Kamati ya Bunge yashauriwa matrekta ya URSUS yateketezwe
Muktasari:
- Wakulima Kiteto waomba wafutiwe madeni kufuatia kukopeshwa matrekta ya URSUS ambayo ni mabovu wakisema lengo la kuwatoa kwenye jembe la mkono halikufanikiwa.
Kiteto. “Kama unaona kitu ni kibovu kinasumbua watu, unapeleka wapi huoni kinaweza kumsumbua watu wengine na kuwatia presha, kwanini matrekta haya yasiteketezwe kwa kuchomwa moto,” amesema.
Akizungumza na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo Viwanda na Biashara Mei 28, 2023 Mollen Mwagile (mkulima) amesema kwa nia ya Serikali ni kumnasua mkulima na jembe la mkono kwa kumsogeza zana bora za kilimo na kuletewa ambazo hazina ubora, haya matrekta ya URSUS yateketezwe kwa moto na wakulima wasamehewe madeni yao na kama wanataka waweke haya matrekta makumbusho.
"Nashukuru kamati ya Bunge kuja hapa... mwenyekiti wakulima tumeathirika kwa kiasi kikubwa sana mpaka sasa mikono yangu haifanyi kazi vizuri presha inanisumbua sana madeni hapa nadaiwa baada ya kukopa…," amesema.
Agnes Jackson (wananchi) anesema mume wake amemtelekeza na watoto kwa miaka miwili amekimbia madeni na hajui alipo hivyo kumfanya aishi kwa tabu na kuiomba Serikali kumsaidia kwani anamzigo mkubwa kulea familia yake mwenyewe baada ya mume wake kukimbia madeni.
"Alipoona kuwa trekta linasumbua na anatengeneza bila mafanikio alikimbia miaka miwili iliyopita na akimpigia simu wakati mwingine anapatikana anasema anaogopa kurudi watu wanamdai madeni yao,"amesema.
Akizungumza na kamati hiyo Rojas Mshikemshike (mkulima) alisema baada ya kukutana na mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo Taifa (NDC), Babati Manyara akihamashisha wakulima kukopa matrekta hayo, yeye alitoa Sh1 milioni na kupatiwa huku akitakiwa kuhamasisha wakulima wengine zaidi ili wakakope NDC," amesema.
"Hili trekta nilipewa kama mfano kwa wakulima waone kwa vitendo na wakati huo nililipakia kutoka Kibaha, Pwani hadi Morogoro na kuanza maonyesho kwa wakulima ili wananchi waone na kukopa," amesema Rojas.
Alisema matrekta hayo yalikuwa 400 na mengine mia 800 yalishafika bandarini yakitakiwa kusambazwa kwa haraka kwa wakulima huku akidai alipewa kazi kuhakikisha biashara hiyo inafanikiwa kwa kuhamasisha wakulima.
Alisema wakati huo changamoto ilianza kujitokeza kwa matrekta hayo kuanza kuharibika na kuendelea kuwaelekeza wamiliki namna ya kureesha katika hali zao kwa kuwa yeye alikuwa fundi fundi
"Nilipigiwa simu kuna trekta inavuruga biashara Kiteto na kuna mtu imemshinda inamsumbua ana kaitelekeza porini na kuikimbia…nikatakiwa niende kuichukua na kufanya hivyo,"amesema Rojas
Mbunge wa Jimbo la Kiteto Edward Ole Lekaita akizungumza mbele ya kamati hiyo alisema baada ya malalamiko mengi ya wananchi wa Kiteto na nchi nzima mapema kabisa bunge aliulizwa swali na kujibiwa na Naibu waziri wa Kilimo na Mifugo kuwa Serikali inashughulikia pamoja na mambo mengine pia alimwomba akutane na wakulima hapo na kufika.
"Baada ya swali lile nilipigiwa sana simu na wakulima nchini.. karibia nch nzima kuelezwa matatizo ya wakulima hao ambao walikopeshwa matrekta hakika yalikuwa mengi sana hivyo leo Mei 28.2023 Bunge limetuma kamati ikutane na wakulima na mimi nashukuru sana Serikali imesikia kilio cha wananchi," amesema Ole Kaita.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati hiyo David Kehenzile Mwakiposa amesema baada ya kuongea na wakulina na kusanya maoni yao Kiteto, ataenda Hanang na Mbulu kisha watarejesha taarifa Bungeni ambapo zitachakatwa na kutolewa maamuzi