Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kamati, wabunge wafichua ‘matobo’ ya bajeti 2026/27

Muktasari:

  • Juni 11, mwaka huu Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, aliwasilisha bajeti hiyo ya mwaka 2026/27, ikitaja baadhi ya hatua za kubana matumizi ikiwamo kupunguza safari za ndani na nje, semina, warsha na makongamano



Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwasilisha bajeti ya Sh62.3 trilioni, Kamati ya Bunge ya Bajeti imesema hatua za kubana matumizi zilizotajwa hazitekelezeki huku ikiitaka Serikali kupitia upya baadhi ya mapendekezo kwa kuwa, yanaumiza wananchi na vijana.

Juni 11, mwaka huu Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, aliwasilisha bajeti hiyo ya mwaka 2026/27, ikitaja baadhi ya hatua za kubana matumizi ikiwamo kupunguza safari za ndani na nje, semina, warsha na makongamano.

Pia, Serikali kupitia bajeti hiyo ilipendekeza kuongezwa ushuru wa bidhaa kwa pikipiki kwa asilimia tano na ushuru kwa magari chakavu kutoka asilimia 15 hadi 20; kwa magari yenye miaka minane hadi 10 asilimia 30 hadi 40 na yenye miaka 10 hadi 20 asilimia 50.

Aidha, ilipendekeza mabadiliko ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura ya 147, Sheria ya Kodi ya Mapato Sura ya 332, Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura ya 220 na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mashimba Ndaki, akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Juni 15, 2026 wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Picha na Said Khamis.

Kamati hiyo, imetaka kutafakariwa upya kwa mapendekezo hayo, ikisema baadhi yana athari kwa ustawi wa vijana na kuhatarisha kuirejesha nchi katika mikataba iliyoiingiza katika hasara.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mashimba Ndaki alipowasilisha tathmini ya hali ya uchumi kwa mwaka 2025/26 na mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2026/27.


Hazitekelezeki

Amesema kamati imefanya uchambuzi wa aya ya 67 ya hotuba ya bajeti hiyo inayoonesha dhamira ya Serikali katika kusimamia matumizi ya fedha za umma na kubana matumizi.

Baada ya uchambuzi huo, amesema kamati imebaini hatua za kubana matumizi zilizowasilishwa ni zilezile ambazo Serikali imekuwa ikizitaja miaka yote na baadhi hazitekelezeki.

“Baadhi ya hatua hizo hazilengi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, baadhi ya maofisa masuhuli kutokeleza vema sheria ya usimamizi wa fedha na umma na maandalizi hafifu ya miradi ya maendeleo inayosababisha gharama za miradi kutoendana na thamani ya fedha,” amesema.

Hata hivyo, amesema uzoefu unaonesha kubana matumizi yasiyo ya lazima ni njia bunifu na ya uhakika inayotumika na nchi nyingi ili kuweka nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis

Aidha, ameeleza njia hiyo inawezesha kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo endapo kuna upungufu wa rasilimali fedha.

“Mifano ya nchi zilizotumia mkakati wa kubana matumizi ni pamoja na Afrika Kusini, Zambia na Ivory Coast. Kamati inaitaka Serikali kupitia upya bajeti ya matumizi ya kawaida na kupunguza matumizi ambayo hayawezi kuathiri utekelezaji wa bajeti,” amesema.


Ushuru pikipiki, magari chakavi

Kuhusu ushuru uliopendekezwa na Serikali katika bodaboda na magari chakavu, Ndaki amesema kamati imeitaka Serikali itafakari upya kwa sababu bodaboda zimetoa fursa ya ajira kwa vijana wengi na zinanunuliwa zikiwa mpya.

“Sababu ya pili, wananchi wa kipato cha chini ndio wanunuzi wakubwa wa magari chakavu, kiwango kinachopendekezwa cha ushuru ni kikubwa na kitaathiri sio tu bei ya pikipiki hizo bali ajira za vijana wanaojiajiri kupitia biashara ya kusafirisha abiria na uwezo wa mwananchi mwenye kipato cha chini kumiliki gari,” amesema.

Mbunge wa Gairo (CCM), Ahamed Shabib akizungumza wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis

Aidha, Ndaki ameitaka Serikali kutafakari upya mapendekezo ya marekebisho ya sheria nne, kwa sababu yanarejesha utaratibu wa mikataba ya makubaliano iliyoiingiza hasara katika Taifa, kwa kuwa, baadhi ilikuwa na vifungu vya mwendelezo wa kutolipa kodi.

“Madini ni rasilimali inayokwisha, tusipokuwa makini tutabaki na mashimo ya madini bila kupata kodi ya aina yoyote. Uamuzi huu ni vyema ukaangaliwa upya,” amesema Ndaki, aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Amelitaka Bunge litambue kwamba, kwa kupitisha mabadiliko hayo ni wazi linakasimu mamlaka yake ya kutunga sheria za kodi kama ilivyoelekezwa katika ibara ya 138 ya Katiba kwa Baraza la Mawaziri.


Bima ya afya

Kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, Ndaki amesema utekelezaji wa mpango huo utaanza kwa kaya zilizotambuliwa katika awamu ya majaribio huku Serikali ikijiridhisha kwanza na uwezo wa kifedha na uhimilivu wa mfuko kabla ya kupanua huduma kwa awamu nyingine.

Amesema Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote imeanzisha Mfuko wa Usawa utakaogharamia matibabu ya wasiokuwa na uwezo, wagonjwa wa magonjwa sugu na huduma za dharura zitokanazo na ajali.

Pia, kamati imeipongeza Serikali kwa kuanzisha vyanzo vya ziada vya mapato kwa ajili ya mfuko huo.

Kwa mujibu wa mpango huo, kaya zisizo na uwezo ni milioni 3.91, sawa na asilimia 26.4 ya wananchi wa Tanzania Bara, zinatarajiwa kunufaika.


Hata hivyo, hadi sasa kaya 931,693 pekee ndizo zimetambuliwa, huku kaya milioni 2.98 zilizobaki zikitarajiwa kutambuliwa kwa miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 hadi 2028/29.

Ndaki, amesema gharama za kuhudumia kaya zote zisizo na uwezo zinakadiriwa kufikia Sh691.3 bilioni kwa mwaka, lakini vyanzo vya sasa vina uwezo wa kukusanya Sh201.9 bilioni pekee, hivyo kuacha pengo la Sh489.5 bilioni.

Kutokana na hali hiyo, kamati imeitaka Serikali kuendelea kukusanya na kulinda fedha za mfuko wakati shughuli ya utambuzi wa walengwa likiendelea.

Aidha, kamati imehimiza kukamilishwa kwa mfumo wa Universal Health Data ili kurahisisha uratibu wa huduma za bima ya afya kwa wote, ikibainisha kuwa kwa sasa kuna mifumo 15 ya afya isiyosomana.

Pia, imependekeza matumizi makubwa ya teknolojia katika utoaji wa huduma za afya na kutafutwa kwa vyanzo vipya vya mapato, ikiwamo tozo kwenye bidhaa zenye athari kwa afya kama vilevi, sigara, shisha na vinywaji vya kuongeza nguvu.


Deni la Serikali

Kuhusu deni la Serikali, Ndaki amesema hadi Machi 2026 lilifikia Sh114.3 trilioni kutoka Sh104.9 trilioni mwaka mmoja kabla huku likiwa sawa na asilimia 48.8 ya Pato la Taifa dhidi ya ukomo wa asilimia 55. Kati ya deni hilo, asilimia 66.4 ni deni la nje na asilimia 33.6 ni deni la ndani.

Kamati imebaini changamoto mbalimbali ikiwamo mikopo kutumika kuziba nakisi ya bajeti, maandalizi hafifu ya miradi na baadhi ya fedha za mikopo kuelekezwa kwenye matumizi ya kawaida badala ya maendeleo.

Pia, imeonya kuwa baadhi ya viashiria vya deni vinaanza kukaribia viwango vya ukomo, hali inayoweza kuathiri uwezo wa nchi kukopesheka kimataifa siku zijazo.

Kutokana na hali hiyo, kamati imeishauri Serikali kuelekeza mikopo kwenye miradi ya kimkakati yenye tija, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuhamasisha mashirika ya umma kutafuta fedha kupitia masoko ya mitaji badala ya kutegemea mikopo ya Serikali Kuu.


Michango ya wabunge

Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby ameishauri Serikali kuanzisha chombo maalumu cha kuchunguza matumizi ya fedha katika wizara, taasisi na miradi ya maendeleo kabla ya kuendelea kutoa fedha zaidi, akisema hatua hiyo itasaidia kudhibiti matumizi yasiyo na tija na kuongeza ufanisi wa fedha za umma.

“Lazima kuwa na chombo maalumu kinachokwenda kujiridhisha kwanza. Muangalie hili daraja, kweli Sh10 bilioni zimetumika? Kama Sh5 bilioni zimetumika kweli tupeleke nyingine, msipoangalia itakuwa hela zinachukuliwa lakini matumizi yatakuwa mengine,” amesema.

Mbunge wa Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa  akizungumza wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis

Mbunge wa Bariadi Vijijini (CCM), Massanja Kadogosa amesema ili kufikia ukuaji wa uchumi wa asilimia 10 ni lazima kuwa na ukuaji mdogomdogo huku akisema vipaumbele vilivyowekwa ni moja ya njia ya kufikia ukuaji huo.

Akizungumza moja ya jambo zuri lililofanyika amesema ni msamaha wa kodi kwa mwaka mmoja kwa watu wanaofungua biashara, huku akisema nchi nyingi zilizoendelea uchumi wake unategemea kwa kiasi kikubwa biashara ndogo.

Amesema licha ya umuhimu wake ni lazima kuwa na sera nzuri ili kuhakikisha biashara zinapoanza, zisife kwa kuwa asilimia 95 ya biashara hizo hufa ndani ya miaka mitano.

Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo amependekeza Tanzania kuelekeza nguvu zake katika sekta sita za kimkakati ili kuharakisha ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini na kufikia lengo la kuwa uchumi wa Dola1 trilioni za Marekani katika miaka 25 ijayo.

Miongoni mwa maeneo yanayapaswa kupewa kipaumbele ili kubeba uchumi wa Tanzania ni kilimo na viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao akipendekeza sekta hiyo ichangie angalau asilimia 30 ya Pato la Taifa.

Amesema pamoja na kilimo kuwa uti wa mgongo wa uchumi, bado nchi inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa mbegu bora na matumizi madogo ya mbolea.

Eneo lingine alilopendekeza ni gesi asilia ambalo amesema ni vyema kuhakikisha inachangia asilimia 25 ya Pato la Taifa kwa kuweka miundombinu itakayofanya gesi hiyo ilete matunda.

Muhongo aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ametaja utalii na viwanda vinavyohusiana na sekta hiyo akisema Tanzania inaweza kuongeza mapato ikiwa itawekeza katika huduma na miundombinu.