Kamera zilivyosaidia kuwatia hatiani askari Magereza watatu

Dodoma. Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa, imewatia hatiani askari Magereza watatu kwa kosa la kusababisha kifo cha Richard Bukombe Bulole.

 Hata hivyo, kilichosaidia askari hao kutiwa hatiani ni teknolojia ya picha (CCTV kamera) iliyofungwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, kwani awali walikana kuhusika na tukio hilo.

 Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Janeth Musaroche, askari hao walihukumiwa mmoja kifungo cha miaka mitatu na wawili miezi sita kila mmoja au kulipa faini.

 Waliohukumiwa ni askari mwenye namba B.1729, Patrick Msengi ambaye katika kesi hiyo alikuwa ni dereva na ndiye alihukumiwa miaka mitatu au kulipa faini ya Sh100,000.

Wengine waliomsaidia kuubeba mwili huo ni B. 4469, Denis Juma Mhina na B. 9377, Bakari Juma Bakari ambao walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh30,000 katika kosa la usalama barabarani lililosababisha kifo, ambapo wote walilipa faini.

 Katika shtaka hilo, ilielezwa kuwa mnamo Septemba mwaka jana katika eneo la Twiga Hoteli (Miyuji), watatu hao wakiwa na gari MT 0061 Toyota Land Cruiser likiendeshwa na Patrick, walimgonga mtembea kwa miguu Richard Bulole na kusababisha kifo chake papo hapo kisha walishuka na kubeba mwili wake.

 Taarifa zinaonyesha, mara baada ya ajali hiyo, walikimbiza gari wakiwakwepa bodaboda hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na moja kwa moja waliupeleka chumba cha kuhifadhia maiti, ambapo waliandika maelezo kuwa wamekuta amekufa barabarani na hafahamiki.

 Habari za mwili huo na jinsi ulivyopelekwa hospitalini ziliandikwa na gazeti hili, ndipo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni akaahidi kulifuatilia jambo hilo ili haki itendeke.

 Katika ushahidi wao, hospitali walipeleka video ikiwaonyesha askari hao wakiingia hospitalini na gari na jinsi walivyoushusha mwili huo na kupokelewa chumba cha kuhifadhia maiti.

 Baada ya ushahidi huo, watuhumiwa walikiri ni picha zao na kuomba wasamehewe.

 Katika hukumu hiyo, Musaroche alisema Mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa watuhumiwa walitenda kosa hilo na kusababisha kifo, lakini kukiri kwao kumewasaidia kupunguziwa adhabu.

 Ofisa Habari wa Hospitali ya rufaa ya Dodoma, Mwahija Amrani alisema tangu wamefunga mtambo wa CCTV kamera wamepunguza malalamiko mengi yaliyokuwa yakielekezwa kwao wakati mwingine pasipo na uhakika pamoja na kudhibiti utendaji wa watumishi, ikiwamo utoro.