioanza kumiminika tangu mwaka 2016.

Rais el-Sisi, aliyekuja nchini Jumatatu, na Rais Magufuli wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya kiuchumi na kijamii na taifa hilo la Kiarabu litajenga kiwanda cha nyama hapa nchini kwa ajili ya kusafirisha kwenda Misri na nchi nyingine za nje.

Misri pia imekubali kuisaidia sekta ya afya kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), teknolojia ya umwagiliaji, kubadilishana walimu katika programu mbalimbali na hivyo Tanzania itaweza kutuma walimu wa Kiswahili vyuo vikuu vya Misri na nchi hiyo kutoa wataalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Kufungua neema

Aliyekuwa wa kwanza kuzuru nchini ni rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye alikuja Februari, 2016 akiwa na mradi wa bomba la mafuta ghafi linalojengwa kutoka Hoima hadi Tanga.

Ujenzi huo utakaogharimu Sh8 trilioni, unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja zipatazo 10,000 na vibarua 30,000 na sherehe za uzinduzi wa ujenzi zilifanyika mwezi huu mjini Tanga.

Rais Museveni pia alitembelea viwanda vya kampuni ya Said Salim Bakhresa na Bandari ya Dar es Salaam katika ziara yake ya kwanza kabla ya kufanya ziara nyingine ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa bomba hilo mkoani Tanga mwezi huu.

Museveni alifuatiwa na jirani yake, Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye amekuwa akionekana kutaka kunufaika na Bandari ya Dar es Salaam kutokana na nchi yake kutopakana na bahari.

Katika ziara yake ya Novemba, 2016, Rais Magufuli na Kagame walikubaliana Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zifungue ofisi katika nchi ya Rwanda ili kurahisisha uhakiki wa bidhaa kwa wafanyabiashara wa Rwanda wanaoingia nchini.

Pia, Serikali ya Tanzania ilitoa eneo la bandari kavu (ICD) kwa ajili ya kuhifadhia bidhaa kutoka Rwanda ili kupunguza urasimu ambao umekuwa kikwazo kwa maendeleo ya biashara.

Wakuu hao walikubaliana kupunguza vituo vya ukaguzi barabarani kutoka Tanzania kwenda Rwanda kufikia vitatu na kukubaliana kuanzisha kituo kimoja cha kukusanya mapato badala ya kila sehemu kuwa na mfumo wake ambao unapoteza mapato mengi kwa kuwa mifumo hiyo haina udhibiti mmoja.

Pia, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Tanzania na Rwanda walitiliana saini muhtasari wa Tume ya Ushirikiano wa pamoja baina ya nchi hizo mbili na kukubaliana ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) kutokea Dar es Salaam hadi Kigali.

Miundombinu ya maji

Wakati marais hao wawili walijikita katika usafirishaji, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliyezuru nchini Julai 2016, aliahidi kutoa msaada wa dola 500 milioni za Kimarekani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

Aliahidi kuendelea kufadhili ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 178 na kutoa dola 92 milioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kisiwani Zanzibar.

Pia, walikubaliana kushirikiana katika sekta za kilimo, viwanda, afya, nishati, madini na viwanda vidogo.

Pia, India ilikubali kuleta wawekezaji katika uzalishaji wa dawa za binadamu na vifaa tiba na kuipa Hospitali ya Bugando mashine maalumu kwa ajili ya kupima ugonjwa wa saratani na katika sekta ya nishati na madini.

Mikataba 21 na Morocco

Ziara nyingine ilikuwa ya Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco, ambaye nchi yake ilisaini mikataba 21 ya ushirikiano katika nyanja tofauti, huku akiahidi kujenga uwanja wa kisasa wa michezo mkoani Dodoma.

Mfalme huyo, ambaye pia alikuwa akitafuta ushawishi wake Morocco irejeshewe uanachama wa Umoja wa Afrika (AU), alitembelea Zanzibar na Hifadhi ya Ngorongoro.

