Kampuni zaingia ubia kuzifanya taka kuwa bidhaa
Mkurugenzi Mkuu wa Chanzi Tanzania, Andrew Wallace alipokuwa akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Kampuni hiyo Leo jijini hapa.
Muktasari:
- Ubia huo unaojumuisha kampuni za Tanzania Breweries Limited (TBL), AB InBev, Unilever pamoja na kampuni za Kitanzania za Chanzi na P4G, umewekeza takriban Sh5.76 bilioni ambapo unatarajia kujenga vituo vya kuchakata taka ngumu nchini Kenya na Afrika Kusini huku ukipanua vituo vya hapa nchini katika mikoa ya Arusha na Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Katika jitihada za kupunguza athari zitokanazo na taka ngumu nchini, kampuni mbalimbali zimeingia ubia ili kuimarisha usimamizi na udhibiti wa taka kwa kuzipa thamani.
Ubia huo unaojumuisha kampuni za Tanzania Breweries Limited (TBL), AB InBev, Unilever pamoja na kampuni za Kitanzania za Chanzi na P4G, umewekeza takriban Sh5.76 bilioni ambapo unatarajia kujenga vituo vya kuchakata taka ngumu nchini Kenya na Afrika Kusini huku ukipanua vituo vya hapa nchini katika mikoa ya Arusha na Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Chanzi Andrew Wallace alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa kampuni hiyo leo jijini hapa.
Akieleza msukumo wa kuanzisha mradi wa Chanzi, Wallace amesema ni kukabiliana na tatizo la taka hapa nchini kwani tatizo hilo ni janga la kitaifa.
Amesema asilimia 50 ya taka zimekuwa zikiishia majumbani, mashuleni na mitaani, huku asilimia 50 nyingine zikishia ardhini, jambo ambalo halikubaliki.
"Tunachokifanya hapa ni njia ya kitaalamu na ya faida ya kusimamia taka. Taka tunazifanya kuwa kitu cha thamani na ndio maana niliona ipo haja ja kuanzisha mradi huu.
"Tunazalisha chakula cha wanyama chenye protini ambacho ni bora na nafuu," amesema Wallace.
Ameongeza kuwa kutupa taka kwenye madampo sio suluhilo la uchafu, kwani jamii inahitaji suluhisho bora na la kudumu, hivyo ni muhimu kukumbatia biashara ambazo nisuluhisho la kudumu katika kuondoa tatizo la taka kwenye jamii.
Kampuni hizo mpya ulioingiwa a kampuni kuimarisha mbalimbali unatarajiwa kuimarisha usimamizi wa taka nchini kwa kuzipa taka thamani huku ukiongeza ajira kwa Watanzania.
"Kuanzia January tumeweza kuchakata takriban tani 3,000 na tunatazamia kufanya zaidi katika kipindi kijacho," amesema Wallace.
Naye Mkurugenzi wa tafiti za Mazingira, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Dk Menani Jangu amesema uwepo wa kiwanda hicho ni picha halisi ya jitihada zinazofanywa na wadau binafsi katika kukabiliana na changamoto ambazo nchi inapambana nazo.
"Changamoto ya kushughulikia taka ngumu katika miji yetu mikubwa imekuwa ni kubwa kutokana na kukosa maeneo ya kutupa taka zetu," amesema.
Dk Jangu amesema uwepo wa kiwanda hicho utasaidia kuchakata taka na kuzifanya kuwa mbolea na chakula cha wanyama kutokana na wadudu wanaotumika kubadilisha taka hizo.
"Sasa taka zitapungua kwenye madampo yetu ambayo mengi hayana uwezo lakini pia taka zinabadilishwa kutoka taka na kuwa na thamani," amesema.
Aidha amesema upatikanaji wa mbolea ya samadi kutokana na taka hizo ngumu utasaidia nchi kuwa na kilimo endelevu kutokana na ubora wa mbolea hizo kutoathiri mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Jose Moran amesema kupitia ubia huo na Chanzi wamekuwa wakifanya nao kazi kwa kuwapatia taka wanazozalisha na kwamba imekua faraja kwao kuona taka hizo zinapewa thamani.
"Muhimu zaidi ni kwamba hii imekuwa ni msaada kwa jamii pia katika kupambana na changamoto ya taka kupitia teknolojia waliyonayo Chanzi," amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya bia ya TBL, Jose Moran dunia inakabiliwa na tatizo la kimazingira ambalo upotevu wa chakula hai uko juu sana.
Moran ameongeza kuwa ni jukumu la Kila mtu kujipa changamoto ili kupata suluhu za kiubunifu, ndio maana wameungana makampuni mbalimbali ili kutafuta suluhisho la taka katika jamii
"Tunafanya kazi kwa bidii, na washirika wetu kujenga ushirikiano huu na tungependa kushiriki hili na ninyi nyote, wadau wetu wa thamani, mfano wa Chanzi," amesema Moran.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa P4G, Robyn McGuckin, amesema, ushirikiano huo ni mfano mzuri wa jinsi ya kushirikiana kati ya sekta za umma na binafsi ili kuweza kuchangia mabadiliko ya nchi kupitia ufumbuzi unaopunguza utoaji wa kaboni na kutoa kazi zinazolipa vizuri katika jamii.
"Kwa mustakabali endelevu, tunahitaji kupitishwa kwa haraka na kuongeza usuluhishi wa hali ya hewa na kwa upande wetu P4G tumejitolea kusaidia ubia huu ili kuunga mkono biashara ambazo zinaweza kuwa endelevu kifedha," amesema McGuckin.