Kamati ya Bunge yacharuka, yataka makandarasi wazembe wanyimwe miradi

Wajumbe wa Kamati  ya kudumu ya Bunge ya uwekezaji wa mitaji ya umma (PIC)  wakitembelea miradi ya Rea mkoani Arusha

Muktasari:

  • Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetakiwa kuwaorodhesha makandarasi wanaochelewesha miradi kinyume na mikataba yao, kisha kuwanyima zabuni za miradi mingine.

Arusha. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuwachukulia hatua za kinidhamu makandarasi wanaochelewesha ukamilishwaji wa miradi kinyume na mikataba.

 Moja ya hatua hizo ni kuwaorodhesha na kuyawasilisha majina yao kwa mamlaka husika, ili wasipewe tena utekelezaji wa miradi mingine.

Hayo yamesemwa jana Machi 14, 2024 jijini Arusha na Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Deus Sangu baada ya kutembelea mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya pili katika vijiji vya Maswara Mkoa wa Manyara na Mswakini juu mkoani Arusha.

Sangu ambaye pia ni Mbunge Kwela mkoani Rukwa, amesema wameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, huku wakiwataka REA kuongeza usimamizi kwa makandarasi wenye kasi ndogo wafanye kazi zao kwa wakati na kwa kuheshimu mikataba waliongia, ili lengo la Serikali lifikiwe hadi mwishoni mwa mwaka huu.

"Kuna baadhi ya maeneo wakandarasi wako nyuma ya muda, nendeni mkawasimamie zaidi na mkiona kuna ukwamo orodhesheni majina yao wafahamike, ili wasipewe kazi tena," amesema Sangu.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha REA wanasimamia vyema jukumu la kuhakikisha nishati ya umeme inafika katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara hadi mwishoni mwa 2024.

"Awali, jukumu hilo lilionekana kuwa gumu na lisingetekelezwa kwa wakati, lakini hadi Machi, 2024 jumla ya vijiji 11,837 vimefikiwa na nishati ya umeme, sawa na asilimia 96 ya lengo, hakika kamati nzima tumefarijika kuona jinsi mambo yanavyokwenda vizuri," amesema Sangu.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alisema mkoa wa Manyara una jumla ya Vijiji 441 ambapo kati ya hivyo, vijiji 420 vimeshafikiwa na huduma ya umeme, huku vijiji 14 vikiwa katika hatua za mwisho za majaribio na saba vikiendelea na utekelezaji na kwamba hadi Juni 2024 vitakuwa na nishati hiyo.

 Amesema kwa Mkoa wa Arusha asilimia 95 ya Vijiji vimefikiwa na huduma ya umeme ambayo ni Vijiji 352 kati vijiji vyote 368 vilivyopo, huku akiahidi vijiji 16 vilivyobakia vikitarajiwa kukamilika kabla ya  Juni, 2024.

"Kwa baadhi ya wakandarasi walioko nyuma ya muda, nitumie nafasi hii kuahidi mbele yako kuwa, hatutawafumbia macho kutuharibia kwa wananchi, bali tutasogeza zaidi usimamizi wetu kwao ili wakamilishe jukumu hilo kwa wakati," amesema Saidy.

Wakizungumzia utekelezaji wa miradi hiyo, Salma Mohamed wa Kijiji cha Maswara amesema  wamefarijika eneo lao kufikiwa na umeme ambao umesaidia kupata baadhi ya huduma katika kituo cha afya Masware, ikiwemo chanjo, huduma ya mama na mtoto pamoja na kujifungua wakati wote.

"Umeme jamani ni uchumi, maana mbali na kusaidia huduma za afya pia mashine yetu ya kusindika nafaka sasa inafanya kazi na vijana hawazururi tena, kwani wamefungua biashara ndogo ndogo za kiujasiriamali" amesema Salma.