JPM amfagilia Dk Ramadhan Dau
Muktasari:
Dk Magufuli alisema Balozi Dau alimfuata ofisini kwake(wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi), akiwa mnyonge na mwenye kukata tamaa ya kufanikisha mradi huo.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa NSSF, Dk Ramadhan Dau ni miongoni mwa watu wenye mchango mkubwa katika ujenzi wa Daraja la Kigamboni.
Dk Magufuli alisema hayo jana mara baada ya kukaribishwa kutoa hotuba ya ufunguzi wa daraja hilo uliofanyika Kigamboni, Dar es Salaam ambako kabla ya kuzungumza, alimwita Dk Dau na kumtambulisha kwa wananchi waliohudhuria sherehe hizo: “Naomba niwatambulishe mtu mmoja mwenye mchango mkubwa katika ujenzi wa daraja hili. Watanzania hawapendi kukumbuka historia, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Dk Dau na NSSF wamefanya kazi kubwa sana,” alisema Rais Magufuli na kushangiliwa na watu wengi.
Dk Magufuli alisema Balozi Dau alimfuata ofisini kwake(wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi), akiwa mnyonge na mwenye kukata tamaa ya kufanikisha mradi huo. “Ndiyo nikamwambia aanze kufanya kazi.” Rais Magufuli alisema ni Dk Dau na NSSF ndiyo waliosimamia na kuhakikisha daraja hilo linajengwa na kukamilika kwa kiwango hicho, akasema haitakuwa busara kulizindua bila kutambua mchango wake. Alisema ni kawaida kwa watu wenye michango mikubwa kusahaulika wakati wa mafanikio.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Dau alizitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa NSSF katika uwekezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.
Aliwakumbusha Watanzania kumtanguliza Mungu akisema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia kukuza uchumi na kurahisisha usafirishaji kwa wakazi wa Kigamboni na Tanzania kwa ujumla. Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisema daraja hilo ni la kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kwamba litasaidia kukuza uchumi, utalii na ndiyo maana hata majirani wanalitamani.
“Daraja hili linabeba zaidi ya tani elfu moja, ni daraja la kipekee, linao uwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka 100,” alisema .
Alisema katika ujenzi wake uliofanyika kwa utaratibu wa PPP (Public Private Partnership), Serikali imetoa asilimia 40 na NSSF asilimia 60 hivyo vyombo vya usafiri kama baiskeli, guta, pikipiki na magari yatalipa kuvuka.
“Leo hii, daraja hili limekamilika... halitambagua mtu kwa sababu wa CCM watapita hapa wa Chadema watapita hapa na bahati nzuri mstahiki meya wa jiji hili ambaye ni Chadema naye yuko hapa na amepita katika daraja hili… lakini wananchi waenda kwa miguu hawatalipia matumizi ya daraja… ila wale waendesha baiskeli, pikipiki, maguta na magari lazima walipie,” alisema Dk Magufuli. Rais aliipongeza kampuni ya China Railway Construction Engineering Group iliyotekeleza mradi huo kwa kushirikiana na kampuni ya China Railway Major Bridge Group.
“Kwa kazi nzuri iliyofanywa na wenzetu hawa kutoka nchini China napenda kutumia fursa hii kuahidi kwa niaba ya Serikali kuwa tutaendeleza ushirikiano wetu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo kumalizia kipande cha barabara kinachounganisha daraja hili kutoka upande wa Kigamboni,’’ alisema.