Kamati kuundwa kuchunguza moto ulioteketeza soko Karume

Muktasari:

  • Soko la Karume (soko la mchikichini) liliteketea moto usiku wa kuamkia leo Jumapili Januari 16, 2022 huku chanzo cha moto huo kikiwa hakijulikani.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla amewataka wafanyabiasha wa soko la Karume lililoungua kuwa watulivu huku akiahidi kuundwa kamati itakayochunguza kujua chanzo cha moto huo.

Makalla amesema hayo leo Jumapili Januari 16, 2022 alipotembelea eneo hilo na kukagua athari za moto huo.

Soko la Karume (soko la mchikichini) liliteketea moto usiku wa kuamkia leo huku chanzo cha moto huo kikiwa hakijulikani.

Imeelezwa kuwa moto huo ulioteketeza sehemu kubwa ya soko hilo lenye wafanyabiashara zaidi ya 3,500 ulianza usiku wa kuamkia leo huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likijitahidi kuuzima lakini uliteketeza soko hilo sehemu kubwa.

Akiwa akiwa kwenye eneo hilo Makalla amesema "Nawapa pole wafanyabishara wote kwa ajali hii ya moto hatujajua chanzo kwa kuwa yanaelezwa mengi, wengine wanasema umesababishwa na watu wanaopika maharage usiku ili wakifika asubuhi yameiva. Nawaomba kuweni watulivu katika kipindi hiki ambacho tunaunda kamati itakayochunguza kujua chanzo," amesema

“Tutaaunda kamati itakayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala kuchunguza kwa siku 14 kisha tutapokea majibu na kujua cha kufanya na wakati wote wa uchunguzi hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kuendelea na biashara katika eneo hili tutaangalia utaratibu mwingine,"amesema

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Wilaya ya Ilala, Elisa Mugisha amesema taarifa za moto huo walizipata baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja.

"Na kwa bahati nzuri wakati huo tulikuwa tunatoka Mabibo ambako nako kuna nyumba ilikuwa inaungua moto na tulifika hapa ndani ya muda mfupi tulifika eneo la tukio lakini moto ulikuwa mkali kutokana na asili ya bidhaa wanazouza hapa mbao, maturubahi na nguo na vinasambaza moto kwa haraka tulijitahidi kuzunguka soko na kuanza kuzima,"amesema

Amesema vibanda vimeungua kwa asilimia 98 na mali zilizokuwemo na niwachache waliofanikiwa kuokoa bidhaa zao hasa walioko pembezoni mwa soko.

"Tunachoshukuru Mungu hakuna madhara kwa binadamu na wala moto haukuvuka kwenda kwenye nyumba za wananchi kwa sababu tulikuwa na gari nne moja kutoka Kinondoni,Ilala, Bandari na Airport," amesema

Wafanyabiashara watofautiana na RC Makalla

Katika hali isiyokuwa ya kawaida wafanyabishara waliokumbwa na madhila ya kuteketea bidhaa zao Soko la Karume (soko la Mchikichini) wamepingana na agizo la Amos Makalla amepiga marufuku shughuli zozote kufanyika kwenye eneo hilo kabla ya kamati kumaliza uchunguzi.

Katika sintofahamu hiyo wafanyabishara hao walidai hawaelewi kinachoelezwa na kiongozi huyo baada ya kutoa maagizo katika kipindi cha kufanya uchunguzi hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kuendelea na shughuli zake katika eneo hilo.

Wakizungumza wakati kiongozi huyo anatoa agizo hilo, wamesema hali ya maisha yao kiuchumi ni ngumu na wakizingatia biashara walizokuwa wanaendesha kwenye soko hilo mitaji yao walikuwa wamekopa kwenye taasisi za kifedha hivyo hawakubali.

Juma Said amesema hawakubaliani na maagizo hayo ya kuwataka wasiendelee na shughuli kwenye eneo hilo kwani hawajuhi ndani ya siku 14 alizotoa wataishije.

"Mkuu wa Mkoa hatukubaliani naye anasema sisi tusifanye kazi kwenye eneo hili tupishe kamati ifanye uchunguzi, sisi tutaishije kwanza biashara yangu nilikuwa nimekopa na kila mwezi nafanya marejesho sielewi," amesema

"Nawaomba sana jambo hili watumie busara Kuna baadhi yetu wanawatoto wanatakiwa kwenda shule ukisema tusifanye kazi eneo hili basi tutafutiwe mbadala tuende wapi,"amesema Maria Salah mfanyabiashara wa nguo za mtumba ambaye Mali zake zimeteketea kwa moto.

Katika maelezo yake Makalla aliwataka wasiendelee kufanya kazi kwenye eneo hilo Hadi wabaini chanzo kilichosababisha kutokea kwa ajali hiyo lakini baada ya kuona baadhi wanapinga alilazimika kutumia nguvu kutoa maagizo hayo na kuliagiza jeshi la Polisi kusimamia ipasvyo eneo hilo.

"Naomba tusikilizane hakuna mtu kufanya biashara hapa hadi Kamati ichunguze  ndani ya siku 14 na kwa muda juu kwa kuwa maisha lazima yaendelee tutajua Cha kufanya nawaomba Polisi msimamie kikamilifu eneo hili," amesema Makalla