JKT waanza safari matumizi nishati safi ya kupikia

Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Hassan Mabena akiangalia majiko ya gesi yaliyofungwa katika kikosi cha Jeshi cha  Mtabila kilichopo Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma.

Muktasari:

  • Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeweka mkakati wa kuondokana na matumizi ya kuni kwenye vikosi vyake, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali linalolenga kulinda mazingira.

Kigoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), limeianza rasmi safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa kufanya tathmini ya miundombinu ya majiko ya vikosi vyake ili kuyabadilishia matumizi kutoka kuni kwenda kwenye nishati safi.

Aprili 12, mwaka jana Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Seleiman Jafo alitangaza kuwa mwisho wa matumizi ya kuni kwa kupikia kwa taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 200 ni Januari, 2025.

Mkuu wa Tawi la Utawala JKT na Mwenyekiti wa Kamati ya Kimkakati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema hayo leo Mei 5, 2024 mara baada ya kuzindua jiko la gesi katika Kikosi 825 KJ Mtabila, wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma.

Amesema katika kutekeleza hilo, JKT iliunda timu iliyoshirikisha Rea ambayo ilifanya tathmini ya kina ya miundombinu ya majiko, katika makambi yote ya jeshi hilo.

“Tumefanya tathmini ya kina kwa kupita kwenye vikosi vyote kuangalia miundombinu ya majiko, ili kuona kama yatafaa kwa ajili ya nishati ambayo wenzetu wa Rea watakuja kuweka katika makambi yetu,” amesema Brigedia Jenerali Mabena.

Amesema kutokana tathmini hiyo, kwa sasa vikosi vinaendelea kutengeneza miundombinu ya majiko kwa ajili ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Vikosi vyote vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa agizo hilo ikiwa ni kuandaa majiko haya, lakini pia kusimika hiyo mitungi ya gesi mikubwa na wakati huo, tuusubiri ule mpango na wenzetu wa Rea ambao sasa utakuja kuboresha zaidi nishati hii safi ya kupikia,” amesema.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mazingira yanakuwa salama nyakati zote.

Amesema kwa mwaka mmoja vikosi vya JKT vinahudumia wastani wa vijana 100,000  wa kundi la mujibu wa sheria hivyo ambao wanapata milo yote vikosini humo, hivyo  ili kulinda mazingira ni lazima kutumia nishati safi ya kupikia.

Akizungumzia kuhusu kukamilika kwa mradi wa nishati safi ya kupikia, Kamanda Kikosi 825 KJ, Mtabila Luteni Kanali Patrick Ndwenya amesema mradi huo umetekelezwa kwa kutumiwa fedha za ndani.

“Tutatumia mradi huu kama shamba darasa kwa vijana wanaopata mafunzo JKT, juu ya namna ya kulinda mazingira,”amesema.

Pia amesema katika kulinda mazingira, kikosi imepanda miti 13,000 ikiwemo 1,000 ya matunda.