Ufadhili, ushirikiano kufanikisha nishati safi kwa wote

Muktasari:

Wadau wamesema ili kuwa na jamii kubwa inayotumia nishati safi ya kupikia, wabia wa maendeleo hawana budi kutoa ufadhili wa kifedha kwa makundi yanayolengwa.

Dar es Salaam. Wadau wamesema ili kuwa na jamii kubwa inayotumia nishati safi ya kupikia, wabia wa maendeleo hawana budi kutoa ufadhili wa kifedha kwa makundi yanayolengwa.

Matumizi ya nishati chafu ya kupikia (kuni na mkaa) yanatajwa kuwa na madhara mengi ya kimazingira na kiafya, takwimu za Wizara ya Afya za mwaka 2017, zinaonyesha watu 22,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya nishati hiyo.

Kutokana na hali hiyo na msukumo wa kujali mazingira,  Serikali imekuwa ikihamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa mitungi ya gesi kwa makundi mbalimbali, kubwa zaidi ni kuanzishwa Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Wanawake Afrika (AWCCSP) uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo, licha ya juhudi hizo za Serikali Mratibu wa miradi ya Equity Group Foundation, Neema Massawe amesema ili kufanikisha jambo hilo wadau wote wanapaswa kushirikiana, hususani katika kuhakikisha walengwa wanakuwa na uwezo wa kuwa na kutumia nishati hiyo.

“Mathalani wabia wa maendeleo wanapaswa kuweka fungu maalumu katika benki ambalo litatumika kama dhamana kwa mtu mmoja-mmoja na makundi ya watu ambao wanahitaji mikopo ya kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi,” amesema Massawe wakati wa mjadala kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ulioandaliwa na Chemba ya Biashara ya Marekani (AmchamTZ), Machi 20, 2024.

Katika mjadala huo wa AmchamTZ ulioandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Massawe amesema pamoja na juhudi za kuwafanya wananchi kumudu kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, elimu inapaswa kuendelea kutolewa zaidi hususani kwa wanawake ili matumizi hayo yawe endelevu.

Massawe aliungwa mkono na Mkuu wa Programu za Shuleni wa WFP, Vera Kwara aliyesema: “Kutokana na changamoto za kifedha shule nyingi hazitumii nishati safi ya kupikia, hivyo kuna haja kwa wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuangalia namna ya kusaidia upatikanaji wa miundombinu ya nishati safi.”

Kwara amesema shule ni miongoni mwa maeneo muhimu ambayo yanapaswa kupewa msukumo mkubwa kwani zilizo nyingi zinatumia kuni na mkaa kama chanzo cha nishati ya kupikia.

Mwenyekiti wa wadau wa nishati safi nchini, Finias Magessa amesema ni vigumu kuwa na matumizi ya nishati safi kwa asilimia 100 lakini hamasa inapaswa walau kuwa na matumizi ya nishati ambazo ni nafuu kwa usafi ikilinganishwa na zinazotumiwa sasa na wengi.

“Serikali inapaswa kuwa na miundombinu ya nishati safi ambayo wadau wa maendeleo na sekta binafsi watawekeza. Kukiwa na ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali ndani ya miaka 10 ijayo matumizi ya nishati ya kupikia yatakuwa yamesambaa nchi nzima,” amesema Muro.

Mtaalamu mwandamizi wa fedha wa programu ya CoockFund, inayosimamiwa na Shirika la UNCDF, Imanuel Muro amesema suala la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia linahitaji ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi.