Kadi ya Nida kukutoa selo

Muktasari:

  • Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ametoa maagizo manane kwa mahakimu, likiwamo la kurahisisha masharti ya dhamana kwa Watanzania kujidhamini kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa(Nida) katika mfumo wa haki jinai, badala ya kutegemea watu wengine.

Tanga/Moshi. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ametoa maagizo manane kwa mahakimu, likiwamo la kurahisisha masharti ya dhamana kwa Watanzania kujidhamini kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa(Nida) katika mfumo wa haki jinai, badala ya kutegemea watu wengine.

Maagizo mengine ni mahakimu kuzuia maahirisho ya mara kwa mara ya kesi yasiyo na sababu za msingi na kuhakikisha maungamo yalichukuliwa ndani ya muda na kwa hiari.

Alitoa kauli hiyo wiki iliyopita, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Tanga huku akiwataka mahakimu kutokuwa wepesi kukubali hoja za waendesha mashtaka za upelelezi unaendelea.

Pia, aliwataka mahakimu kutokubali kuahirisha mashauri kwa muda mrefu ili kuandaa maamuzi madogo ya pingamizi na kuhakikisha hakuna mtuhumiwa anashikiliwa bila kufikishwa mahakamani ndani ya muda kisheria.

Jaji Juma alitaka mashauri ambayo washtakiwa wamekosa dhamana yasikilizwe haraka pamoja na kuwapo matumizi ya adhabu mbadala. Katika maagizo hayo yaliyopokewa na mahakimu kwa hisia tofauti na mawakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Juma aliwataka kuachana na mfumo wa makaratasi, badala yake watumie mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kurahisisha shughuli za utoaji haki kwa wananchi.

“Kwa kuwa Mahakama ni msimamizi wa haki ya kila mtu kuwa huru na kuishi kama mtu huru, ni wajibu kutoa dhamana kwa makosa yenye dhamana,” alisema Jaji Mkuu wakati akifanya majumuisho ya ziara yake hiyo.

“Vigezo vya kutumiwa kutoa dhamana ni pamoja na kutumia vitambulisho vya Taifa na vinavyokubalika. Mahakama ziwaruhusu washtakiwa wajidhamini zinapojiridhisha na utambulisho wao na watahudhuria mahakamani.

“Mtu anapojidhamini kwa kutumia kitambulisho cha Taifa anakuwa ameacha uraia wake mahakamani, hivyo hawezi kwenda popote bila kitambulisho hicho na kwamba inakuwa rahisi kumpata endapo atatoroka.”

Jaji Juma alisema ni muhimu kwa mahakimu kufuata taratibu wakati wa dhamana na wasifanye ugumu mtu kupewa dhamana kwa kuwa sheria imeweka wazi suala hilo, hivyo ni wajibu wao kufuata na kutekeleza kwa kufuata taratibu.

“Sasa hivi Serikali imeweka mfumo wa anuani za makazi unaorahisisha shughuli za Mahakama, hivyo mtuhumiwa atatambulika mpaka nyumba anayoishi sasa, kuna ugumu gani akijidhamini kwa kutumia kitambulisho cha Taifa?” alihoji Jaji Juma.

Pia, alisisitiza Mahakimu wahakikishe Mahakama inakuwa sehemu salama kwa mtuhumiwa kwa kuwa ndio mahala anapotarajia kupata haki kwa mujibu wa Katiba.

“Mtuhumiwa anapoletwa mahakamani anatakiwa ajione yupo mahali salama na mnawahoji, ukiona ametoka mahabusu ameletwa mahakamani ana vidonda mwilini amedhoofika muulize kwa utaratibu tatizo nini,” alisema Jaji Juma.

“Mahakama ni sehemu ya haki, hivyo wananchi wanatakiwa wakiwa hapa wajihisi wamefika mahali salama, sio kuanza kufokea kwa kumtishia nitakufunga, hili ni kosa muache mara moja.

“Mtu anapochelewesha ushahidi kila mara na kutoa ahadi kwamba bado wanaendelea kutafuta ushahidi hakimu usipende kukubali kirahisi na wewe mwambie aje na kiapo kwamba ametoa sababu na atakapokuja tena unamkumbusha kwa kiapo alichoapa. Hapa mtakwenda vizuri”

Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kanda ya Tanga, Humphrey Paya alisema wamelipokea agizo hilo litafanyiwa kazi kwa kufuata taratibu zote, kwa kuwa lengo ni kuhakikisha mahakimu wanaondoa vikwazo katika dhamana.


Mawakili ‘wampa tano’

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Mkoa Kilimanjaro, David Shillatu alisema kauli ya Jaji Juma ni ushindi mkubwa kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiulalamikia mfumo wa haki jinai nchini.

“Ni wazi NPS (Ofisi ya Taifa ya Mashitaka), hawatakubali kupeleka shauri mahakamani kama upelelezi haujakamilika, kutokana na maagizo hayo ya Jaji ya kuleta kiapo cha sababu za kuahirisha kesi,” alisema Shillatu.

“Hiyo hati ya kiapo aliyoagiza wailete Mahakamani wanapoomba ahirisho, ni dhahiri inakuwa kisu kwao, kwa kuwa wakifanya vinginevyo wataonekana wamesema uongo chini ya kiapo.

“Madhara ya kusema uongo chini ya kiapo yanafahamika, kwa kuwa unaweza kutupwa ndani kwa kudharau. Huu ni mwanzo mpya, kuelekea kwenye mapinduzi ya kweli katika uendeshaji wa mashauri ya jinai nchini,” alisema Shillatu.

Wakili Rwezaura Kaijage wa Mkoa wa Iringa alisema maagizo ya Jaji mkuu yanapaswa kuwa dira kwa mahakimu wote nchini kwa sababu mtuhumiwa anatakiwa aonekane hana hatia hadi atakapotiwa hatiani na kuhukumiwa.

“Naunga mkono maagizo ya Jaji mkuu, hasa hili la dhamana. Kwa makosa ambayo yanadhaminika tumekuwa tukipata shida sana mahakamani kwa mahakimu kutaka watu kuleta hati za nyumba, magari au barua za watendaji,” alisema wakili Kaijage.