Kambi Zuberi, wenzake wasomewa upya mashtaka ya uhujumu uchumi
Aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba Sport Club, Muharami Sultani(wa kwanza kulia) akiwa na washtakiwa wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Hii ni mara ya pili, washtakiwa hao kufikishwa katika Mahakama ya Kisutu, kwa mara ya kwanza Novemba 21, 2022, ambapo walisomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka manane yakiwemo ya kusafirisha heroini yenye uzito wa kilo 34.89
Dar es Salaam. Saa chache baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kufuta kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikiwakabili mmiliki wa Cambiasso Sport Academy, Kambi Zuberi Seif na wenzake watano, washtakiwa hao walikamatwa tena na leo Ijumaa Juni 19, 2026 kufikishwa upya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusomewa mashtaka yanayofanana na yale ya awali.
Katika shauri jipya la uhujumu uchumi namba 13825 la mwaka 2026, Kambi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka manane, yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 34.89 na kutakatisha fedha.
Mbali na Kambi (40), washtakiwa wengine ni aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba SC, Muharami Sultani maarufu Shilton (40), Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54), Said Matwiko (41), John Andrew maarufu Chipanda (40) na Sarah Joseph.
Hatua hiyo imekuja baada ya DPP jana Juni 18, 2026 kutumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 92(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kufuta kesi ya awali ya uhujumu uchumi namba 71 ya mwaka 2022 iliyokuwa ikiwakabili washtakiwa hao katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi.
Baada ya kufutiwa kesi hiyo, washtakiwa walikamatwa tena na kufunguliwa shauri jipya ambalo leo limesomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Kambi Zuberi akiwa na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya uhujumu. Picha na Hadija Jumanne
Kabla ya kusomwa mashtaka, Hakimu Nyaki aliwaeleza washtakiwa kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Aidha, aliwaeleza kuwa shitaka la utakatishaji fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Akiwasomea hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Erick Mabagala, alidai kuwa kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na Pwani, washtakiwa wote waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroini Hydrochloride.
Katika shitaka la pili, Jamhuri inadai kuwa Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule wilayani Ilala, washtakiwa hao walikutwa wakisafirisha heroini yenye uzito wa kilo 27.10.
Shitaka la tatu linadai kuwa Novemba 4, 2022 katika eneo la Kamegele wilayani Mkuranga, washtakiwa walikutwa wakimiliki heroini yenye uzito wa kilo 7.79.
Mashtaka mengine matano yanamhusu Kambi peke yake, ambaye anadaiwa kutakatisha fedha kwa kujipatia magari matano aina ya Tata kupitia kampuni ya Safia Group of Companies Ltd kati ya Aprili 15 na 25, 2021 huku akijua mali hizo zilipatikana kutokana na shughuli za uhalifu.
Baada ya mashtaka kusomwa, upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.
Hata hivyo, wakili wa utetezi, Josephat Mabula, alihoji hatua ya Jamhuri kueleza kuwa upelelezi haujakamilika wakati washtakiwa hao walikuwa tayari wamefikishwa Mahakama Kuu baada ya kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo (committal proceedings) katika kesi ya awali.
Alidai kuwa kwa kuwa kesi ya kwanza ilifutwa na kufunguliwa upya, ilikuwa muhimu kwa upande wa mashtaka kuieleza mahakama hatua iliyofikiwa katika upelelezi wake.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Mabagala alisisitiza kuwa upelelezi bado unaendelea na kwamba Jamhuri itatoa taarifa rasmi mara utakapokamilika.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Nyaki aliahirisha shauri hilo hadi Juni 29, 2026 kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa wote walirudishwa rumande kutokana na uzito wa makosa yanayowakabili, ikiwemo shitaka la utakatishaji fedha ambalo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.