Kapteni wa jeshi kortini, adaiwa kuingilia mfumo wa kompyuta

Kapteni wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Exavery Mroso akitoka kwenye chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Pamela Chilongola.

What you need to know:

  • Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), Kapteni Exacery Mloso kutoka kikosi cha  603 KJ cha Anga, Kituo cha  Banana, Dar es Salaam amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuingilia mfumo wa kompyuta na kubadilisha neno la siri.

Dar es Salaam. Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kapteni Exacery Mloso kutoka kikosi cha 603 KJ cha Anga, Kituo cha Banana, Dar es Salaam amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la kuingilia mfumo wa kompyuta na kubadilisha neno la siri.

Akisoma hati ya mashtaka leo Jumatano Juni 7, 2023 Wakili wa Serikali, Erick Davies alidai mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la kuingilia mfumo wa data za kompyuta na kuzuia matumizi ya data hizo.

Davies alidai kati Februari 11, 2023 akiwa ndani ya Jamhuri ya India, kwa makusudi kupitia mfumo wa kompyuta, aliingilia akaunti ya Instagram iitwayo mamakajatz kwa kubadili barua pepe ya [email protected] kwenda za[email protected] huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Katika shtaka lingine inadaiwa kuwa tarehe hiyo na maeneo hayo mshtakiwa huyo aliingilia mfumo wa data wa kompyuta wenye jina la Hashim Ally Mubi, Jerson Brown na Steven Magombeka kwa kubadilisha neno la siri akaunti ya Instagram kutoka mama2022 kwenda mamakaja 1321 huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Shtaka la mwisho inadaiwa kuwa tarehe hiyo akiwa ndani ya Jamhuri ya India mshtakiwa huyo alizuia data za kompyuta kwa kuwazuia viongozi wa utawala wa akaunti ya Instagram ya mamajaztz ambao ni Hashim Ally Mubi, Jerson Brown na Steven Magombeka kwa kubadilisha neno la siri la akaunti hiyo kutoka mama2020 kwenda mamakaja 1321 huku akijua ni kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa alikana makosa yote na upelelezi bado haujakamilka.

Hakimu Mkazi Mkuu Rhoda Ngimilanga amesema mshtakiwa huyo anatakiwa awe na wadhamini wawili mmoja ambao wanatakiwa kuwa na vitambulisho vinayotambulika pamoja na barua kutoka Serikalini.

"Wadhamini hao wawe wanatoka Jiji la Dar es Salaam ambao watasaini bondi ya Sh5 milioni," amesema Ngimilanga.

Mstakiwa huyo ameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti hayo na shauri hilo limeahirishwa hadi Juni, 21 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.