Jukwaa la Wahariri Tanzania lamlilia Ubwani

Muktasari:

  • TEF, limetuma salamu za rambirambi baada ya kutokea kifo cha Mwandishi wa habari mkongwe nchini, Zephania Ubwani kilichotokea Aprili 6, 2024 wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi.

Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEf), limetuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Mwandishi wa habari mkwonge nchini, Zephania Ubwani (70) kilichotokea Aprili 6, 2024 wakati akitekeleza majukumu yake.

 Ubwani aliyekuwa akiandikia Gazeti la The Citizen linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jijini Arusha, alifariki dunia baada ya kuugua ghafla wakati akiwa katika majukumu ya kikazi katika Hoteli ya Kibo Pallace jijini humo.

Kupitia taarifa iliyotolewa hii leo Jumatatu Aprili 6, 2024 na Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deodatus Balile, TEF imeeleza kupokea kwa masikitiko habari za kifo cha Ubwani ambaye uchunguzi wa daktari umeeleza alikuwa na tatizo la moyo kwa muda mrefu, hivyo alipatwa na shambulio la moyo.

“Jukwaa la Wahariri Tanzania tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, Chama cha Wanahabari Arusha na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kutokana na msiba huo. Mungu ailaze mahala pema peponi roho ya marehemu,” imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, taarifa za awali zinaeleza Ubwani alianza kupata tatizo la afya wakati akifanya mahojiano na Mkurugenzi wa Costech katika Hoteli ya Kibo Palace. Alijisikia vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya AICC ambapo alifariki dunia wakati akifanyiwa uchunguzi

Awali, uongozi wa MCL ulitangaza Jumamosi kuwa Ubwani, ambaye pia aliwahi kuchangia hadithi katika magazeti ya The East African and Daily Nation of Kenya pamoja na Daily Monitor ya Uganda, atakumbukwa kwa umahiri wake wa kuandika habari kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika uandishi wake, Ubwani aliandika kwa kina kuhusu utalii, biashara, uchumi na madini, huku moja ya andiko lake likichapishwa The Citizen siku moja kabla ya kifo chake.

"Tunatoa pole kwa familia ya Ubwani na wanahabari wote wa Arusha. Tunaahidi kushirikiana nao katika kila hatua ya mazishi... Roho yake ipumzike kwa amani," ilisema taarifa ya MCL.

Ubwani alianza taaluma yake ya uandishi wa habari gazeti la Daily News linalomilikiwa na Serikali, lakini baadaye akahamia kampuni ya MCL.

Ubwani alizaliwa Septemba 12, 1953 na ameacha mjane na watoto wanne. Kwa sasa taratibu za maziko zinafanyika katika msiba uliopo Kimandolu jijini Arusha.