Kamati ya Bunge yataka Tanapa kupewa fedha

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Silaa akiwasilisha taarifa ya kamati yake kwa kipindi cha Februari mwaka 2022 hadi Januari 2023 leo Februari 7, 2023. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imeliomba Bunge kuazimia kuitaka Serikali kutoa fedha za kutosha kwa Shirika la Hifadhi Nchini (Tanapa) ili kuwezesha ufanisi kwenye hifadhi 22.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, (PIC) imeitaka Serikali kulipatia fedha za kutosha Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) ili liweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuleta tija kwa nchi.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Februari 7,2022 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerry Silaa wakati akiwasilisha taarifa ya kamati yake kwa kipindi cha Februari mwaka 2022 hadi Januari 2023.

Amesema Tanapa imeongezewa idadi ya hifadhi kutoka 16 hadi 22 na kusababisha changamoto ya fedha za uendeshaji na za kutekeleza miradi ya uwekezaji ya hifadhi.

“Kutokutekeleza miradi ya uwekezaji ya hifadhi kunaathiri upatikanaji wa mapato ya kutosha kutokana na kupungua kwa watalii kwani mazingira ya hifadhi hayarithishi, hivyo kukosekana ufanisi na tija ya uwekezaji katika hifadhi,”amesema.

Ametaka Bunge linaazimie kwamba, Serikali ihakikishe inaipatia Tanapa fedha za kutosha ili kuongeza ufanisi katika hifadhi zote 22 hivyo, waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na tija iweze kupatikana.