Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kabudi ataka kuwepo fidia waathirika ukatili wa kijinsia

Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa,Prof. Palamagamba Kabudi akitoka katika kikao cha Tume ya Haki Jinai jijini Dar es Salaam leo, baada ya kumaliza kutoa maoni yake katika kikao cha tume hiyo. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Kubudi asisitiza uwepo wa fidia kwa waathirika wa vitendo vya ubakaji, ukatili wa kijinsia au kudhalilishwa, asema sio sawa kuegemea kwa watu wanaotenda vitendo hivyo.

Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ni wakati muafaka kuwepo na mfumo wa fidia kwa waathirika kwa vitendo vya uhalifu, kudhalilishwa au vitendo vya ukatili wa kijinsia badala ya kukazana na wahusika wanaotekeleza vitendo.

"Tumekazana na wanaotenda vitendo hivi ikiwemo kuwapa adhabu, lakini suala la fidia au utaratibu wa kuwarejesha waathirika wa vitendo hakuna. Mfano mwathirika wa kubakwa, mtu kufungwa sawa miaka 20, lakini aliyefanyiwa kitendo lazima aangaliwe.

" Pia anahitaji kusaidiwa kisaikolojia na matibabu ili kutoka katika hali ya kuathirika, kwa muda mrefu mkazo wetu ni kumuangalia mhalifu tu na kumsahau mwathirika wa uhalifu ambaye anachukulia kama shahidi katika kesi, "  amesema Profesa Kabudi.

Profesa Kabudi ambaye ni mtaalamu wa sheria ameeeleza hayo leo Jumanne Aprili 4, 2023 wakati akitoa maoni yake mbele ya Tume ya Haki Jinai inayokusanya maoni kuhusu mwenendo wa haki jinai wa kuangalia mfumo wa utoaji wa haki.

Tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Othman Chande pamoja na wajumbe mbalimbali wakiwemo viongozi waandamizi wastaafu wa jeshi la polisi.

Profesa Kabudi ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba katika maoni yake amekwenda mbali zaidi akitaka pia uwepo wa skimu ya fidia kwa waathirika wa uhalifu.

"Katika Katiba kuanzia ibara ya 9, 12 na 13 inasisitiza heshima na utu kwa kila mtu na binadamu wote wanastahili heshima na utu. Mhalifu anastahili heshima na utu vile vile mwathirika wa uhalifu anastahili utu na heshima," amesema Profesa Kabudi.

Profesa Kabudi ambaye pia ni Mbunge wa Kilosa mkoani Morogoro, amependekeza mfumo wa magereza uangalie zaidi namna ya kuwapa ujuzi wafungwa badala ya kubadilisha tabia zao pekee. Ameshauri wapewe ujuzi na elimu ili wakitoka wawe na shughuli za kufanya.

"Tuwe na mpango maalumu wa mafunzo magerezani, tuwe na Veta, pia wahalifu wenye umri mdogo na vifungo virefu wawezeshwe kusoma na kuhitimu katika ngazi mbalimbali," amesema Profesa Kabudi aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Pia katika mapendekezo yake, Profesa Kabudi amesema watu ambao makosa yao sio ya mauaji au ukatili Serikali ifikirie kuwepo kwa magereza ya wazi yatakayowawezesha watu hao kufanya shughuli nyingine za Taifa.

"Kama mwalimu au daktari akabiliwi na makosa mazito na ana tabia njema baada ya kuwa gerezani, tuanze kuwa na suala la magereza ya wazi. Ni muhimu kuwa na adhabu mbadala zitakazopunguza watu kwenda magerezani.

"Pia ni muhimu kuwepo chombo kitakachosimamia haki za watu mbalimbali ili panapokuwa na matumizi madaraka wajue pakwenda kutoa malalamiko yao au chombo hiki kuwaona," amesema Profesa Kabudi.