Prime
Kanali Kipingu: Mwanafunzi mtembea peku aliyeacha alama jeshini
Muktasari:
- Akiwa na miaka minane mwaka 1960, alianza elimu ya msingi katika Shule ya Magunga iliyokuwa chini ya mfumo wa misheni.
Dar es Salaam. Kutoka kijijini Magunga hadi kufikia nafasi ya kuwa mwanzilishi wa shule za jeshi, mtaalamu wa mizinga na kiongozi wa taasisi za elimu zilizojenga historia nchini, safari ya Kanali mstaafu Iddi Kipingu ni mfano wa kipekee wa uvumilivu na mafanikio. Kipingu, aliyezaliwa Machi 16, 1952, anasema misingi ya maisha yake ilijengwa tangu utotoni akiwa chini ya malezi ya bibi yake mzaa baba, aliyemfundisha umuhimu wa nidhamu, uwajibikaji na kuthamini elimu.
Akiwa na miaka minane mwaka 1960, alianza elimu ya msingi katika Shule ya Magunga iliyokuwa chini ya mfumo wa misheni.
Hata hivyo, kabla hata ya kuanza masomo rasmi, tayari alikuwa na uhusiano wa karibu na shule hiyo kutokana na kipaji chake cha mpira wa miguu.
Jambo hili lilimfanya awe karibu na mazingira ya elimu tangu mwaka 1959 ambapo alikuwa akienda kucheza soka kila siku shuleni hapo hadi alipoandikishwa rasmi kuanza darasa la kwanza mwaka uliofuatia.
Safari yake haikuwa rahisi hata kidogo; alilazimika kutembea kilomita tano kwenda shuleni na kilomita nyingine tano kurudi nyumbani kila siku, mara nyingi akiwa pekupeku kutokana na familia yake kutokuwa na uwezo wa kumnunulia viatu.
“Bibi yangu hakuwa na uwezo wa kuninunulia viatu, hivyo ilikuwa kawaida kwenda shule peku,” anasema.
Mbali na changamoto hiyo, hata suala la kuonekana nadhifu lilihitaji ubunifu mkubwa kutokana na hali ya maisha. Mafuta ya ngozi yalikuwa bidhaa ya gharama ya juu wakati huo, hivyo bibi yake aliyekuwa akitengeneza vitumbua alimpa mafuta aliyotumia kwenye biashara yake hiyo ili ajipake mwilini.
“Ili nionekane smart, bibi alikuwa akinipaka mafuta ya vitumbua, mafuta ya ngozi yalikuwepo lakini yalikuwa ghali sana,” anasema.
Licha ya changamoto hizo zote, mazingira hayo magumu yalimjenga na kumpa hamu kubwa ya kusoma.
Akataa ajira ili asome
Mwaka 1966 alipohitimu elimu ya msingi, Kipingu alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza nchini kumaliza darasa la saba baada ya mfumo wa elimu kubadilika kutoka darasa la nane hadi la saba.
Wakati huo, wahitimu wa elimu ya msingi walikuwa na nafasi kubwa ya kupata ajira serikalini, tofauti na hali ya sasa. Wengi kijijini kwao walitarajia angeingia kazini, lakini yeye aliamua kuendelea na masomo ya sekondari.
“Tulipomaliza darasa la saba nilipata ajira, lakini nilikataa kwa sababu nilikuwa na ndoto ya kuendelea na masomo,” anasema.
Uamuzi huo uliwashangaza wengi, lakini ulimpeleka katika Shule ya Sekondari Magamba, Lushoto mwaka 1967. Wakati huo nafasi za kuingia sekondari zilikuwa chache sana, na wanafunzi watatu pekee ndiyo walipata nafasi hiyo kutoka kijijini kwao, akiwamo yeye.
Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari Milambo, Tabora kwa masomo ya kidato cha tano na sita kabla ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makutupora mwaka 1973.
Kipaji chake cha mpira wa miguu na riadha kiliendelea kumfungulia milango tangu shule ya msingi hadi sekondari ambako aliwakilisha mkoa kwenye mashindano ya Umisseta.
Akiwa JKT Makutupora, uwezo wake ulimfanya kuitwa kwa dharura kupitia radio call ya polisi Korogwe ili kuripoti kambini haraka kuchezea timu ya jeshi iliyokuwa ikitetea ubingwa wa Kombe la CCM.
“Niliitwa haraka kwa sababu walijua uwezo wangu wa mpira,” anasema Kipingu, akiamini michezo ilimfundisha nidhamu na uvumilivu.
Mwaka 1977, baada ya kuhitimu Shahada ya Sanaa na Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alijiunga rasmi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Siku aliyomaliza mtihani wake wa mwisho, gari la jeshi lilikuwa likimsubiri.
“Waliniambia nafasi yangu jeshini ipo inanisubiri. Walijua uwezo wangu darasani na uwanjani,” anasema.
Akiwa bado kijana mpya jeshini mwenye cheo cha Luteni, alikumbana na jukumu zito la kwenda kwenye Vita ya Kagera. Akiwa sehemu ya kikosi cha mizinga, walilazimika kupata mafunzo ya haraka usiku na mchana kwa wiki tatu tu badala ya miezi sita. Wakati huo walitegemea ramani, dira na mahesabu ya umbali badala ya teknolojia ya sasa.
“Katika mizinga, kosa dogo linaweza kugharimu maisha ya askari wengi, hivyo ilihitajika umakini na nidhamu ya hali ya juu,” anasema.
Hali hiyo ilimpa mtihani mkubwa wa kifamilia....“Niliondoka na kuacha mke wangu ametoka kujifungua, ilikuwa ni ngumu kwangu, lakini lazima nikawajibike, tulipofika Kagera nilikabidhiwa mizinga yangu sita, tayari kwa mapambano,” anasema.
Baadaye jeshini, akiwa na cheo cha kapteni alilazimika kuwafundisha wakubwa zake wenye cheo cha umeja kozi ya Junior Command and Staff. Jukumu hili alilifanya kwa ustadi mkubwa, na kujituma kwake kulimwezesha kupanda madaraja hadi kufikia ngazi ya juu ya Kanali.