Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kampeni ukaguzi magari ya shule, 10 yadakwa

Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Zauda Mohamed,akikagua moja ya magari ya shule,leo Jumatatu Januari 13,2025 jijini Arusha

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa  Mkuu wa Kikosi hicho mkoani Arusha,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Zauda Mohamed, amesema magari hayo ni ambayo hayakukaguliwa ambapo baadhi yao wametozwa faini huku mengine yakizuiwa kufanya shughuli zake na kupewa muda wa kwenda kuyafanyia matengenezo

Arusha/Simiyu. Jeshi la Polisi nchini limeendelea na kampeni yake ya kuyakamata magari ya shule ambayo yamekiuka agizo la kukaguliwa kabla ya shule kufunguliwa.

Inaelezwa kuwa lengo la kampeni hiyo inalenga kuboresha viwango vya usafirishaji wa wanafunzi.

Mkoani Arusha kikosi hicho kilianza msako huo wa kuwamakata madereva wote waliokaidi kupeleka magari yao kukaguliwa.

Ukaguzi huo ulianza Desemba mwaka jana wakati shule zimefungwa na nia ni kutaka kuondokana na ajali zinazosababishwa na ubovu wa magari hayo ambayo yanalalamikiwa na wazazi wengi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Januari 14, 2025, Mkuu wa Kikosi hicho mkoani Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Zauda Mohamed, amesema baadhi yametozwa faini kwa mujibu wa sheria.

“Hadi sasa magari 10 yamekamatwa na kati ya hayo, kuna yaliyotozwa faini na mengine yamezuiwa kufanya kazi mpaka yatakapofanyiwa matenegenezo

“Tutayaruhusu kufanya shughuli zake tukiridhika na matengenezo yatakayokuwa yamefanyika, kazi hii ya ukaguzi bado inaendelea kufanyika mkoa mzima,”amesema kamanda huyo.

Jana alisema kikosi hicho kilitangaza kuanza rasmi kampeni ya ukaguzi wa magari yote yanayobeba wanafunzi kwa kuwa shule nyingi zilifunguliwa.

Alisema takwimu za mkoa huo wa Arusha zinaonesha una magari 563ya shule yanayobeba wanafunzi, lakini baada ya ukaguzi wa hiyari kukamilika, ikabainika kuna magari 178 hayakupelekwa kukaguliwa.

“Nitoe wito kwa wamiliki wote wa magari hayo ambayo hayajakaguliwa wayalete yakaguliwe lengo ni kuhakikisha usalama wa watoto wetu,” amesisitiza Mohamed.


Lakini pia ametoa rai kwa wananchi kushirikiana na Jeshi kuwaelekeza wanafunzi wa madarasa ya awali na shule za msingi matumizi sahihi ya barabara kwa tayari ni kundi jipya na kubwa lililoanza kutumia barabara hivi sasa.

 Mkoani Simiyu

Wakati huo huo, Mkuu wa Polisi kikosi cha Usalama barabarani mkoani Simiyu, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Philibert Rwomunshaka amesema kabla ya shule za msingi na sekondari kufunguliwa Januari 13 mwaka huu tayari walikuwa wamekagua magari hayo na lengo lilikuwa kuhakikisha vyombo hivyo vinakuwa salama.

Anasema ukaguzi wa awali ulifanyika katika maeneo ya wilaya za Bariadi, Maswa, Busega, Meatu na Itilima.


"Tunashukuru wamiliki wote wa shule wanaotumia magari kusafirisha wanafunzi tulipowapa wito wa kuleta magari kwa ajili ya ukaguzi waliyaleta na tumeyakagua, hatutakubali kuona gari bovu linatumika kubeba wanafunzi,” amesema.

Kamanda Rwomunshaka amesema katika ukaguzi huo walibaini changamoto mbalimbali kwa baadhi ya magari hayo na walitoa maelekezo kwa wamiliki kuhakikisha wanayafanyia matengenezo kabla ya shule hazijafunguliwa yarudishwe yakakaguliwe tena.

“Niwatoe wasi wasi wazazi na walezi wa watoto wanaotumia magari ya shule katika mkoa wetu wa Simiyu, magari hayo yalikaguliwa mara mbili na tukahakikisha yako,” amesema.

Hata hivyo, amezitaja baadhi ya changamoto zilizoonekana kwa baadhi ya magari hayo kuwa ni pamoja na kukosa mikanda pamoja na ubovu wa viti, “lakini yote yaliyobainika kuwa na tatizo hilo wamerekebisha na tumeyakagua upya.”

Rwomunshaka amewasisitiza madereva na watumiaji wote wa vyombo vya moto kuendelea kufuata utaratibu, sheria na kanuni za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na nakutoendesha kwa mwendo kasi ili kupunguza ajali zisizo za lazima.

"Nasisitiza madereva wote wa mkoa huo kuheshimu vivuko vya watembea kwa miguu kwa kuwapa vipaumbele wanao vuka,"amesema.

Pia amesema ni muhimu kwa madereva wote katika mkoa wa Simiyu kuzingatia maadili ya udereva.