Jowuta yaanza kuwashughulikia wamiliki wa vyombo vya habari wanaodaiwa
Muktasari:
Chama hicho kinafuatilia maslahi ya wafanyakazi 195 wa Sahara Media Group (SMG) ambao wengi ni wanahabari na baadhi ni wanachama wa Jowuta wakidai malimbikizo ya mishahara yao zaidi ya Sh 3.5 bilioni.
Mwanza. Chama cha wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini (Jowuta) kimewataka wamiliki na waajiri kuzingatia sheria za ajira na kazi kwa kuhakikisha maslahi ya waandishi wa habari yanatimizwa kwa kuwalipa stahiki zao kwa wakati na kuwawekea mazingira salama ya kazi.
Akizungumza leo Alhamisi Aprili 6, 2023 jijini Mwanza, Mwenyekiti wa chama hicho, Mussa Juma amesema chama hicho tayari kimeanza kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ikiwemo Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) wamiliki wote wanaodaiwa na waandishi wa habari.
Amesema chama hicho kimepeleka shauri la madai ya Sh3.5 bilioni ya wafanyakazi 195 wa Sahara Media wanaodai malimbikizo ya mishahara kwa muda mrefu.
kuhusu maslahi ya wanahabari nchini, amewatahadharisha wamiliki wa vyombo vya habari na waajiri kuwa hatua hiyo haitaishia kwenye taasisi hiyo kwani watafika kote kwa sababu vyombo vingi vya binafsi wafanyakazi wanapitia changamoto nyingi ikiwamo kufanya kazi bila mikataba.
Amesema Jowuta kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na idara ya kazi mkoa wa Mwanza watapeleka shauri hilo kwenye vyombo vya sheria, huku takwimu za idara ya kazi zikionyesha kuwa hadi kufikia Mei, 2021 jumla ya wafanyakazi 152 wanaodai Sh 2.6 bilioni mashauri yao yaliwasilishwa.
“Tunaomba wafanyakazi wa Sahara waendelee kuwa watulivu na wasichukue hatua za kufanya mgomo suala lao tunalifanyia kazi tunaamini haki zao zitapatikana tayari kamishna wa kazi ameshapeleka maombi ya mmiliki kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ndani ya muda mfupi suala hili litabaki kuwa historia,”
“Tunawasihi waandishi wa habari waepuke kufanya kazi katika vyombo vya habari bila mikataba na waajiri, watambue haki zao na ukiona mwajiri hajakulipa miezi miwili mfululizo una haki ya kufungua madai ofisi ya idara ya kazi ili kuepusha malimbikizo ya madeni,”amesema Juma
Mjumbe wa Bodi ya Jowuta Taifa, Mutta Robert amesema bodi ya chama hicho imekubaliana kuanza na madai ya wafanyakazi wa Sahara Media na wamechukua maamuzi kulifikisha kwenye tume ya usuluhishi wakiamini haki itatendeka kwani changamoto zinazowakabili waandishi wa habari nchini zinapaswa kuisha ambapo wengi wanahangaika wanapopata matatizo ya magonjwa na kifo.
Naye, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko amewashauri waandishi kujiunga na chama hicho ili kiwasaidie kutetea maslahi yao, kujitambua katika maeneo yao ya kazi huku wamiliki wakitakiwa kuzingatia sheria za kazi na ajira ili waajiriwa hao wafanye kazi kwa weledi akidai wanastahili kazi na huduma kama ilivyo kwa sekta nyingine.