Kagaigai awataka wakulima wa kahawa kuongeza ubora
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wakulima na wazalishaji wa kahawa nchini kuongezea ubora zao hilo lishindane katika soko la kimataifa na kupata bei nzuri.
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wakulima na wazalishaji wa kahawa nchini kuongezea ubora zao hilo lishindane katika soko la kimataifa na kupata bei nzuri.
Katika taarifa yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, kwenye hafla fupi ya kutoa zawadi kwa washindi watatu wa kahawa kwa mwaka 2021 leo Novemba 10, Kagaigai amesema ili kahawa inayozalishwa nchini iweze kupata bei nzuri katika soko la dunia, ni lazima iwe bora.
Amesema asilimia zaidi ya 90 ya kahawa inayozalishwa nchini, inategemea soko la nje ya nchi na kwamba uzalishaji wa kahawa bora ndiyo kutakaoifanya Tanzania, kuendelea kubaki kwenye ramani ya wazalishaji wa kahawa duniani.
"Tuwatake wakulima na wazalishaji wa Kahawa, kuongeza ubora wa kahawa, kwani ili tupate soko na bei nzuri, ni lazima kahawa yetu iwe bora iweze kushindana na soko la dunia, ili tupate bei iliyo bora, kwani wanywaji wangependa wanywe kahawa iliyo bora zaidi.
"Tanzania kama nchi mzalishaji na mwenye ardhi nzuri yenye rotuba, tuna fursa ya kushiriki katika kutoa kikombe bora cha kahawa duniani kwa kuongeza uzalishaji wa kahawa bora," amesema.
Ameongeza kuw wanunuzi watanunua kahawa kwa kuchagua kahawa bora zaidi sokoni.
"Nchi yetu hutegemea soko la nje la kahawa kwa zaidi ya asilimia 90 ya uzalishaji wetu na tunapokea bei inayopatikana katika soko la kimataifa, hivyo ubora wa kahawa yetu, ndiyo utaksotusaidia tubaki kwenye ramani ya wazalishaji na kuwa ba ushawishi kwa wakulima kuoata bei nzuri," amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo, amesema lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha wakulima, kuzalisha kahawa bora ili kuweza kupata masoko ya uhakika na bei nzuri.
"Ubora wa kahawa unatokana na muonjo wake na leo hapa tunatafuta kahawa bora. Kahawa inapokuwa bora na bei ya mkulima inakuwa nzuri zaidi na kahawa hizi ndizo tunazoenda kuzitangaza kwenye masoko ya kimataifa na masoko yake pia huwa bora," amesema Kimaryo.
Meneja Mauzo na Ubora wa Kahawa wa (TCB), Frank Nyarusi, alisema kwa mwaka huu wamepokea sampuli 65 za kahawa, ambapo walishindanisha aina tatu ambazo ni Arabika iliyooshwa, Arabika Ngumu na Robusta, ambapo majaji wabobevu walipata washindi wa kahawa bora kwa mwaka 2021.
Mmoja wa washindi wa kwanza kwenye uzalisha wa kahawa kutoka chama cha ushirika cha wakulima wa Mara, David Mwita ameiomba Serikali kuongeza nguvu katika Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nhini (TaCRI) ili kuondoa upungufu wa miche ya kahawa nchini hasa ile ambayo invumilia ukame na maradhi.
"Naomba Serikali itie nguvu zaidi kuongeza uzalishaji wa miche hasa hizi ambazo zinastahimilivu ukame pamoja na magonjwa pamoja na kuiongezea nguvu TaCRI ili miche ya kahawa iweze kupatikana kwa wingi zaidi," amesema Mwita.