Mikataba hiyo 21 itashuhudia Tanzania na Morocco zikiimarisha uhusiano katika siasa, sekta ya uvuvi, viwanda, madini, mbolea, masuala ya bima, uwekezaji, reli, biashara, elimu na afya, huku zikikubaliana kubadilishana wataalamu na kuwezeshana kufikia malengo endelevu.

Ushawishi wa kisiasa

Ziara nyingine inayoonekana kulenga kujenga ushawishi wa kisiasa ni ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki aliyezuru nchini Januari mwaka huu akiwa na ujumbe wa watu 150 wakiwamo mawaziri, wabunge, maofisa wa serikali na wafanyabiashara.

Erdogan, ambaye alinusurika kupinduliwa mwaka 2016, alionekana kushawishi wapinzani wake, ambao anawaita magaidi, washughulikiwe katika nchi marafiki, lakini suala hilo halikutolewa msimamo.

Hata hivyo, ziara hiyo ilifanikisha kampuni ya Kituruki kushinda zabuni ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na pia nchi hizo kusaini mikataba ya ushirikiano katika maeneo tofauti.

Wengine waliotembelea nchini katika kipindi hicho ni Rais wa Jamhuri ya Chad, Idriss Deby Itno aliyekuja nchini Novemba 2016, Edgar Lungu wa Zambia, Jacob Zuma wa Afrika Kusini.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, Truong Tan Sang wa Vietnam na Salva Kiir wa Sudan Kusini.

Ni jambo bora kutembelewa

Wakizungumzia ziara za wakuu hao 15 wa nchi katika kipindi kisichozidi miaka miwili, wadau waliohojiwa na Mwananchi walikuwa na maoni tofauti.

“Ni jambo la kawaida (kutembelewa na marais tofauti), lakini ziara hizo zitakuwa na maana kiuchumi iwapo viongozi hao wanatoka kwenye nchi zilizoendelea,” alisema Profesa Mohamed Bakari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Wako marais ambao wanakuja na wawekezaji, wanaingia mikataba ya kujenga viwanda, wako wenye kusaidia sekta za kilimo. Ni jambo bora kutembelewa na watu wa aina hiyo.”

Alitoa mfano wa Rais wa Misri ambaye alisema pamoja na sehemu kubwa ya nchi hiyo kuwa jangwa, imebobea kwenye kilimokutokana na kutumia maji ya mto Nile kwa umwagiliaji.

“Wenzetu watakuwa wanaishangaa Tanzania kuwa pamoja na ardhi kubwa yenye rutuba na mito mingi, huwa inakabiliwa na njaa,” alisema.

Alisema viongozi wa aina hiyo wanapokuja, Tanzania itafaidika kwa kujifunza kutoka kwao.

Hata hivyo, pamoja na Serikali kudhibiti safari ili kubana matumizi yasiyo ya lazima, alisema kuna haja ya Rais Magufuli kutembelea nchi mbalimbali ili kujifunza kwa wengine.

“Ni jambo jema kupunguza safari za Rais ili kupunguza matumizi, lakini tufahamu kuwa asipokwenda kabisa nje kuna mambo ya kujifunza tunayakosa,” alisema.

Profesa wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema marais wanapofanya ziara, kunakuwa na pande mbili zinazofaidika.

Hata hivyo, alisema idadi ya marais 15 waliotembelea Tanzania katika kipindi cha miaka miwili ni wengi.

“Hakuna Rais anayefanya biashara ya hasara ni lazima kuwe na kutegemeana, mgeni atafaidika na mwenyeji atafaidika, hivyo siyo sisi tu tunaofaidika na ziara hata wageni wanafaidika,” alisema.

Alisema wafanyabiashara wanapokuja nchini kuwekeza, wanatarajia kupata faida kwa maendeleo ya nchi zao.

“Lakini sisi pia tutapata kodi kwa uwekezaji unaofanywa na watu wetu watapata ajira kwa hiyo pande zote zinafaidika,” alisema.

Alisema katika kipindi hiki, huwezi kujitenga na dunia kwani wote tunaishi kwa kutegemeana.

Nyongeza na Raymond Kaminyoge