Kamanda Muliro amtaka Makonda kuripoti polisi

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amemshauri Paul Makonda kwenda kituo cha polisi kuripoti tuhuma alizozitoa mtandaoni, ikiwamo ya kudai kutishiwa maisha.

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amemshauri Paul Makonda kwenda kituo cha polisi kuripoti tuhuma alizozitoa mtandaoni, ikiwamo ya kudai kutishiwa maisha.

“Sijaongea naye (Makonda), lakini kupitia ninyi (vyombo vya habari), namshauri aende kituo chochote cha polisi endapo madai aliyoyatoa yana ukweli. Inategemea yeye (Makonda) anakaa wapi, lakini aende kituo cha polisi cha karibu kwa ajili ya kutoa maelezo ya madai yake,” alisema Muliro.

Juzi katika mitandao ya kijamii zilisambaa taarifa zilizoibua mjadala zikimhusu Makonda, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ikiwamo iliyokuwa na kichwa cha habari, “nafahamu kuna mkakati unaoratibiwa na makundi matano kuangamizi maisha yangu.”

Hata hivyo, Kamanda Muliro alisisitiza umuhimu wa Makonda kwenda kutoa taarifa polisi, akisema hivi sasa mifumo inafanya kazi vizuri, hivyo akipeleka jambo lake hata kwa maandishi litashughulikiwa.

“Kazi yetu polisi kuchunguza malalamiko yoyote ya kijinai, lakini jambo linalochunguzwa lazima kuwepo kwa ushahidi wa kuridhisha. Narudia kama kweli amelalamika na madai yana ukweli basi aende kituo cha polisi cha karibu,” alisema Kamanda Muliro.